STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, April 17, 2014

Bale akifunga bao la ushindi la Real Madrid jana
BAO lililofungwa kiufundi kwa juhudi binafsi za Gareth Bale zimeiwezesha Real Madrid kunyakua taji la kwanza kwa msimu huu kwa kuilaza Barcelona katika mchezo wa fainali ya Kobe la Mfalme.
Mechi hiyo iliyochezwa kwenye uwanja wa  Mestalla mjini Valencia, Hispania, ilikuwa ya kusisimua na Real Madrid waliwafunika wapinzani wao, licha ya wenyewe kumiliki sehemu mkubwa wa pambano hilo.
Real walianza kuandika bao  la kuongoza katika dakika ya 11, mfungaji Angel di Maria akimalizia pasi ya Karim Benzema, lakini Bartra akaisawazishia Barca dakika ya 68 kwa pasi ya Xavi.
Dakika tano kabla ya pambano hilo kumalizika nyota wa Wales, Gareth Bale aliyefunga bao la ushindi dakika ya 85 kwa pasi ya Fabio Coentrao na kumkimbiza beki wa Barcelona aliyemuondoka kwenye mstari kabla ya kuzidiwa mbio na kufunga bao maridadi lililompa Carlo Ancelotte furaha ya aina yake.
Katika mchezo huo, Mwanasoka bora wa dunia, Cristiano Ronaldo alikuwa nje leo akiendelea kuugulia maumivu yake na aliungana na wenzake kuwapongeza baada ya mechi kwa ushindi huo.
Baada ya kunyakua taji la kwanza msimu huu, Real sasa inaelekeza nguvu zake katika mataji mengine mawili, La Liga na Ligi ya Mabingwa ambako imefika hatua ya Nusu Fainali na itamenyana na mabingwa watetezi, Bayern Munich.
Kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Hispania, Real inachuana na Atletico Madrid walio kileleni na Barca walio nafasi ya tatu. 

Yanga yaiwinda Simba Kawe Beach, Mnyama aenda Zenji

Yanga
Simba
KLABU ya Yanga ambayo ilirejea jijini Dar es Salaam jana ikitokea Moshi ilikocheza mechi ya kirafiki dhidi ya Panone FC wakati ikiwa njiani kutokea Arusha, imeweka kambi yake Kawe Beach na imeelezwa kwamba huenda wakahamia Bagamoyo mkoani Pwani kwa ajili ya mechi yao ya kukamilisha ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wao Simba.
Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema jana kwamba aulizwe kuhusu kambi ya timu hiyo akishafika Dar es Salaam akitokea Moshi, lakini mara baada ya kutua walikwenda moja kwa moja Kawe Beach na habari kutoka ndani zilisema kwamba kambi hiyo inaweza ikahamia Bagamoyo.
Hata hivyo, mshambuliaji wa kimataifa kutoka Uganda, Emmanuel Okwi, yuko katika hatihati ya kujiunga na kambi hiyo kutokana na kuhitaji alipwe fedha zake za usajili anazoidai klabu hiyo.
Okwi aliyejiunga na Yanga Desemba mwaka jana anaidai klabu hiyo dola za Marekani 50,000 na imeelezwa kwamba juzi alikataa kupokea kiasi cha dola za Marekani 20,000 ambazo ilikuwa atanguliziwe.
Chanzo cha gazeti hili kilieleza kuwa Okwi aliambiwa apokee dola 20,000 ili arejee kundini kujiandaa na mechi dhidi ya Simba Jumamosi lakini Mganda huyo alikataa.
Habari zaidi kutoka Yanga zilieleza kuwa aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Francis Kifukwe, alimtaka Okwi akubali kiasi hicho na kuahidiwa kumaliziwa fedha nyingine zilizobakia mara baada ya viongozi wengine wa juu wa Yanga watakaporejea nchini.
Rafiki wa karibu wa Okwi aliliambia gazeti hili kwamba mshambuliaji huyo amegoma kupokea malipo hayo kwa mafungu ili kujiepusha na suala na kuja kusotea kiasi kilichobakia.
"Mechi hiyo ya Simba Jumamosi ndiyo ya mwisho, anajua asipolipwa sasa itakula kwake", alisema rafiki huyo ambaye alikuwa naye tangu alipokuwa anaichezea Simba.
Okwi hapatikani katika simu zake za mkononi na inaelezwa pia hata mahali anapolala amekuwa anabadilisha kulingana na atakavyojisikia siku hiyo.
Yanga tayari imeshavuliwa ubingwa na Azam FC na inachotaka katika mechi hiyo ya funga dimba ni kulinda heshima kwa wanachama na wapenzi wa timu hiyo.
Kwa kumaliza katika nafasi ya pili, Yanga itaiwakilisha nchi mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho mapema mwakani.
Kocha wa timu hiyo, Mholanzi Hans van der Pluijm, alisema kuwa atawatumia wachezaji waliofanya mazoezi tu kwa ajili ya mechi hiyo ya Jumamosi.
Alisema kuwa hataki kuzungumzia mchezaji asiyekuwa pamoja na timu kwa sababu za kiutawala.
Wakati Yanga ikijichimbia Dar, wapinzani wao wamekimbilia Zanizbra kwa ajili ya kusaka ubani wa kuiua wana Jangwani siku ya Jumamosi Taifa.
Mwenyekiti wa Kamati ya usajili wa klabu hiyo, Zakaria Hanspope ndiye aliyeokoa jahazi timu kwenda kambini Zenji baada ya kudaiwa kuwapo kwa mgomo baridi kwa wachezaji kudai posho na mishahara waliyokuwa wanadai.
NIPASHE.