STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, February 1, 2013

Kampira awasihi wapiga kura uchaguzi mkuu wa TFF

Ramadhani Kampira


ALIYEWAHI kuwa mchezaji wa soka wa Yanga na TAMCO Kibaha, Ramadhani Kampira amewakumbusha wapiga kura watakaoshiriki uchaguzi mkuu wa TFF, kuwachagua viongozi watakaouendeleza mchezo huo kama alivyokuwa Leodger Tenga.
Aidha amewasihi wapiga kura wasije wakachagua kiongozi kwa uwezo wake kifedha au ahadi tamu bali wawasikilize kwenye kampeni sera na mipango yao yenye tija kwa soka la Tanzania ambalo alidai linahitaji ukombozi kuinuka mahali lilipo.
Kampira, Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Soka wilaya ya Kinondoni, alisema wapiga kura wa TFF wanapaswa kutambua kuwa soka la Tanzania linahitaji viongozi wenye uchungu wa kweli wa mchezo huo kama alivyokuwa Tenga aliyemwagia sifa.
"Nilikuwa nawaomba wapiga kura wa TFF, kuhakikisha wanawachagua viongozi wwenye uchungu wa kweli na soka la Tanzania ili kuendeleza pale alipopaacha Tenga, kosa lolote watakalofanya wapiga kura hao wataurudisha tulipotoka," alisema Kampira.
Kampira aliongeza mara baada ya kuanza kwa kampeni, wapiga kura wanapaswa kuzisikiliza sera na mipango ya wagombe na kuzipima kabla ya kuwapigia kura wale ambao wanaona wanafaa kuliongoza shirikisho hilo.
Alisema itakuwa kosa kubwa kama wapiga kura hao wataamua kuwaangalia au kuwapima wagombea kwa umahiri wao wa kuzungumza na kutoa ahadi sawia na uwezo wao kifedha bila kujali kama watakuja kuliangamiza soka la Tanzania.
"Wapiga kura wasiangalie uwezo wa kifedha za wagombea, bali wachague viongozi ambao watalitoa soka la Tanzania kutoka mahali lililpo hadi kwenye maendeleo ya kweli," alisema.
Uchaguzi mkuu wa TFF unatarajiwa kufanyika Februari 24 jijini Dar es Salaam ambapo mrithi wa Tenga na viongozi wengine ndani ya shirikisho hilo watafahamika rasmi.

No comments:

Post a Comment