STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, August 2, 2013

Mieno, Umony waachwa msafara wa Azam Afrika Kusini

Mieno (kushoto) akiwa na Seif Abdallah Karihe. Mieno hatakuwepo kwenye msafara wa Azam kesho kwa vile ni majeruhi
Brian Umony ambaye hatakuwepo kwenye msafara wa Azam kesho

WACHEZAJI wa kimataifa kutoka Kenya,  Humphrey Mieno na Mganda Brian Omony wameondolewa kwenye msafara wa klabu ya Azam unaotarajiwa kuondoka kesho asubuhi kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya kambi ya mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi.
Meneja wa Azam, ambaye ndiye mkuu wa msafara wa timu  katika ziara hiyo Jemedari Said alisema Omony na Mieno wameachwa kwa sababu ya kuwa majeruhi na kwamba wachezaji 22 tu ndiyo watakaokuwa katika msafara wao utakaokuwa wa watu 33.
"Msafara wetu wa watu 33 utaondoka kesho saa 5:45 ukiwa na wachezaji 22 kati ya 24 waliosajiliwa msimu huu, Mkenya Humphrey Mieno na Mganda Brian Omony tunawaacha kwa vile ni majeruhi na wanaendelea na matitabu yao wakati wenzao wakienda kujifua," alisema.
Said alisema wengine watakaokuwa katika msafara huo ni benchi la ufundi lenye watu nane na waandishi wa habari watatu na kwamba wakiwa huku watacheza jumla ya mechi nne na timu za Ligi Kuu ya Afrika Kusini  kuanzia Jumatatu.
Azam ambayo itaitumia michezo hiyo minne pia kujiandaa na pambano lao la Ngao ya Hisani dhidi ya Yanga Agosti 17, itaanza kuvaana na Kaizer Chiefs Agosti 5 kabla ya kushuka tena dimbani Agosti 7  kuvaana na Mamelodi Sundowns.
Mchi nyingine itakayocheza timu hiyo itakayoiwakilisha Tanzania kwa mara ya pili kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ni ile ya Agosti 9 itakapovaana na Orlando Pirates na kumalizia kambi yao ya muda nchini humo kwa kupepetana na Moroka Swallows Agosti 12.
Said, nyota wa zamani wa aliyewahi kutamba timu kadhaa ikiwamo Majimaji-Songea, alisema anaamini kambi hiyo itaisaidia timu yao kwa ajili ya maandalizi yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara na pambano lao dhidi ya Yanga litakalochezwa kwenye uwanja wa Taifa.
Alisema mara watakaporejea nchini wataingia kambini moja kwa moja kwa ajili ya pambano hilo la Ngao ya Hisani na mechi yao ya fungua dimba ya Ligi Kuu kati yao na Mtibwa Sugar ambayo itachezwa Manungu Complex, nyumbani kwa wapinzani wao.

No comments:

Post a Comment