STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, October 31, 2013

Rais JK kushiriki mbio za Uhuru Marathon

Rais Jakaya Kikwete

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete anatarajiwa kushiriki katika mbio maalum za Uhuru (Uhuru Marathon) zitakazofanyika Desemba 8 jijini Dar es Salaam imefahamika.
Mshindi wa jumla wa mbio hizo za marathoni (kilomita 42) atakabidhiwa zawadi ya Sh. milioni 3.5.
Akizungumza jana kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Katibu Mkuu wa kamati ya maandalizi ya mbio hizo, Innocent Melleck, alisema kuwa Rais Kikwete atakabidhiwa fomu namba moja ya kujisajili katika ushiriki wa mbio hizo huku akimtaja Spika wa Bunge, Anne Makinda kuwa atapewa fomu namba mbili.
Melleck alisema kuwa viongozi hao watashiriki mbio za kilomita tatu na kumtaja mshiriki mwingine wa mbio hizo ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni na Mbunge wa Jimbo la Hai, Freeman Mbowe.
Alisema kuwa tayari fomu za kujiandikisha zimeanza kutolewa katika vituo mbalimbali nchini jana huku zoezi hilo likitarajiwa kufanyika kwenye viwanja vya Bunge mkoani Dodoma Jumanne na Jumatano wiki ijayo.
Alisema ada ya fomu hizo kwa mbio za marathoni ni Sh. 6,000 huku za kilomita tano zikiwa ni Sh. 2,000 na zitashirikisha pia wanariadha kutoka nje ya nchi.
Alieleza kuwa lengo la kuanzisha mbio hizo ni kutaka kuenzi na kudumisha amani iliyopo nchini na kukumbushana kutochezea thamani hiyo.
"Kupitia mbio hizi tutaweka tofauti zetu pembeni, Tanzania kwanza, Amani Kwanza," alisema katibu huyo wa kamati ya maandalizi.
Aliwataka wadau na taasisi mbalimbali kujitokeza kudhamini mbio hizo zitakazokuwa zinafanyika kila mwaka nchini.

TASWA WAPONGEZA UONGOZI MPYA WA TFF

 
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kinatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) uliochaguliwa Jumapili iliyopita.
 
Tunaungana na wapenda michezo na Watanzania kwa ujumla kuitakia kila la heri Kamati ya Utendaji ya TFF na shirikisho hilo kwa ujumla chini ya Rais mpya Jamal Malinzi na Makamu wake, Wallace Karia.
 
TASWA inaamini Malinzi, Karia na wajumbe wao ni wazoefu na ni watu wenye kujua mambo mengi yanayohusu mpira wa miguu nchini, hivyo tunaamini watakuwa viongozi wazuri kwa nafasi zao katika kuhakikisha shirikisho hilo linasonga mbele.
 
Tunawatakia kila la heri Wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji, huku tukiamini hawatawaangusha Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF waliowaamini kushika nafasi hizo.
 
TASWA na waandishi wa habari za michezo kwa ujumla hapa nchini tunaahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha ili watekeleze majukumu yao ipasavyo.
 
Nawasilisha.
 
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
30/10/2013

Mtanzania kuwania ubingwa wa Dunia wa WBC

Bondia Omer Kimweri
BONDIA Mtanzania anayefanya shughuli zake nchini Australia, Omari Kimweri 'Lion Boy' anatarajiwa kuwa Mtanzania wa kwanza kupanda ulingoni kuwania taji la Dunia la WBC katika pambano litakalofanyika Novemba 30.
Kimweri atapanda ulingoni katika pambano la uzito wa Minimum (kilo 47.5) nchini China kupigana na bingwa mtetezi wa taji hilo duniani, Mchina Xiong Zhao Zhong.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotumwa kwa MICHARAZO, Kimweri amepata nafasi ya kupigana na Zhong kutokana na rekodi nzuri aliyonayo katika mchezo huo akiwa amepanda ulingoni mara 16 na kushinda michezo 13.
Kati ya michezo hiyo Mtanzania huyo amepoteza michezo mitatu tu, wakati mpinzani wake amecheza michezo 26 na kushinda 21 na kupigwa michezo minne na mmoja kuambulia sare hali inayoonyesha pambano hilo litakuwa kali.
"Kura zilimuangukia Kimweri baada ya kutakiwa bondia kutoka Afrika mwenye rekodi nzuri kupambana na bingwa huyo wa dunia wa WBC Minimum Weight, hivyo Kimweri anakuwa Mtanzania wa kwanza kuwania taji hilo," taarifa hiyo ilisomeka hivyo.
Mara ya mwisho kwa Mtanzania huyo kupanda ulingoni ilikuwa Julai 25 mwaka huu ambapo aliibuka na ushindi wa TKO ya raundi ya kwanza.
Kimweri yupo kwenye mazoezi makali akifanyishwa akisaidiwa na bondia bingwa wa Lightfly kutoka Ufilipino, Randy Petalcoria.