KUNDI la polisi wenye silaha za moto juzi usiku walivamia nyumbani kwa
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman
Mbowe, kwa nia ya kumkamata.
Askari hao wanaokisiwa kufikia saba, wakiwa na silaha
nzito katika gari la wazi waliwasili nyumbani kwa Mbowe majira ya saa saba na
nusu usiku na kuwaamuru askari wanaolinda nyumbani kwake kumtoa Mbowe nje ili
waonane naye.
Walinzi wa Mbowe walihoji uhalali wa ukamataji huo na
kuwataka polisi wawaoneshe hati ya kumkamata, lakini hawakuweza kuionesha, hali
iliyozusha wasiwasi kwa walinzi wa kiongozi
huyo.
Hata hivyo walinzi hao waliwaambia polisi hao kuwa
Mbowe ambaye pia ni kiongozi mkuu wa kambi ya upinzani bungeni alikuwa safarini,
jibu ambalo lilipokewa kwa shingo upande na askari
hao.
Polisi hao baada ya kuona wameshindwa kukamilisha
kazi hiyo, waliwaachia walinzi hao namba ya simu 0754-085600 ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi wa
Kinondoni, Ernest Kimola, wakiwaagiza kuhakikisha wanamwambia Mbowe awasiliane
na kamanda huyo.
RCO amsukumia RPC,
akana
Hata hivyo, alipohojiwa na Tanzania Daima Jumapili
kwa njia ya simu, Mkuu wa Upelelezi Kimola aligoma kuzunguzia suala hilo na
kumtaka mwandishi kuwasiliana na mkuu wake wa kazi, ambaye ni Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Kinondoni, Kamilius Wambura, akidai ndiye mwenye haki ya kutoa ufafanuzi
wa jambo hilo.
“Unajua mimi si msemaji wa polisi, wasiliana na
kamanda wa mkoa, maana ndiye mwenye uwezo wa kutoa maelezo,” alisema Kimola
na kukata simu. Lakini alipopigiwa simu Kamanda Wambura aliruka kimanga, kwa
mshangao, akidai kutojua lolote kuhusiana na polisi kuvamia nyumbani kwa
Mbowe.
“Kwa kweli ndiyo napata
taarifa hizo kutoka kwako, kuwa kiongozi huyo alifuatwa na polisi, maana silijui
suala hilo hata kidogo,” alisema Wambura, naye kama alivyofanya
Kimola akakata simu.
Kauli ya CHADEMA
Lakini wakati Kimola
akikataa kusema chochote, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema
kuwa alizungumza kwa njia ya simu na Kimola kuhusiana na kitendo cha polisi
kuvamia nyumbani kwa kiongozi huyo wa juu wa kisiasa, na kudai kupewa majibu ya
kushangaza.
Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara
uliofanyika Manzese, Wilaya ya Kinondoni, Dk. Slaa alisema Kimola alijitetea
akidai kwanza kukana kufika nyumbani kwa Mbowe usiku wa manane. Pili, alisema
kuwa hawakwenda kumkamata Mbowe, isipokuwa kufanya naye mazungumzo na kisha
wangemwacha.
Slaa alisema kitendo hicho kimewashitua na ni cha
kinyama na kilichokiuka sheria za nchi na haki za binadamu. Aliongeza kwamba,
daima wamekuwa wakilishutumu Jeshi la Polisi kwa kutumika vibaya kukandamiza
wapinzani, lakini mara zote CHADEMA kimepuuzwa na sasa jeshi hilo limeamua
kuvamia makazi ya viongozi wa kisiasa kwa madhumuni
yasiyoeleweka.
Alisema haijulikani nini kingetokea ikiwa Mbowe
angekuwa ndani, ikiwa walinzi wangeamua kugoma kumwachia kiongozi wao. “Tuna hofu kubwa na usalama wetu, maana pale wangeweza
kufanya lolote, hata kumuua na kisha kutoa matamshi kuwa walikuwa wanajibishana
kwa risasi, kama ambavyo imekuwa jadi ya askari polisi kutoa taarifa za uongo na
upotoshaji wanapoua watu,” alisema Slaa.
Alisema ikiwa polisi
walikuwa na shida ya kweli, wangemwita kwa njia sahihi na si kumvamia na
kuingilia uhuru wake na wa familia yake kama wanakamata gaidi ama jambazi
hatari.
Dk. Slaa alisema Mbowe anayo ofisi inayojulikana, na
kama kweli hakukuwa na jambo baya lililopangwa na polisi hao wasingeweza kufanya
uhuni kama walioufanya.
“Kama wanaweza kuvamia nyumbani kwa kiongozi
mkubwa kama Mbowe wakiwa na silaha nzito, itakuwaje kwa viongozi wa kawaida na
raia?” alihoji Slaa.
Kutokana na tukio hilo la kuogofya, CHADEMA imemtaka
Rais Jakaya Kikwete kuwaeleza Watanzania maana ya matukio haya ambayo
yamedhamiria kuleta vurugu kubwa nchini. Kadhalika, wamemtaka Mkuu wa Jeshi la
Polisi nchini, Said Mwema, kuueleza umma kile kilichokusudiwa na askari wake
kuvamia nyumbani kwa Mbowe mithiri ya jambazi.
Itakumbukwa pia kuwa
hivi karibuni askari polisi wa Mkoa wa Arusha walivamia nyumbani kwa Mbunge wa
Arusha Mjini, Godbless Lema, wakiwa na silaha nzito na mbwa, na kumkamata, kisha
kumtupa rumande kwa siku nzima.
SOURCE: JAMII
FORUM
No comments:
Post a Comment