STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, October 24, 2013

Breaking News: OCD-Kilindi apigwa risasi

TAARIFA zilizotufikia muda huu zinasema kuwa, Mkuu wa Kituo cha Polisi (OCD) Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga, Inspekta Lusekelo Edward amejeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi na kundi la watu wasiojulikana.
Inadaiwa kuwa watu hao kabla inadaiwa walimuua Mgambo aliyekuwa akiendesha zoezi la ushuru wa mazao na ndipo Polisi walipoenda kwa ajili ya kutuliza ghasia na kuwakamata wauaji hao na ndipo akafyatuliwa risasi zilizomjeruhi tumboni na mkononi.
Kwa sasa majeruhi huyo amelazwa Hospitali ya mkoa wa Bombo, huku ikielezwa watu wawili wanashikiliwa kuhusiana na tukio hilo, lililotokea siku chache mkoani humo baada ya Mpelelezi wa Makosa ya Jinai wa wilaya ya Lushoto, Ufoo Maanga kushambuliwa na mapanga na wanakijiji waliokerwa na kitendo cha Polisi walioenda kumkamata mtuhumiwa wa mgogoro wa Ardhi kufytulia mtu risasi na kumuua.

PSG, Baravania 'waua' Ulaya, Man U, City nazo zapetaZlatanZla

Zlatan Ibrahimovic akionyesha makeke yake uwanjani
ZLATAN Ibrahimovic jana aliiongoza PSG kufanya maajabu ya 'Shalobela' ugenini baada ya kufunga mabao manne wakati mabingwa hao wa Ufaransa wakiizabua Anderlecht kwa mabao 5-0, huku Cristiano Ronaldo na Sergio Aguero 'Kun' wakizibeba timu zao za Real Madrid na Manchester City zikishinda mechi zao za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Zlatan alifunga mabao hayo manne na kuondoka na mpira wake huku mkali mwingine wa kikosi hicho cha Matajiri wa Ufaransa Edinson Cavani akifunga bao jingine.
Katika mechi nyingine Cristiano Ronaldo  aliisaidia Real Madrid kupata ushindi baada ya kufunga mabao mawili yaliyoiua Juventus ya Italia kwa 2-1, huku bao la pili akilifunga kwa mkwaju wa penati na kumfanya kufikisha jumla ya mabao 7 na kuongoza oprodha ya wafungaji bora kwa sasa mbele ya  Zlatan mwenye mabao sita.
Mechi hiyo ilikuwa ya kuvutia zaidi katika zilizochezwa jana kwani Juventus pamoja na kucheza ugenini lakini ilipiga soka la uhakika mbele ya wenyeji wao ikisawazisha bao la dakika nne la Ronaldo kupitia kwa Fernanod Llorente, kabla ya Ronaldo kuongeza jingine na kudumu hadi kipindi cha kwanza kinaisha na cha pili vilevile.
Nao mabingwa watetezi Bayern Munich aliendeleza rekodi yao ya kushinda michezo yake kwa 100% baada ya kuipasua Viktoria Plzeň kwa mabao 5-0, huku mchezaji bora Ulaya, Frank Ribery akipiga mabao mawili.
Mechi nyingine iliwashuhudia Didier Drogba akiiongoza Galatasaray nyumbani kuwachapa Copenhagen kwa mabao 3-1. Drogba akitupia moja huku Melo na Sjneider wakiongeza mengine.
Nao mabingwa watetezi wa Ligi ya England, Manchester United ikaenda kileleni mwa Kundi A baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Real Sociedad, shukurani kwa bao la kujifunga la Inigo Martnez. huku mahasimu wao wa jiji hilo la  Manchester, Manchester City wakishinda ugenini mabao 2-1, shukrani ikiwa ni kwa Kun Aguero aliyefunga yote dhidi ya CSKA Moscow.
Matokeo ya michezo hiyo ya jana ni kama ifuatavyo:
Bayern Munich 5-0 Viktoria Plzen
Man United 1-0 Sociedad
Galatasaray 3-1 Copenhagen
Real Madrid 2-1 Juventus
Anderlecht 0-5 PSG
Benfica 1-1 Olympiakos
Beyer Leverkusen 4-0 Shakhtar
CSKA Moscow 1-2 Manchester City.
Leo barani humo kutakuwa ni patashika ya michuano ya Ligi Ndogo ya UEFA 'Europa League'

Sikinde kwenda kusherekea miaka yao 35 mjini Morogoro

Baadhi ya wanamuziki wa Sikinde, toka kushoto ni Hassani Kunyata, Abdallah Hemba na Hassani Rehani Bitchuka

BENDI kongwe ya muziki wa dansi ya Mlimani Park 'Sikinde' inatarajiwa kusherehekea miaka 35 ya tangu kuanzishwa kwake rasmi mwaka 1978 kwa kufanya onyesho maalum kesho mkoani Morogoro.
Katibu wa bendi hiyo, Hamis Milambo alisema wameamua kwenda kusherehekea miaka hiyo Morogoro kutokana na ukweli wana muda wa miaka mitano hawajawahi kwenda kutumbuiza mjini humo.
Milambo alisema sherehe hizi zitafanyika kwenye ukumbi wa DDC na watataumia kutambulisha nyimbo zao mpya zinazoandaliwa kwa ajili ya albamu yao.
"Katika kuadhimisha miaka 35 tangu kuanzishwa kwa bendi ya Sikinde, tunatarajia kwenda kujumuika na mashabiki wetu wa mkoa wa Morogoro siku ya Jumamosi, ambapo tutazitambulisha nyimbo zetu mpya," alisema.
Katibu huyo alizitaja nyimbo watakazotumbuiza katika onyesho hilo ni pamoja na 'Kibogoyo', 'Kukatika kwa Dole Gumba', 'Jinamizi la Talaka' ambao umekuwa gumzo kubwa tangu uanze kusikika hewani, 'Za Mkwezi' na 'Mahangaiko ya Kazi'.
Milambo alisema  bendi yao itaenda mjini humo ikiwa kikosi kamili wakiwamo waimbaji wao nyota Hassani Kunyata, Hassain Rehani Bitchuka, Abdallah Hemba na wapiga ala, huku akisisitiza kuwa pia watatumia onyesho hilo kukumbushia vibao vya zamani vilivyoifanya Sikinde kuwa Mabingwa wa Muziki wa Tanzania.
"Tutawapigia kuanzia nyimbo za mwaka 1978 miaka ya 1980 mpaka hizo mpya, tukiwa na maana ya kukata kiu ya wakazi wa Morogoro ambao wameikosa Sikinde kwa muda mrefu," alisema Milambo.

Wednesday, October 23, 2013

Yanga 'yaua' Taifa, Mnyama abanwa Tanga, Kiiza hashikiki


MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga imesahihisha makosa yake leo kwa kuicharaza Rhino Rangers ya Tabora kwa mabao 3-0 wakati Simba ikilazimisha suluhu jijini Tanga dhidi ya wenyeji wao Coastal Union.
Mabao mawili ya Hamis Kiiza kila moja katika kipindi na jingine la Frank Dumayo yalitosha kuwapa nafuu vijana na Ernie Brandts ambao Jumapili walishindwa kulinda ushindi wao wa mabao 3-0 na kulazimishwa sare ya mabao 3-3 na watani zao Simba.
Kiiza akifunga bao la kwanza dakika ya 12 kwa krosi safi ya Simon Msuvah, goli lililodumu hadi kipindi cha kwanza kilipoisha.
Kipindi cha pili Yanga ilionekana kuzidisha mashambulizi dhidi ya wageni hao wa Ligi Kuu na kuongeza bao la pili dakika ya 73 kupitia Frank Domayo kabla ya Kiiza kurudi tena nyavuni dakika ya 81 na kuipa Yanga pointi tatu muhimu zilizowafanya wafikishe pointi 19.
Hata hivyo ushindi huo haukuisaidia Yanga kutoka nafasi ya nne kwani watani zao Simba waliongeza pointi moja wakiwa uwanja wa Mkwakwani Tanga baada ya kutoka suluhu na Coastal Union na kufikisha pointi 20 zilizowarejesha kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
Simba imelingana pointi na Azam na Mbeya City, lakini Wekundu wa Msimbazi wana uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa na hivyo kurejea katika uongozi ikisubiri pambano lake la Jumapili dhidi ya Azam kwenye mfululizo wa ligi hiyo.
Katika pambano la Yanga na Rhino Brandts alipangua kikosi chake kwa kumpanga kipa Deo Munishi Dida, huku Ally Mustafa Barthez, Athumani Chuji na Nadir Cannavaro wakiwa nje ya dimba.

SHAMBA LINAUZWA

LIPO KISANGA KISARAWE MBELE YA KIWANDA CHA SIMENTI.
UKUBWA NI EKARI MOJA KASORO KIDOGO.
BEI SH.MILIONI 6 (MAELEWANO YAPO)
LIPO JIRANI NA BARABARA LINA MAZAO MBALIMBALI
KAMA MAFENESI, MACHUNGWA, MACHENZA NA MITI YA MINAZI.

WASILIANA KWA 0655 006971 AU 0755 006970
EMAIL: mkatedaniel@gmail.com

Arsenal yafa nyumbani, Chelsea yaua, Messi arejea na sare Barca

Roberto Lewandowski
 
Leveling up: Olivier Giroud celebrates making it 1-1
Giroud akishangilia bao lao
VINARA wa Ligi Kuu ya England, Arsenal usiku wa kumkia leo imeshindwa kutamba nyumbani baada ya kunyukwa mabao 2-1 na Borussia Dotmund katika mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Bao la dakika za lala salama la Robert Lewandowski lilitosha kuizima Arsenal ilikuw aimeamini imambulia sare na wanafainali hao wa ligi ya msimu uliopita.
Henrikh Mkhitaryan aliifungia bao la kuongoza Borussia Dortmund kabla ya Olivier Giroud kusawazisha na katika dakika ya 80 Lewandowski akaiua Arsenal iliyokuwa dimba lake la nyumbani la Emirates.

Katika mapambano mengine, Chelsea iliifumua Schalke 04 ya Ujerumani kwa mabao 3-0, mshambuliaji Fernando Torres akitupia mawili na Eden Hazard moja, huku Lionel Messi alirejea uwanjani kwa kasi baada ya kuifungia Barcelona bao lililoipa sare ya ugenini dhidi ya Ac Milan baada ya kufungana bao 1-1.
Robinho alitangulia kuwafungia wenyeji bao dakika ya tisa na Messi kusawazisha dakika ya 24 baada ya kumalizia pasi ya Iniesta.
Nayo Steaua Bucuresti imetoka 1 - 1 na  Basel, Olympique Marseille imefungwa 2-1 na Napoli, Porto ikalala 1-0 mbele ya Zenit, Austria Wien imefungwa 3-0 na Atletico Madrid na Celtic imeshinda 2 - 1 dhidi ya Ajax.
Michuano hiyo itaendelea tena leo kwa michezo mingine nane, ambapo machoi yanaelekezwa katika pambano kati ya Real Madrid ya akina Cristiano Ronaldo na Gareth Bale watakaoikabili Juventus ya Carlos Tevez.
 

Tuesday, October 22, 2013

Kuiona Twiga Stars, Msiumbiji Buku tu, TFF yamlilia Mhango


Na Boniface Wambura
KIINGILIO cha chini kwenye mechi ya wanawake chini ya miaka 20 katika ya Tanzania na Msumbiji itakayochezwa Jumamosi (Oktoba 26 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kitakuwa sh. 1,000.

Mechi hiyo itachezwa kuanzia saa 10 kamili jioni, na kiingilio hicho ni kwa ajili ya viti vya rangi ya kijani, bluu na chungwa. Viingilio vingine ni sh. 2,000 kwa VIP C, sh. 5,000 kwa VIP B wakati VIP A itakuwa sh. 10,000.

Timu ya Msumbiji inatarajiwa kuwasili nchini kesho (Oktoba 23 mwaka huu) saa 8 kamili mchana kwa ndege ya LAM. Msumbiji yenye msafara wa watu 25 itafikia kwenye hoteli ya Sapphire.
***
UCHAGUZI TPL BOARD KUFANYIKA IJUMAA
Uchaguzi wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPL Board) utafanyika Oktoba 25 mwaka huu kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Golden Jubilee Tower.
Kwa mujibu wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wajumbe wanaounda Mkutano wa Uchaguzi ni wenyeviti kutoka klabu 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL), na 14 wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL).

Wagombea kwenye uchaguzi huo ni Hamad Yahya Juma (Mwenyekiti), Said Muhammad Said Abeid (Makamu Mwenyekiti) wakati wanaoumba ujumbe wa Kamati ya Uendeshaji ni Khatib Omari Mwindadi na Kazimoto Muzo.
 ***
RAMBIRAMBI MSIBA WA JIMMY MHANGO
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mjumbe wa Bodi ya klabu ya Ashanti United, Jimmy Mhango kilichotokea jana (Oktoba 21 mwaka huu).

Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani Mhango aliutumikia mpira wa miguu kwa muda mrefu, tangu akiwa mchezaji, kocha na baadaye kiongozi.

Kabla ya kuingia kwenye Bodi ya Ashanti United, enzi za uchezaji wake alichezea timu za Mapinduzi ya Dodoma, Ushirika ya Moshi na Pan African ya Dar es Salaam. Pia aliwahi kuwa Kocha Mkuu wa Ashanti United.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Mhango, klabu ya Ashanti United na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Maziko yamefanyika leo mchana katika makaburi ya Abeid (Mchikichini) Dar es Salaam. Mungu aiweke roho ya marehemu Mhango mahali pema peponi. Amina.

Makamu wa Rais awaongoza waombolezaji kuuaga mwili wa Julius Nyaisangah


  Sehemu ya Wanakamati wa Kamati ya maziko....
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akitia saini katika Kitabu cha maombolezo ya Kifo cha aliyewahi kuwa mtangazaji wa Redio Tanzania, ITV na Redio One na Redio Aboud, marehemu Julius Nyaisanga, aliyefariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita huko mjini Morogoro kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu. Marehemu Nyaisanya ameagwa leo katika viwanja vya Leaders Club Kinondoni na anasafirishwa leo hii kuelekea Tarime kwa ajili ya maziko.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akitoa heshima za mwisho mbele ya jeneza lenye mwili wa aliyewahi kuwa mtangazaji wa Redio Tanzania, ITV na Redio One na Redio Aboud, marehemu Julius Nyaisanga, aliyefariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita huko mjini Morogoro kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu. Marehemu Nyaisanya ameagwa leo katika viwanja vya Leaders Club Kinondoni na anasafirishwa leo hii kuelekea Tarime kwa ajili ya maziko.
 Leah Nyaisanga, ambaye ni mke wa marehemu wa aliyewahi kuwa mtangazaji wa Redio Tanzania, ITV na Redio One na Redio Aboud, marehemu Julius Nyaisanga, akitoa heshima za mwisho mbele ya jeneza lenye mwili wa marehemu mumewe, aliyefariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita huko mjini Morogoro kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu, wakati wa shughuli za kuagwa mwili huo zilizofanyika kwenye viwanja vya Leaders Club Kinondoni na anasafirishwa leo hii kuelekea Tarime kwa ajili ya maziko.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimfariji mfiwa Leah Nyaisanga, ambaye ni mke wa marehemu wa aliyewahi kuwa mtangazaji wa Redio Tanzania, ITV na Redio One na Redio Aboud, marehemu Julius Nyaisanga, aliyefariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita huko mjini Morogoro kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu. Marehemu Nyaisanya ameagwa leo katika viwanja vya Leaders Club Kinondoni na anasafirishwa leo hii kuelekea Tarime kwa ajili ya maziko.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda akisema machache
Menyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP  Dkt. Reginald Mengi, akizungumza machache....
 Mwenyekiti wa Chadema na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe akisema machache
Makamu wa Rais, Dkt. Bilal, akizungumza kutoka salam za rambirambi kwa wafiwa.
  Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda (kulia) akiteta jambo na Mwenyekiti wa Chadema na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, wakati wa shughuli hiyo Viwanja vya Leaders.
 Sehemu ya waombolezaji waliojitokeza kumuaga marehemu Nyaisanga, katika Viwanja vya Leaders Club.
 Sehemu ya waombolezaji waliojitokeza kumuaga marehemu Nyaisanga, katika Viwanja vya Leaders Club. Picha Zote na Ofisi ya Makamu wa Rais

Kamanda Kombe hatunaye duniani

Picture:  James Kombe, SACP
James Kombe
Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi.
ALIYEKUWA kuwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha usalama barabarani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) mstaafu James Kombe amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia kifo hicho Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Advera Senso alisema, 
Kombe alifariki Oktoba 22 mwaka huu na taratibu za mazishi  zinaendelea.

Aidha Senso alisema Marehemu Kombe alizaliwa mwaka 1950 huko Mwika mkoani Kilimanjaro na alijiunga na Jeshi la Polisi tarehe 15 mwezi machi mwaka 1970 baada ya kuhitimu elimu ya sekondari mwaka 1969 nchini Uganda ambapo alipandishwa vyeo na kupewa madaraka mbalimbali.

Baadhi ya vyeo alivyopitia na miaka ya kupata vyeo hivyo katika mabano ni pamoja na Sagenti wa Polisi (1973) Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (1977), Mkaguzi wa Polisi (1984), Mrakibu Msaidizi (1986), Mrakibu wa Polisi(1991), Mrakibu Mwandamizi (1995), Kamishna Msaidizi wa Polisi (1998) na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (2002) hadi alipostaafu mwaka 2010.

Baadhi ya nafasi alizowahi kuzitumikia katika Jeshi la Polisi ni pamoja na kuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) katika wilaya za Dodoma, Tarime, Serengeti na Arusha pamoja na Kuwa Mkuu wa Polisi wa Mkoa (RPC) katika mikoa ya Lindi, Arusha, Kigoma pamoja na Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza ghasia Tanzania na hadi anastaafu alikuwa mkuu wa kikosi cha Usalama barabarani Tanzania.