STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, January 12, 2017

SIMBA, AZAM NI ZAIDI YA VITA KOMBE LA MAPINDUZI 2017

Kikosi cha Simba
Wababe wa Chamazi, Azam FC
Na Rahma White
HABARI ndio hiyo. Leo Alhamisi ndio kilele cha sherehe za Mapinduzi, ukiwa ni mwaka wa 53, lakini kazi bwana ipo kesho kwenye Uwanja wa Amaan.
Unajua nini? Wekundu wa Msimbazi, Simba kesho itavaana na Matajiri wa Azam kwenye pambano la fainali za michuano ya Kombe la Mapinduzi 2017.
Sasa kama ulikuwa haujui ni kwamba Simba ndio klabu iliyotwaa Kombe la Mapinduzi mara nyingi, ikifanya hivyo mara tatu tangu lianze kuchezwa kwa mfumo wa sasa. Pia Simba ndio klabu iliyotinga mara nyingi kwenye fainali  ambapo pambano lao la kesho dhidi ya Azam litakuwa ni la sita sita ikiiacha Mtibwa Sugar waliokuwa wakilingana nao ambayo msimu haikualikwa.
Vinara hao wa Ligi Kuu Bara kesho itavaana na Azam klabu inayofuata kwa kulibeba taji hilo mara nyingi nyuma ya Simba, ikilitwaa mara mbili tena ikiwa klabu pekee kuwahi kulitetea ikifanya hivyo mwaka 2012 na 2013.
Simba imefika hatua hiyo ya fainali za mwaka huu kwa kuitambia Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya kumaliza dakika 90 la pambano lao bila milango ya timu hiyo kuguswa, huku Azam ikifika hatua hiyo kwa kuing'oa Taifa Jang'ombe kwa bao 1-0.
Azam ndio klabu ambayo mpaka inafika fainali wavu wake haujaguswa ikiweka rekodi, huku Simba ikifuata ikiruhusu bao moja tu.
Kwa mnasaba huo fainali ya kesho itakuwa tamu ile mbaya kwani, licha ya kila timu kusaka heshima ya kulibeba taji hilo, lakini pia zinataka kuonyesha nani mkali zaidi katika suala zima la kulinda lango lao.
Mchezo huo wa kesho una uhondo zaidi kwenye eneo la kiungo ambako klabu zote zinatambia mafundi walionao ambao wamezifanya kuwa kali katika kuzuia na kushambulia.
Makocha wa pande zote wamekuwa wakijinasibu timu zao kuibuka na ushindi, lakini kwa kulinganisha na rekodi zilizopo ni lazima Simba iwe makini mbele ya Azam ambao waliistaajabisha Yanga kwa kuipiga mabao 4-0.
Ingawa mpaka sasa kwenye michuano hiyo ya Mapinduzi, Azam imekuwa wanyonge wa Simba, lakini kwa namna walivyoizima Yanga ni wazi Simba isiende kichwa kichwa Uwanja wa Amaan kama wanataka kurejesha taji lao hilo walilolipoteza mwaka jana na kuliacha likibebwa na URA ya Uganda.
Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja amekiri pambano litakuwa gumu, lakini kubwa wanachotaka ni kurudi jijini Dar es Salaam na taji hilo, huku Idd Nassor 'Cheche' akiamini hakuna cha kuwazuia kubeba Kombe la mwaka huu.
Vikosi vya timu hizo vinatarajiwa kuwa hivi;
AZAM: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gadiel Michael, Yakub Mohammed, Aggrey Morris, Stephan Kingue, Salum Abubakar, Frank Domayo, John Bocco, Yahya Mohammed na Joseph Mahundi.
SIMBA:
Daniel Agyei, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein, Abdi Banda, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Mzamiru Yasin, Juma Liuzio, Mohammed Ibrahim na James Kotei.

Mabingwa wa Mapinduzi

2007-Yanga
2008-Simba
2009-Miembeni
2010-Mtibwa Sugar
2011-Simba
2012-Azam
2013-Azam
2014-KCCA
2015-Simba
2016-URA
2017-  ''

No comments:

Post a Comment