STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, July 17, 2013

Mganga wa Jadi Tanzania agundua dawa ya Ukimwi, NIMR kuijaribu


Na Suleiman Msuya
TAASISI  ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) imesema ipo kwenye majaribio ya dawa ya kudhibiti virusi vya Ukimwi ambayo imegunduliwa na imewasilishwa kwenye taasisi hiyo na mmoja wa waganga wa jadi wa hapa nchini.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Kuratibu na Kukuza Utafiti NIMR Dk. Julius Massaga wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Habari Maelezo jijini Dar es Salaam.
Dk. Mssaga alisema mganga huyo wa jadi aliyegundua dawa hiyo ambayo imepewa jina la warburgistat aliitunza katika vifungashio vya kawaida ambapo NIMR wao wameweza kufanyia maboresho kwa kuitengenezea kwenye mfumo wa vidonge.
Alisema kulingana na taarifa za Mganga huyo wagonjwa 20 wa awali ambao walitumia dawa hiyo wamepona kabisa na hamna madhara yoyote ambayo yamepatikana.
"Tunapenda kuwaambia watanzania kuwa ipo dawa ya kudhibiti virusi vya ukimwi ambayo iliwasilishwa NIMR na baada ya kuifanyia uchunguzi tunapata matumaini kuwa inaweza kufanya kazi hiyo,'' alisema.
Mkurugenzi huyo wa Kuratibu na Kukuza Utafiti NIMR alisema dawa hiyo wameiwasilisha  Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ambapo wanatarajia baada ya uchunguzi wataingiza sokoni ili iweze kutumika rasmi.
Alisema NIMR imekuwa ikishirikiana na nchi zingine mbalimbali kama Afrika Kusini na Swaziland katika kufanya utafiti dhidi ya dawa asili ambazo zimekuwa zikileta matokeo makubwa kwa jamii.
Dk. Massaga alisema NIMR inawakaribisha waganga wa jadi ambao wana amini kuwa wana dawa ambazo  zinaweza kusaidia jamii ili wao waweze kuzifanyia utafiti kwa uthibitisho zaidi.
Mkurugenzi huyo alisema pamoja na dawa hiyo pia wamefanikiwa kuboresha dawa za tiba asili kwa ajili ya matumizi ya binadamu kama vile TMS 2001 tiba ya malaria, hepacure inatibu ini, persician tiba ya kisukari, persivin tiba ya tezi dume, nimrex tiba ya kikohozi na nimrevit kinywaji kinachoboresha afya ya kuongeza damu.
Pia alizitaja dawa zingine ni mundex dawa ya kuongeza nguvu jinsia ya kiume, fukuza mbu dawa ya kupakaa inayofukuza mbu,usambara balm dawa ya kupaka kwa ajili ya kutuliza homa na mafua,usambara mosquito repellent mshumaa unafukuza mbu na takasa maji tiba ya maji ya kunywa dhidi ya vimelea vya magonjwa yakiwemo ya kuhara na homa ya matumbo.
Kwa upande mwingine Dk. Massaga alisema NIMR inakabiliwa na changamoto mabalimbali kama kukosekana kwa uhamasishaji na uwezeshaji katika eneo la kilimo cha miti dawa hali ambapo inasababisha ukosefu wa dawa asili.
Changamoto nyingine ni kukosekana na mitaala ya wataalamu wa tiba ya kisasa (madaktari, wafamasia na manesi) ambao wamenyimwa fursa ya kuelewa kwa kina na kupata maarifa juu ya tiba asilia na matumizi yake katika tiba.
Aidha changamoto nyingine ni uhusiano mdogo kati ya watafiti, wataalamu wa tiba asilia na tiba ya kisasa katika suala zima la tiba asili na kutokuwepo kwa orodha ya miti dawa na taarifa ya matumizi yake katika tiba na maingiliano yake na dawa za kisasa.
Dk. Massaga alisema pamoja na changamoto hizo NIMR inatarajia kusajili dawa na kiwanda kabla ya uzalishaji katika mwaka huu wa fedha, kuanzisha uzalishaji wa kati wa dawa za asili kulingana na mahitaji na kuuingiza dawa asali katika mfumo wa tiba.
Hata hivyo alisema katika mwaka wa fedha wa 2013/14 serikali imetenga kiasi cha sh800 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuboresha tiba asilia pamoja na mitambo ya kuzalishia dawa hizo.
Ambapo kwa sasa serikali imeikabidhi NIMR mitambo midogo ya daraja la kwanza ya utendenezaji wa dawa asili kwa matumizi ya binadamu na kujenga kiwanda cha daraja la kwanza cha kisasa kwa ajili ya utafiti na utengenezaji wa tiba asili katika eneo la Mabibo jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Mtafiti Mwandamizi wa NIMR Hamis Malebo alitoa wito kwa wananchi kuwa makini na ongezeko la baadhi ya watu ambao wanajiita waganga wa jadi.
Alisema kwa muda sasa hasa katika jiji la Dar es Salaam kumekuwepo na ongezeko kubwa la watu wa aina hiyo hali ambayo inahatarisha maisha ya wananchi ambao wamekuwa wakitumia dawa hizo.
"Jamani kuweni makini wapo watu (matapeli) ambao wapo tayari hata kutumia mapumba ya mbao kuwapa watu kama dawa jambo ambalo si sahihi hata kidogo," alisema.

1 comment: