STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, October 24, 2013

Breaking News: OCD-Kilindi apigwa risasi

TAARIFA zilizotufikia muda huu zinasema kuwa, Mkuu wa Kituo cha Polisi (OCD) Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga, Inspekta Lusekelo Edward amejeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi na kundi la watu wasiojulikana.
Inadaiwa kuwa watu hao kabla inadaiwa walimuua Mgambo aliyekuwa akiendesha zoezi la ushuru wa mazao na ndipo Polisi walipoenda kwa ajili ya kutuliza ghasia na kuwakamata wauaji hao na ndipo akafyatuliwa risasi zilizomjeruhi tumboni na mkononi.
Kwa sasa majeruhi huyo amelazwa Hospitali ya mkoa wa Bombo, huku ikielezwa watu wawili wanashikiliwa kuhusiana na tukio hilo, lililotokea siku chache mkoani humo baada ya Mpelelezi wa Makosa ya Jinai wa wilaya ya Lushoto, Ufoo Maanga kushambuliwa na mapanga na wanakijiji waliokerwa na kitendo cha Polisi walioenda kumkamata mtuhumiwa wa mgogoro wa Ardhi kufytulia mtu risasi na kumuua.

PSG, Baravania 'waua' Ulaya, Man U, City nazo zapetaZlatanZla

Zlatan Ibrahimovic akionyesha makeke yake uwanjani
ZLATAN Ibrahimovic jana aliiongoza PSG kufanya maajabu ya 'Shalobela' ugenini baada ya kufunga mabao manne wakati mabingwa hao wa Ufaransa wakiizabua Anderlecht kwa mabao 5-0, huku Cristiano Ronaldo na Sergio Aguero 'Kun' wakizibeba timu zao za Real Madrid na Manchester City zikishinda mechi zao za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Zlatan alifunga mabao hayo manne na kuondoka na mpira wake huku mkali mwingine wa kikosi hicho cha Matajiri wa Ufaransa Edinson Cavani akifunga bao jingine.
Katika mechi nyingine Cristiano Ronaldo  aliisaidia Real Madrid kupata ushindi baada ya kufunga mabao mawili yaliyoiua Juventus ya Italia kwa 2-1, huku bao la pili akilifunga kwa mkwaju wa penati na kumfanya kufikisha jumla ya mabao 7 na kuongoza oprodha ya wafungaji bora kwa sasa mbele ya  Zlatan mwenye mabao sita.
Mechi hiyo ilikuwa ya kuvutia zaidi katika zilizochezwa jana kwani Juventus pamoja na kucheza ugenini lakini ilipiga soka la uhakika mbele ya wenyeji wao ikisawazisha bao la dakika nne la Ronaldo kupitia kwa Fernanod Llorente, kabla ya Ronaldo kuongeza jingine na kudumu hadi kipindi cha kwanza kinaisha na cha pili vilevile.
Nao mabingwa watetezi Bayern Munich aliendeleza rekodi yao ya kushinda michezo yake kwa 100% baada ya kuipasua Viktoria Plzeň kwa mabao 5-0, huku mchezaji bora Ulaya, Frank Ribery akipiga mabao mawili.
Mechi nyingine iliwashuhudia Didier Drogba akiiongoza Galatasaray nyumbani kuwachapa Copenhagen kwa mabao 3-1. Drogba akitupia moja huku Melo na Sjneider wakiongeza mengine.
Nao mabingwa watetezi wa Ligi ya England, Manchester United ikaenda kileleni mwa Kundi A baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Real Sociedad, shukurani kwa bao la kujifunga la Inigo Martnez. huku mahasimu wao wa jiji hilo la  Manchester, Manchester City wakishinda ugenini mabao 2-1, shukrani ikiwa ni kwa Kun Aguero aliyefunga yote dhidi ya CSKA Moscow.
Matokeo ya michezo hiyo ya jana ni kama ifuatavyo:
Bayern Munich 5-0 Viktoria Plzen
Man United 1-0 Sociedad
Galatasaray 3-1 Copenhagen
Real Madrid 2-1 Juventus
Anderlecht 0-5 PSG
Benfica 1-1 Olympiakos
Beyer Leverkusen 4-0 Shakhtar
CSKA Moscow 1-2 Manchester City.
Leo barani humo kutakuwa ni patashika ya michuano ya Ligi Ndogo ya UEFA 'Europa League'

Sikinde kwenda kusherekea miaka yao 35 mjini Morogoro

Baadhi ya wanamuziki wa Sikinde, toka kushoto ni Hassani Kunyata, Abdallah Hemba na Hassani Rehani Bitchuka

BENDI kongwe ya muziki wa dansi ya Mlimani Park 'Sikinde' inatarajiwa kusherehekea miaka 35 ya tangu kuanzishwa kwake rasmi mwaka 1978 kwa kufanya onyesho maalum kesho mkoani Morogoro.
Katibu wa bendi hiyo, Hamis Milambo alisema wameamua kwenda kusherehekea miaka hiyo Morogoro kutokana na ukweli wana muda wa miaka mitano hawajawahi kwenda kutumbuiza mjini humo.
Milambo alisema sherehe hizi zitafanyika kwenye ukumbi wa DDC na watataumia kutambulisha nyimbo zao mpya zinazoandaliwa kwa ajili ya albamu yao.
"Katika kuadhimisha miaka 35 tangu kuanzishwa kwa bendi ya Sikinde, tunatarajia kwenda kujumuika na mashabiki wetu wa mkoa wa Morogoro siku ya Jumamosi, ambapo tutazitambulisha nyimbo zetu mpya," alisema.
Katibu huyo alizitaja nyimbo watakazotumbuiza katika onyesho hilo ni pamoja na 'Kibogoyo', 'Kukatika kwa Dole Gumba', 'Jinamizi la Talaka' ambao umekuwa gumzo kubwa tangu uanze kusikika hewani, 'Za Mkwezi' na 'Mahangaiko ya Kazi'.
Milambo alisema  bendi yao itaenda mjini humo ikiwa kikosi kamili wakiwamo waimbaji wao nyota Hassani Kunyata, Hassain Rehani Bitchuka, Abdallah Hemba na wapiga ala, huku akisisitiza kuwa pia watatumia onyesho hilo kukumbushia vibao vya zamani vilivyoifanya Sikinde kuwa Mabingwa wa Muziki wa Tanzania.
"Tutawapigia kuanzia nyimbo za mwaka 1978 miaka ya 1980 mpaka hizo mpya, tukiwa na maana ya kukata kiu ya wakazi wa Morogoro ambao wameikosa Sikinde kwa muda mrefu," alisema Milambo.