Bondia Francis Cheka |
Cheka na Mmarekani huyo wanatarajiwa kuvaana Agosti 30 kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee kuwania mkanda wa WBF katika mchezo wa raundi 12 uzito wa Super Middle (kilo 75).
Hata hivyo, kuna taarifa kwamba Cheka anayeshikilia taji la Mabara la IBF atapanda ulingoni mwanzoni mwa Agosti dhidi ya Mmalawi Chimwemwe Chiotcha katika pambano lisilo la ubingwa.
Hata hivyo, Rais wa TPBO, Yasin Abdallah 'Ustaadh', alisema kwa mujibu wa mkataba na taratibu za ngumi, Cheka hawezi kucheza mapambano mawili ndani ya mwezi mmoja na hivyo kutoa tahadhari mapema.
Ustaadh alisema Cheka alishasaini mkataba wa pambano hilo dhidi ya Mmarekani tangu Mei mwaka huu na kwa taratibu ndani ya mwezi mmoja hawezi kupigana pambano jingine la sivyo yatamkuta kama ya Karama Nyilawila.
Nyilawila aliyekuwa bingwa wa WBF, alipoteza mkanda wake kutokana na ratiba ya pambano lake la utetezi kuingilia na mechi isiyo na mkanda dhidi ya Cheka mapema mwaka jana.
"TPBO tunahofia yasitokee yaliyotokea kwa Nyilawila, Cheka alisaini mkataba tangu Mei kwa ajili ya pambano hilo, hivyo wanavyoibuka watu na kusema kuwa bondia huyo atapigana na Mmalawi ndani ya mwezi huo ni kutaka kuvuruga pambano hilo la kimataifa ambalo litamsaidia kumtangaza Cheka," alisema.
Alisema kama kuna watu wanataka kumsaidia Cheka wamlete Chiotcha ili ampe mazoezi katika kambi yake kujiandaa na pambano hilo la WBF au wasubiri akishapigana na Mmarekani.
Ustaadh alisema imefika wakati wadau wa ngumi washirikiane kuwasaidia mabondia wao kufanya vyema kwenye mechi za kimataifa ili kurejesha heshima katika mchezo huo hasa yanapokuwapo na mapambano yanayotambuliwa duniani.
Aliongeza Chiotcha ni bondia hatari hivyo kama atapigana na Cheka katika kipindi kilichotangazwa anaweza pengine kumjeruhi Cheka na hivyo kushindwa kupigana na Derrick.
Aliongeza siku ya pambano hilo la Cheka na Derrick, mabondia Mada Maugo na Thomas Mashali wataonyeshana kazi kuwania mkanda wa WBF-Afrika, huku Alphonce Mchumiatumbo atapigana na De Andre McColl wa Marekani.
No comments:
Post a Comment