STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, February 15, 2013

Liverpool chali, Chelsea, Tottenham zapeta UEFA

gareth Bale akifunga moja ya mabao yake katika mec hi yao ya jana usiku

JAHAZI la timu ya Liverpool ya Uingereza limezidi kuzama baada ya usiku wa jana kukandikwa mabao 2-0 na Zenith, wakati timu zinazofukuzana kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England, Chelsea na Tottenham Hotspurs zikitakata kwa kushinda mechi zao za Ligi ya UEFA.
Liverpool inayochechemea kwenye ligi ya nyumbani ilipata kipigo hicho ugenini kwa magoli ya Hulk na Semak, huku nyota wake kutoka Uruguay, Luis Suarez akikosa mabao kadhaa ya wazi.
Katika mechi nyingine za michuano hiyo maarufu kama Europa ndogo, Chelsea ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Sparta Praha likitumbukizwa wavuni na Alex, huku Tottenham wakiwa nyumbani waliishinda Olympicque Lyonn ya Ufaransa mabao 2-1 yote yakifungwa na Garetht Bale.
Nao Newcastle United ilijikuta ikipata sare ya bila kufungana dhidi ya Metalist ya Ukraine huku ikinyimwa mabao mawili yaliyotumbukizwa wavuni na Msenegal, Bemba Cisse na kumfanya kocha Allan Pardew.
Matokeo mengine ya mechi hizo timu ya Samuel Et'oo, Anzhi Makhachkala ya Russia iliishindilia Hannover ya Ujerumani mabao 3-1, Et'oo akitupia moja,  Bate na Fenerbahce (0-0), Levante v Olympiiakos Piraeus (3-0), Dynamo Kyiv v Bordeaux (1-1), Bayer Leverkusen v Benfica (0-1), Ajax v Steaua Bucuresti (2-0), Napoli v Viktoria Plzen (0-3), Atletico Madrid v Rubin Kazan (0-2), Inter Milan v CFR Clui (2-0), Stuttgart v Genk (1-1), Dnipro Dnipropetrovsk v Basel (0-2) na Borrusia M'gladbach v Lazio (3-3).
Mechi za marudiano za michuano hiyo zinatarajiwa kuchezwa wiki ijayo kwenye viwanja tofauti kwa zile zilizokuwa ugenini kuhamia nyumbani na kinyume chake kwa zile zilizokuwa nyumbani kusafiri ugenini.









Sikinde yapata mdhamini ikijiandaa kwenda Marekani

Baadhi ya wanamuziki wa Sikinde wakiwajibika

WAKATI safari yao ya kwenda Marekani ikisubiri ujio wa mfadhili wao mwezi ujao, bendi kongwe ya muziki wa dansi nchini, Mlimani Park 'Wana Sikinde' imepata mdhamini kwa ajili ya kurekodi nyimbo zake.
Kwa mujibu wa Katibu wa bendi hiyo, Hamisi Milambo alimtaja mdhamini huyo kuwa ni Werner Grabner, raia wa nchi ya Ujerumani, ambaye atagharamia kazi ya kurekodi baadhi ya nyimbo mpya na za zamani za Sikinde kwa lengo la kuitangaza kimataifa.
Milambo alisema Mjerumani huyo atagharamia kazi ya kurekodi 'audio' na video kwa kile kilichoelezwa na wanasikinde kwamba amevutiwa na ukali wa bendi hiyo aliyokuwa akiifuatilia kwa muda mrefu bila Sikinde kufahamu.
Katibu huyo aliongeza kuwa neema hiyo imewaangukia wakati wakijiandaa kumpokea mfadhili wao mwingine kutoka Marekani kwa ajili ya kumalizia mipango yao ya kwenda nchini humo kutumbuiza na kurekodi.
Milambo alisema mfadhili huyo anatarajiwa kutua mwezi ujao ili kuweka mambo sawa kabla ya Sikinde kupaa kuelekea kwa 'Obama'.
"Safari yetu ya Marekani ipo kama tulivyoitangaza, tulikuwa tunasubiri kumalizana na mfadhili wetu atakayetua nchini mwezi ujao baada ya awali viongozi wenzetu kwenda kufanya mazungumzo ya awali nchini humo," alisema Milambo.
Aidha aliongeza bendi yao imenyakua wanamuziki wapya akiwemo mkongwe, Adolph Mbinga 'Mtuhumiwa' aliyeanza kuonekana kwenye maonyesho yao huku wengine walitarajiwa kutambulishwa katika maonyesho yao ya mwishoni mwa wiki.
Sikinde ilipata pigo kwa kupoteza baadhi ya nyota wake, mmoja akifariki na wengine watatu wakihamia kwa wapinzani wao Msondo Ngoma akiwamo Athuman Kambi.

HUSSEIN MACHOZI AMFANANISHA DIAMOND NA KUKU JIKE

HUSEIN MACHOZI
‘Addicted hit maker’ Hussein Machozi amefunguka kuhusu uhusiano wake na Diamond platnumz na kuonesha kuwa hawana urafiki hata kidogo, japo hakusema moja kwa moja kama wana uadui na kwamba yeye na Diamond ni kama ‘Jogoo na kuku Jike’ na yeye Hussein ndiye jogoo!


Hussein Rashid a.k.a Hussein Machozi amefunguka kwenye XXL ya Clouds fm katika segment ya U Heard, alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu tuhuma zilizowafikia ‘Timu Makorokocho’ kuwa Hussein Machozi alipigana na Diamond Platinumz huko Mombasa.


Japo Hussein alikiri kuwa anauwezo wa kupigana kama bondia, lakini alikanusha kabisa kuwa hajawahi kupigana na Diamond na wala hajawahi kuzinguana nae, kwa sababu hawajawahi kabisa kuwa karibu, na sababu ni kwamba wanatokea katika sayari tofauti kabisa, yeye anatokea sayari nyingine na hajui Diamond anatokea sayari gani.


Japo aliongea kwa ufupi sana lakini hii ilitoa picha ya moja kwa moja kuwa inawezekana Hussein ana kitu moyoni ama hasira flani kuhusu Diamond Platinumz. Je wewe unamtazamo gani kuhusu hili?


DIAMOND

SIMBA YATAMBA, LAZIMA LIBOLO IFE JUMAPILI TAIFA



MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage ametamba kuwa, kikosi chake kinao uwezo wa kutoa kipigo kwa wapinzani wao, Libolo ya Angola katika pambano lao la kwanza la Ligi ya Mabingwa Afrika litakalofanyika kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Rage amesema kwa kawaida, Simba huwa inabadilika inapocheza katika michuano ya kimataifa hivyo amewataka mashabiki wa timu hiyo wasiwe na wasiwasi kuhusu mechi hiyo.
Kauli ya Rage imekuja huku mashabiki wa klabu hiyo wakiwa na hofu na kikosi chao ambacho katika mechi za mwisho za duru la kwanza na mechi tatu za duru la pili walizocheza imekuwa na matokeo yasiyowafurahisha.
Akizungumza mjini Dar es Salaam jana, Rage alisema mabadiliko ya benchi la ufundi hayawezi kuiathiri Simba katika mechi hiyo kwa vile vijana wake wana ari kubwa ya kuonyesha maajabu.
"Ni kweli baada ya kumuondoa Milovan Cirkovic mfumo wa uchezaji umebadilika, lakini tumejipanga vyema kushinda mechi hiyo na sababu ya kufanya hivyo tunayo,"alisema.
Rage alisema wachezaji wote wapo katika hali nzuri na timu inatarajiwa kurejea Dar es Salaam kutoka Arusha, ambako ilikuwa imeweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo.
Kocha Msaidizio wa timu hiyo ambaye pia ni meneja, Jamhuri Kihwelu 'Julio' alitamba kwamba mashabiki wa soka hawapaswi kuwa na hofu na wajitokeze kwa wingi katika pambano lao la Jumapili wapate raha.
Hata hivyo Julio alisema ni kweli matokeo ya mechi zilizopita hazivutii, lakini soka ndivyo lilivyo na wao wamejipanga hasa baada ya kufanywa marekebisho kwa dosari zilizofanya timu yaoi isitakate katika mechi hizo za Ligi Kuu ikilazimishwa sare mbili mfululizo dhidi ya JKT Ruvu na JKT Oljoro.
Katika hatua nyingine viingilio vya pambano hilo la Wekundu wa Msimbazi na Waangola vimewekwa hadharani ambapo kiingilio cha chini katika mechi kati ya Simba na Libolo kitakuwa sh. 5,000
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, viingilio vingine vitakuwa sh. 10,000 kwa jukwaa la VIP C, sh. 15,000 VIP B na sh.30,000 VIP A.
Kamwaga alisema maandalizi kwa ajili ya mechi hiyo yanakwenda vizuri na tiketi zinatarajiwa kuanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo.

MAKALLA AIPONDA KAMATI YA MTIGINJOLA




NAIBU Waziri wa Habari, Vijana, Utamduni na Michezo, Amos Makalla, ameiponda Kamati ya Rufani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kitendo chake cha kumuengua Jamal Malinzi kuwania urais wa
shirikisho hilo.

Makalla amesema kitendo hicho kimemsikitisha kwa vile sababu zilizotolewa na kamati hiyo kuhusu uamuzi huo hazina msingi na zimeonyesha ubabaishaji mkubwa.

Naibu Waziri huyo amesema sababu hizo zinatia shaka na zimekosa ushawishi, ambao unaweza kueleweka kwa wadau wa soka nchini.

Makalla alisema hayo juzi alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Michezo Extra kilichorushwa hewani na kituo cha redio cha Clouds FM.

Kamati ya Rufani ya TFF chini ya Mwenyekiti wake, Idd Mtiginjola, mwanzoni mwa wiki hii ilimuengua Malinzi kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo utakaofanyika Februali 24, mwaka huu kwa madai ya kukosa sifa.

Makalla alisema kitendo kilichofanywa na kamati hiyo kimeishushia heshima ikiwa ni pamoja na kutilia shaka maamuzi yao, ambayo ameyaita kuwa ni mepesi.

"Bila kupepesa macho wala kuumauma maneno, nikiwa mdau wa soka na kuuvua wadhifa wangu wa unaibu waziri, hapa kuna tatizo kwani kamati haijamtendea haki Malinzi," alisema Makalla.

Naibu Waziri alisema kamati hiyo haikuwa na hoja za msingi na sababu zilizotolewa zimekosa nguvu na haziwezi kukubalika kwa mtu yeyote mwenye mapenzi ya soka ya Tanzania.

Alisema uamuzi huo unaweza kusababisha kuibuka kwa machafuko na kuirudisha TFF kwenye migogoro iliyodumu kwa miaka mingi miaka ya 1980 hadi 1990. Alisema ipo haja ya uamuzi huo kutazamwa upya.

"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete amefanya kazi kubwa sana katika kusimamia soka ya Tanzania ili izidi kufanikiwa, sasa baada ya kufanikiwa tusitake kurudisha nyuma maendeleo hayo," alisisitiza Makalla.

Mbali ya Makalla, wadau wengi wa soka nchini wamelalamikia uamuzi wa kamati hiyo kwa madai kuwa, umefanywa bila kuzingatia ukweli wa mambo na kulenga kuwabeba baadhi ya wagombea.

KOCHA COASTAL UNION KUBWAGA MANYANGA AKIFUNGWA MBILI


KOCHA wa Coastal Union, Hemed Morocco ameweka wazi kuwa endapo anafungwa mechi mbili zijazo dhidi ya Oljoro JKT na Ruvu Shootiga atabwaga manyanga.
Morocco alisema hayo baada ya timu hiyo kupata pointi moja Kanda ya Ziwa, kwa kutoka suluhu na vibonge Toto African na kufungwa bao 1-0 na Kagera Sugar.
Alisema yeye pamoja na kocha msaidizi Ally Kidi wamejitahidi kadri ya uwezo wao kuhakikisha timu inafanya vizuri lakini baadhi ya wachezaji hawana nia njema na klabu hiyo.
"Inavyoonekana kuna wachezaji hawana nia nzuri na timu yao. Kwa sababu hawataki kubadilika."
"Kwa hiyo siwezi kufanya kazi kwenye mazingira hayo hata siku moja. Kama tatizo ni mimi waniambie."
Kocha huyo alisema; "Kama timu itashindwa kufanya vizuri mechi mbili zijazo nafikiri sitatangaza kujiuzulu."
Coastal Union imecheza mechi nne za mzunguko wa pili wa ligi na kutoka sare mbili dhidi ya Prisons na Toto African. Imeshinda dhidi ya Mgambo JKT na kupoteza na Kagera Sugar.  

CHANZO:SHAFII DAUDA