CRISTIANO Ronaldo alifunga magoli manne katika ushindi wa Real Madrid wa 5-1 dhidi ya Elche katika Ligi Kuu ya Hispania juzi na kuwa 'hat-trick' yake ya 25 kwa Real Madrid.
Ilikuwa ni 'hat-trick' ya pili katika siku tatu baada ya kufunga magoli matatu katika ushindi wa 8-2 dhidi ya Deportivo la Coruna Jumamosi.
Ronaldo ndiye aliyesababisha penalti iliyowapa Elche goli la kuongoza baada ya kuukosa mpira na kumpiga teke Pedro Musquera wakati akijaribu kuokoa kutokea ndani ya boksi la Madrid. "Licha ya kwamba nililalamika kwa refa, ilikuwa ni penalti. Ni lazima niwe mkweli. Alikuja ghafla, lilikuwa ni shambulio ambalo sikulitarajia. Yalikuwa ni maamuzi sahihi ya refa," alisema Ronaldo.
"Nimefunga magoli manne katika mechi moja mara mbili ama tatu. Nina furaha mpira (wa 'hat-trick' nampelekea mwanangu," alisema.
'Hat-trick' hiyo ya 25 inamfanya kubakisha tatu kumfikia Alfredo di Stefano anayeshikilia rekodi ya Real Madrid ya kufunga 'hat-trick' 28. Pia ilikuwa ni ya 21 katika La Liga pekee, moja nyuma ya vinara wanaoshikilia rekodi, Di Stepano na Telmo Zarra, gwiji wa Athletic Bilbao.
Ronaldo tayari msimu huu amefunga magoli 13 katika michuano yote na kufikisha mabao 264 tangu ajiunge na Madrid, hivyo kubakisha magoli 59 kumfikia mshikarekodi wa zama zote klabuni hapo Raul aliyefunga magoli 323. Na kwa kuwa Madrid wana mechi 56 zilizobaki msimu huu, huenda akaivunja rekodi hiyo 2014-15.
No comments:
Post a Comment