Kava la filamu ya Salamu Toka Kuzimu |
Muonekano wa filamu ya Katikati ya Jiji |
MSANII wa zamani wa muziki wa kizazi kipya aliyejitosa kwenye uongozaji wa filamu, Hussein Ramadhan 'Swagger One' amerekodi filamu mpya tatu kwa mpigo za 'Jeshi la Mfu', 'Sauti Toka Kuzimu' na 'Katikati la Jiji'.
Akizungumza na MICHARAZO, Swagger aliyetamba na makundi ya Double W na Crime Busters, alisema filamu ya kwanza kutoka kati ya hizo ni 'Jeshi la Mfu' itakayofuatiwa na 'Sauti Toka Kuzimu' na kisha 'Katikati ya Jiji' inayozungumzia maisha halisi ya biashara ya miili inayofanywa na baadhi ya wanajamii nchini.
Alisema filamu zote hizo zimewashirikisha wasanii mchanganyiko wakiwamo wenye majina na chipukizi kwa lengo la kutoa ladha tofauti na pia ni kati ya filamu anazotarajia zitaleta mapinduzi katika tasnia hiyo kutokana na simulizi zake.
"Ni filamu za aina yake, sijisifu kwa vile nimeziandaa, ila ukweli ndivyo ulivyo siyo filamu za sebuleni na kulilia mapenzi, ni kazi za kusisimua ambazo tumezoea kuziona kwa watayarishaji na waongozaji wa kimataifa duniani," alisema.
Mtayarishaji huyo aliongeza kuwa amekuja na filamu za kusisimua ili kuondoa dhana kwamba soko la filamu limetekwa na masimulizi ya mapenzi tu.
"Nimekuja tofauti ili kuwapa fursa wasiofagilia filamu za kimapenzi wapate ladha nyingine ya kusisimua hasa hii ya 'Sauti Toka Kuzimu' au 'Jeshi la Mfu' ni kama filamu zile zinazozalishwa Hollywood kwa simulizi na mandhari zake, watu wasubiri kuziona," alisema Swagger.
Kabla ya kujitosa kwenye utayarishaji wa filamu, Swagger alianza kuigiza akishirikiana na mama yake aliyekuwa nyota wa michezo wa kuigiza sambamba na akina Mzee Majuto, Mzee Small, marehemu Mwanachia n Qudrat Olomoda maarufu kama 'Chombeza'.
No comments:
Post a Comment