STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, January 12, 2017

Utamu wa Ligi Kuu Bara umerudi tena

JKT Ruvu
Toto Africans
Ruvu Shooting
Na Rahim, Junior
ACHANA na pambano la kesho la fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi,
itakayozikutanisha Simba na Azam kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, unaambiwa utamu wa Ligi Kuu Bara nao unarudi rasmi wikiendi hii.
Ligi hiyo iliyokuwa mapumziko ya wiki kama mbili hivi, inarudi kwa michezo itakayochezwa mfululizo kuanzia leo mpaka Jumatano.
Wapinzani wa jadi, maafande wa JKT Ruvu na Ruvu Shooting zinatarajiwa kumaliza ubishi katika pambano linalosubiriwa kwa hamu kwenye Uwanja wa Mabatini, ulioko Mlandizi mkoani Pwani.
Pambano hilo la kisasi linafanyika huku kila timu ikiwa katika hali tofauti, JKT Ruvu wakiwa hoi mkiani, huku wapinzani wao angalau wakipumua maeneo ya juu na wanatambia ushindi wa bao 1-0 iliyopata katika mechi yao ya kwanza.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ligi hiyo itaendelea Jumamosi kwa pambano jingine la 'derby' ya Mkoa wa Shinyanga kati ya Stand United na Mwadui  zitakazovaana kwenye Uwanja wa Kambarage mjini humo, huku kukiwa hakuna mbabe wa mechi ya awali.
Jumamosi pia kutakuwa na mtanange mwingine mkali wa Kagera Sugar itakayokuwa mwenyeji wa Ndanda ya Mtwara kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Utamu utaendelea tena Jumapili kwa mchezo mmoja tu ambapo Mbao itaialika African Lyon ya Dar kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Kivumbi cha ligi hiyo inayoingoa raundi ya nne ya duru la pili, itaendelea tena Jumatatu kwa mchezo mmoja tu kati ya Prisons Mbeya itakayokuwa mgeni wa Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Michezo mitatu ambayo ilikuwa haijapangiwa tarehe hapo awali kwa alama ya TBA ikiwa na maana ya kutajwa baadaye (To Be Announced), tayari Bodi ya Ligi, chombo cha TFF, kinachosimamia na kuendesha ligi, imepanga tarehe.
Jumanne ya Januari 17, 2017, Yanga itakuwa ugenini mjini Songea kuvaana na Majimaji kwenye Uwanja wa Majimaji na siku inayofuata yaani Jumatano, Mtibwa Sugar itakayocheza na Simba kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro wakati Azam itakuwa mwenyeji wa Mbeya City Uwanja wa Azam Complex.
Mchezo huu wa Azam na Mbeya City umepangwa kuanza saa 1.00 usiku wakati michezo yote tajwa hapo juu itaanza saa 10.00 jioni lengo likiwa ni kutoa nafasi kwa mashabiki kushuhudia mechi nyingi kupitia Kituo cha runinga cha Azam.

Ratiba ya VPL imekaa hivi;
 
Jan 13, 2017   
JKT Ruvu v Ruvu Shooting

Jan 14, 2017Stand United v Mwadui
Kagera Sugar v Ndanda

Jan 15, 2017Mbao v African Lyon

Jan 16, 2017
Toto Africans v Prisons

Jan 17, 2017Majimaji v Yanga

Jan 18, 2017Mtibwa Sugar v Simba
Azam v Mbeya City
 

No comments:

Post a Comment