STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, February 1, 2013


TEGETE, MAFTAH WATOSWA STARS ITAKAYOIVAA CAMEROON

Mshambuliaji nyota wa Yanga, Jerryson Tegete

KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ametaja kikosi cha wachezaji 21 kitakachoingia kambini siku ya Jumapili kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Cameroon (Indomitable Lions), huku akiwaacha mshambuliaji aliyerejea kwa kasi, Jerryson Tegete na beki wa kushoto, Amir Maftah.
Akitangaza kikosi hicho jana, Poulsen aliwataja wachezaji watakaoingia kambini ni makipa Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ali (Azam) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Nassoro Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Nadir Haroub (Yanga), Kelvin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (Simba) na Issa Rashid (Mtibwa Sugar).
Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Simon Msuva (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Salum Abubakar (Azam), Khamis Mcha (Azam), Athuman Idd (Yanga) na Mwinyi Kazimoto (Simba). Washambuliaji ni Mrisho Ngasa (Simba), na Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Kocha Poulsen, alisema mechi dhidi ya Cameroon itakuwa kipimo kizuri kwake kwa sababu ni sehemu ya maandalizi kabla ya kucheza mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco itakayofanyika Machi mwaka huu.
“Itakuwa mechi ngumu na kipimo sahihi kwetu. Tuko tayari, tutacheza kwa staili yetu kwa sababu ni sehemu ya maandalizi kabla ya mechi dhidi ya Morocco. Ni mechi nzuri kwa sababu wachezaji wameonyesha wako tayari.
“Tumetoka kucheza dhidi ya Zambia na Ethiopia. Lengo ni Taifa Stars kucheza fainali za AFCON 2015, kwa hiyo mechi dhidi ya Cameroon ni sehemu ya mipango yetu kuhakikisha tunafika huko,” amesema Kim ambaye amerejea nchini juzi kutoka Afrika Kusini kuzifuatilia timu za Morocco na Ivory Coast zilizo kundi moja na Tanzania katika mechi za mchujo za Kombe la Dunia.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itacheza na Morocco, Machi 24 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Stars inashika nafasi ya pili katika kundi lake nyuma ya Ivory Coast inayoongoza. Timu nyingine katika kundi hilo ni Gambia.

No comments:

Post a Comment