KLABU ya Liverpool ni
moja ya vilabu kadhaa vinavyotarajiwa kufanyiwa uchunguzi kama wamekiuka
Sheria ya Matumizi ya Fedha-FFP.
Kwa mujibu wa sheria za Shirikisho la
Soka barani Ulaya-UEFA vilabu vyote barani humo vinapaswa kuweka kikomo
cha hasara kutofikia paundi milioni 35.4 kwa misimu miwili.
Kuna adhabu
hutolewa kwa wasiotimiza masharti hayo ambapo Manchester City tayari
wameshakumbana nayo kwa kutozwa faini na kuwekewa kiwango cha matumizi
katika usajili na kupunguziwa idadi ya wachezaji katika kikosi chake Mei
mwaka huu.
Lakini pamoja na kupata hasara ya paundi milioni 49.8 katika
msimu wa mwaka 2012-2013 na paundi milioni 41 msimu wa mwaka 2011-2012,
Liverpool wana uhakika wanaweza kuvuka kikwazo hicho bila
adhabu.
Liverpool sambamba na Monaco, Inter Milan na AS Roma
ambazo zote hazikushiriki michuano ya Ulaya msimu uliopita tayari
zimepeleka taarifa za akaunti zao Bodi ya Udhibiti wa Fedha ya
Klabu-CFCB lakini kuna uwezekano wa kuagizwa kupelekea maelezo zaidi
kuhusu fedha hizo.
Msimu uliopita vilabu 76 viliingia katika uchunguzi
wa FFP lakini vilabu tisa pekee ndio vilipewa adhabu kwa kukiuka sheria
hiyo.
No comments:
Post a Comment