BEKI wa kutumainiwa wa timu ya URA ya Uganda, Joseph Owino (kati waliokaa) akitia saini mkataba wa wa kuichezea Simba kwa miaka miwili.
MCHEZAJI wa nafasi ya beki wa kati aliyekuwa akiichezea URA, Joseph Owino hatimaye ametua Msimbazi baada ya jana kusaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Simba.
Owino alisaini mkataba huo jijini Dar es Salaam na kutuliza akili za wanamsimbazi ambao kikosi chao kilikuwa na tatizo la beki wa kati na kutua kwake ni kama amelimaliza tatizo hilo, ikizingatiwa kuwa alishawahi kukipiga katika timu hiyo.
Beki huyo alishaichezea Simba misimu miwili iliyopita kabla ya kuumia na kusajiliwa na Azam ambao walimgharamia matibabu kisha kumuacha na kurejea URA alikoendeleza 'libeneke' kiasi cha kuzifanya timu kadhaa kummezea mate ikiwamo Simba.
Kabla ya kutua nchini Owino alishawahi kuidokeza MICHARAZO kwamba alikuwa tayari kurejea Bongo kukipiga timu yoyote itakayomridhisha kimasilahi na hivyo kutua kwake Msimbazi kumetimiza madai yake hayo, japo awali kulikuwa na taarifa za sintofahamu.
Taarifa hizo zilidai kuwa huenda beki huyo mpole asingerejea Bongo kwa vile alikuwa amepata dili ya mamilioni ya fedha katika nchi za Arabuni na Ulaya ya Mashariki, lakini kutua kwake kumekata kilimilimi chote cha waliodai asingerejea tena Simba.
Simba inayoonyesha imedhamiria msimu huu, pia ilikuwa ikijiandaa kumsainisha beki mwingine wa kimataifa toka Burundi ili kuimarisha safu hiyo ya ulinzi baada ya awali kumnasa Issa Rashid 'Baba Ubaya' toka Mtibwa.
No comments:
Post a Comment