Na Boniface Wambura
TIMU ya Taifa (Taifa Stars) imeondoka leo asubuhi (Julai 14 mwaka huu) kwenda Mwanza ambapo itapiga kambi ya siku kumi kujiandaa kwa mechi ya marudiano dhidi ya Uganda (The Cranes) kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imeondoka kwa ndege ya PrecisionAir na itafikia hoteli ya La Kairo wakati mazoezi yatafanyika Uwanja wa CCM Kirumba kulingana na programu ya Kocha Mkuu Kim Poulsen.
Wachezaji walioko katika kikosi hicho ni Juma Kaseja, Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vincent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd na Haruni Chanongo.
Mechi ya marudiano itachezwa kati ya Julai 26 na 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nelson Mandela ulioko Namboole nje kidogo ya Jiji la Kampala. Tarehe rasmi itapangwa na Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu vya Uganda (FUFA) siku kumi kabla ya mechi.
No comments:
Post a Comment