STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, August 2, 2013

Golden Bush Fc yawakumbuka yatima Sikukuu ya Eid el Fitry

 
Kikosi cha timu ya Golgen Bush Veterani katika picha ya pamoja walipokuwa mjini Morogoro kwa mechi zao za kirafiki

TIMU ya soka ya Golden Bush FC inayojumuisha timu ya veterani na ile ya vijana inayoshiriki Ligi Daraja la Nne Wilayani Kinondoni, siku ya Jumapili inatarajiwa kugawa msaada wa vyakula na vitu vingine kwa yatima wanaolelewa katika kituo cha New Orphans Family, kilichopo Kigogo jijini Dar es Salaam.
Zoezi hilo la ugawaji wa misaada hiyo kwa yatima hao utafanyika mara baada ya timu ya veterani kutoka kukipiga na timu ya Kijitinyama Veterani katika pambano la kurafiki litakalofanyika kwenye uwanja wa Kijitinyama.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mlezi na Msemaji wa timu ya Golden Bush, Onesmo Waziri 'Ticotico' klabu yao imeamua kufanya jambo hili wakati wa kuelekea kwenye sherehe ya sikukuu ya Eid el Fitry kama njia ya kuwakumbuka na kuwafariji yatima ikiwa ni jukumu la kila mwana jamii.
Taarifa rasmi ya klabu hiyo kupitia Ticotico, inasomeka vizuri hapo chini isome mwenyewe;
Kwa niaba ya uongozi wa Golden Bush FC pamoja na wadau wote ambao tumekuwa nao katika timu yetu, tunaomba wapenzi wetu waungane na timu yetu siku jumapili ambapo Golden bush FC tutakuwa na shughuli nzito ya kutoa zawadi kwa baadhi ya wahitaji katika mojawapo ya vituo vya watoto yatima. Shughuli hiyo itarabiwa na baadhi ya viongozi wakishirikiana na wachezaji wetu ambapo kuanzia saa nne na nusu asubuhi siku ya jumapili ya tarehe 04/08/2013 kundi la wachezaji wote wataelekea maeneo ya Kigogo tayari kutoa zawadi kadhaa kwa kikundi cha New Orphans family.

Tumelazimika kufanya shughuli hii ya kijamii kwasababu timu yetu imejijengea jina kubwa kutokana na mafanikio makubwa katika soka yaani timu yetu ya vijana ambayo mpaka sasa ndiyo inayoongoza ligi daraja la nne Wilaya Kinondoni na timu yetu ya veterans inayoundwa na wachezaji mahili sana na waliocheza mpira wa miguu hadi kiwango cha timu ya taifa. Hivyo unaweza kuona kwamba pamoja na kutoa burudani ya uwanjani Golden bush FC tunalazimika kuungana na kundi hili maalum kuburudika kwa pamoja katika sherehe ya Eid.

Tumesukumwa na ubinadamu na wajibu wetu katika jamii, hivyo kwa pamoja tumechangishana na kupata kiasi flani kitakacho tuwezesha kununua walau zawadi kadhaa zitakazo saidia jamii hii ya wahitaji nao kusherehekea sikukuu kubwa ya Eid.

Nawatakieni kila la kheri katika mfungo huu wa Ramadhani.

Asanteni
Onesmo Waziri 'Ticotico' 
Msemaji wa Timu

No comments:

Post a Comment