STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, January 24, 2015

Serikali yalaani ubaguzi aliofanyiwa Tambwe mechi ya Ruvu

Amissi Tambwe (wa Tano toka Kulia) akichuana kwenye mechi yao na Ruvu Shooting ambapo alilalamika kubaguliwa na kukabwa na George Assey (wa kwanza kulia) katika pambano lililoisha kwa sare ya 0-0
WIZARA ya Habari Utamaduni na Michezo imeliagiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutoa adhabu kwa timu ya Ruvu Shooting kutokana na kitendo cha ubaguzi kilichofanywa na wachezaji wa timu hiyo dhidi ya mshambuliaji wa Yanga kutoka nchini Rwanda, Amissi Tambwe.
Akizungumza na Ripota wa Globu ya Jamii, Naibu Waziri wa Habari, Juma Nkamia amesema kuwa TFF isikae kimya kutokana na matamshi ya udhalilishaji juu ya Tambwe na kuiagiza TFF kuchukua hatua za kinidhamu haraka iwapo itathidibitika mshambuliaji huyo alitolewa maneno hayo ya udhalilishaji ili iwe fundisho kwa wengine.
"Hakuna nchi yoyote duniani inayopenda vitendo vya ubaguzi, kitendo ambacho upendi kufanyiwa usimfanyie mwenzie, nimesikia malalamiko ya Tambwe kama ni kweli Ruvu Shooting wamemuita mkimbiza wajue sio kitu kizuri tena wale ni jeshi, nadhani wanajua madhara ya vita.
"Wenzetu Burundi hawakupenda kuingia vitani, hakuna nchi yoyote inayopenda kuwa vitani, vita ni mbaya hata hapa inaweza kutokea, ni jambo la kumshukuru Mungu mpaka leo mna amani, uwezi kujua mtu unayemwambia ameumia kiasi gani na hiyo vita ni ndugu wangapi au marafiki wangapi amewapoteza sio kitu kizuri, naiagiza TFF ishugulikie suala hili kwa kuchukua hatua za haraka."alisisitiza Nkamia.
Kauli ya Nkamia imekuja siku moja baada ya Tambwe kulalamikia kitendo cha kuitwa mkimbizi na wachezaji wa Ruvu Shooting wakiongozwa na George Michael ikiwa ni pamoja na kumkaba nusura wamtoe roho.
"Maneno makali waliyonitamkia yananiuma sana roho hadi sasa, wameniita mkimbizi, eti nimekimbia vita nyumbani Burundi, vita hata hapa inaweza kutokea, hakuna anayependa mabaya kama hayo yatokee, kumwambia mtu haujui kapoteza ndugu wangapi, si sahihi kabisa, cha kushangaza wale ni wanajeshi lakini hawaonyeshi kuwa wanajua athari za vita." kauli iliyotolewa na Tambwe jana.
Hata hivyo Chama cha Waamuzi nchini (FRAT), kimetangaza kumfungia mwamuzi wa kati wa mchezo huo Mohamed Theofil, huku ikiwaweka kwenye uchunguzi waamuzi wasaidizi Michael Mkongwa na Yusuf Sekile.
Mwenyekiti wa FRAT, Salum Chama aliiambia Globu ya Jamii kuwa wamefikia uamuzi wa kumsimamisha Theofil baada ya ripoti ya Kamisaa kuonyesha kuna mapungufu yaliyofanywa na mwamuzi huyo ambaye katika mchezo huo uliomalizika kwa suluhu, alishindwa kumudu mchezo kutokana na rafu za mara kwa mara kitendo kilicholazimu mpira kusimama kila dakika.
"Ripoti ya kamisaa imeonyesha kuna udhaifu mkubwa uliofanywa na mwamuzi, kamati yangu imemfungia kupisha uchunguzi, na bado tunaendelea na uchunguzi pia kwa waamuzi wasaidizi, kikao cha kamati yangu kitakaa Februari 6 kuwajadili na kuangalia adhabu stahiki itakayofaa.
"Kitendo kinacholalamikiwa sana ni kile cha Tambwe, na ni kweli kila mtu ameona, hata kama ripoti ya kamisaa isingesema tungechukua hatua kwa sababu wapo viongozi wa TFF walioona, tunachunguza ripoti ya mechi asesa, kamisaa,"alisema Chama.
Hata hivyo, Chama alisema kuwa hawafanyi kazi kwa shinikizo la Yanga ambao waliwapa mpaka Jumamosi wawe wameshatoa adhabu kwa waamuzi wa mchezo wao na Ruvu Shooting la sivyo watagomea Ligi.
Kwa hisani ya Michuzi blog

No comments:

Post a Comment