STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, July 18, 2014

Miili 100 yaokotwa ajali ndege 'iliyodunguliwa' Ukraine


Mabaki ya miili zaidi ya 100 yameokotwa jirani na eneo ilipoanguka ndege ya Malaysian Airlines kule Grabovo jirani na mpaka wa Ukraine na Urusi . 

 
Reuters iliripoti mapema Alhamisi kuwa ndege hiyo yenye namba MH17 ilianguka jimboni Donetsk ikiwa njiani kuelekea Kuala Lumpur ikitokea mjini Amsterdam, Uholanzi.
 
Kuna taarifa zisizo rasmi kuwa ndege hiyo ‘imetunguliwa’ na aidha majeshi ya Ukraine, ama waasi wanaoiunga mkono Urusi, vyanzo mbalimbali vya habari vimeripoti.
 
Waokoaji wamesema miili imeokotwa katika eneo la umbali unaozidi kilometa 15 toka ndege ilipoanguka.
 
“Hatuwezi kuthibitisha kama ndege hiyo imetunguliwa ama la,” alisema Rais wa Ukraine Petro Poroshenko.
 
“Hata hivyo, tunasisitiza kuwa Ukraine haijarusha makombora yoyote angani leo,” aliongeza.
 
Katika taarifa iliyotolewa mapema leo, Malaysian Airlines ilidai ilipoteza mawasiliano na ndege hiyo mnamo saa 8 na dakika 15 GMT.
 
Tovuti ya The Guardian inaripoti kuwa vyanzo toka ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ukraine vinadai ndege hiyo ilitunguliwa na kombora toka mfumo wa kurusha roketi hewani unaojulikana kama BUK.
 
Teknolojia ya BUK ilikuwa maarufu sana Urusi miaka ya 1970, na ilirithiwa na bado yaendelea kutumika na zile zilizokuwa Jamhuri za Kisovieti, ikiwamo Ukraine.
 
Wachambuzi sasa wanahoji walorusha kombora hilo wamelipataje, huku baadhi wakidai hiyo ni uthibitisho tosha kuwa waasi wanaoiunga mkono Urusi wako nyuma ya ‘shambulizi’ hilo.
 
Kati ya watu 295 walokuwa ndani ya ndege hiyo aina ya Boeing 777, 280 walikuwa abiria na walobaki ni wahudumu na marubani.
 
Picha zilizotupwa katika mitandao ya kijamii na tovuti mbalimbali zinaonyesha masalia ya ndege hiyo yenye rangi za bluu na nyekundu yakifuka moshi.


Picha hizo zimeamsha hisia kali, zikiukumbusha umma kuhusu ajali nyingine inayohusisha ndege ya Malaysia namba MH370 ilopotea toka Machi, huku ikiwa haijaonekana.
 
Mataifa mbalimbali yanaendelea na jitihada za kutathmini kama raia wake walikuwamo ndani ya ndege ‘ilotunguliwa,’ huku baadhi ya mashirika ya ndege, ikiwemo Emirates, Lufthansa, British Airways na Aeroflot, yakisitisha safari zote kwenya anga la Ukraine.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment