MECHI ya marudiano kati ya timu ya soka ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) dhidi ya wenyeji wao Uganda (The Cranes) ambayo ni ya kusaka tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani (CHAN) itafanyika Julai 27 kwenye Uwanja wa Mandela jijini Kampala imeelezwa jana.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Angetile Osiah, alisema jana kuwa Chama cha Soka cha Uganda (FUFA) kimesema kwamba mchezo huo utachezwa jioni na maandalizi yake yanaendelea vizuri.
Osiah alisema kuwa katika kujiandaa na mchezo huo, Stars ilielekea Mwanza tangu Jumapili asubuhi kuweka kambi na itaondoka nchini kuelekea Kampala Julai 24 mwaka huu.
Alimtaja mchezaji, Mudathir Yahya, kuwa ameshachukua nafasi ya kiungo, Mwinyi Kazimoto, ambaye ametoroka katika kambi ya Taifa Stars tangu Jumamosi usiku na kuelekea Qatar kusaka klabu ya kuichezea soka la kulipwa.
"Safari hii timu itaanzia safari yake Mwanza kwenda Kampala na haitarudi Dar es Salaam kuanzia safari yake," alieleza Osiah.
Stars ilifungwa goli 1-0 dhidi ya Uganda katika mechi yake
ya kwanza iliyofanyika nchini ambapo wadau wengi wa mchezo huo akiwamo Rais wa TFF, Leodegar Tenga, walielezea kusikitishwa na kiwango kibovu kilichoonyeshwa na kikosi hicho.
Hata hivyo, Tenga alisema kuwa huu ni wakati wa kuwapa moyo wachezaji wa Taifa Stars na anaamini wana uwezo wa kuifunga Uganda nyumbani kwao na kusonga mbele lakini ni lazima wajiamini.
Bao pekee ya Uganda inayofundishwa na Mserbia Sredojevic Milutin 'Micho' lilifungwa na Denis Iguma katika dakika ya 47 ya mchezo huo wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.
Mshindi kati ya Stars na The Cranes atafuzu kushiriki katika fainali za tatu za CHAN zitakazofanyika Afrika Kusini mapema mwakani.
Tayari wenyeji Afika Kusini (Bafana Bafana) na Ghana wameshakata tiketi ya kushiriki fainali hizo.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment