STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, December 26, 2013

Ismail Rage awashangaa wanaombeza Simba

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage
MWENYEKITI wa Simba, Ismail Aden Rage, amesema hakuwatuma askari Polisi kwenda kuwatimua Wajumbe wa Kamati ya Utendaji na wanachama wa klabu hiyo waliokuwa wanakutana klabuni kuipanga mikakati ya kuishinda Yanga.
Bali alifanya hivyo ili kwenda kuhakikisha usalama kwao na mali ya klabu na ndiyo maana aliposikia wanaipangia mikakati Yanga aliwataka askari hao awaache waendelee na mkutano..
Pia alidai kushangazwa akidaiwa hakushiriki kufanikisha ushindi wa Simba dhidi ya Yanga katika mechi ya Nani Mkali Jembe, wakati yeye aliyewasajili wachezaji Ally Badru na Awadh Juma aliyefunga bao la tatu, na kudai Kamati ya Utendaji haikamiliki bila ya Mwenyekiti.
Akizungumza MICHARAZO, Rage alisema siyo kweli kama aliwatumia viongozi na wanachama wenzake askari ili kuwatimua klabu wakipanga mikakati ya kuifunga Yanga, bali alifanya hivyo ili kulinda usalama klabuni.
"Siyo kweli kama mimi niliwatumia Polisi ili kuwatimua, bali kulinda usalama kwa kuhisi labda mkutano wao ulikuwa na ajenga mbaya na hivyo kuzua tafran na kuharibu mali za klabu, lakini nilipoelezwa lengo lao nini niliagiza askari hao awaache wafanye mkutano wao ili kufanikisha ushindi wa Simba," alisema.
Pia alisema madai kwamba hakushiriki kwa namna yoyote kufanikisha ushindi wa Simba wa mabao 3-1 dhidi ya Yanga, hayana mashiko kwa vile alikutana na matawi siku moja kabla ya wenzake kukutana, na kamati haikamiliki bila ya Mwenyekiti ambaye ni yeye (Rage).
"Mimi ndiye mwenyekiti, ni mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, sijachangia vipi wakati katika usajili wa dirisha dogo nimesajili wachezaji wawili Ally Badru na Awadh Juma aliyefunga bao moja na kusababisha jingine, watu watambue hizi ni blabla za kutaka kunitia ubaya tu," alisema Rage.
Aliongeza anafahamu ni watu watatu tu ndiyo wakorofi wanaomsakama kila uchao, bahati nzuri wanachama wa Simba wanafahamu yeye ni mmoja wa viongozi shupavu na makini wasiyoyumbishwa ataendelea kusimama mpaka dakika ya mwisho kuona Simba inakuwa ya amani na utulivu.
Rage alisimamishwa na Kamati ya Utendaji ya Simba kabla ya TFF kumrejesha na kumtaka aitishe mkutano wa dharura aliougomea na sakata lake limepelekwa katika Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi ya Wachezaji kwa maamuzi.

Majaribio tiketi za Electroniki saa 10 leo

MECHI ya kujaribu matumizi ya tiketi za elektroniki kati ya Azam na Ruvu Shooting inachezwa leo (Desemba 26 mwaka huu) saa 10 kamili jioni Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Viingilio katika mechi hiyo ya majaribio ni sh. 1,000 na sh. 2,000 ambapo tiketi zinapatikana kupitia M-Pesa na mawakala wa CRDB Fahari Huduma. Tiketi zitaendelea kuuzwa hadi kitakapoanza kipindi cha pili.
Mawakala 18 wa Fahari Huduma wanaouza tiketi hizo ni ABC Computer- Mtaa wa Samora, Abraham Anangisye Mwampetele- Maji Matitu, Apex Security Services- Mtaa wa Mibega, Kinyerezi, Athuman Fakhi Adam- Kongowe Mbagala, Fedha Investment Limited- Pamba Road na Fuya Godwin Kimbita- Tegeta Block.
Ghomme Health & Education Limited-Bahari Beach, Herman Arbogast Tarimo- Kigamboni, K- Finance Limited- Shekilango, Sinza, Koli Finance Limited- Mtaa wa Samora, LB Pharmacy- Mtoni Kijichi, Lista Phares Barnabas- Tabata Segerea na Maly Investment Company Limited.
Wengine ni Micu Enterprises- Mtaa wa Congo, Kariakoo, S&D Collection Company Limited- Mikocheni, Shoppers Plaza, Therry Investment Limited- Tegeta Kibaoni, TSHS Distributors Limited- Mtoni kwa Aziz Ali na Wemerick Independent Vehicle- Mtaa wa Boko, .
Mechi nyingine ya majaribio itakuwa kati ya Ashanti United na JKT Ruvu ambayo itachezwa Januari Mosi mwakani kwenye uwanja huo huo.