STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, February 15, 2014

Azam wapo tayari kuwavaa Wamakonde, KMKM kufanya maajabu kwa Wahabesh?, KMKM

Azam Fc watakaokuwa ugenini nchini Msumbiji
KMKM ipo nyumbani kurudiana na Wahabeshi

WAKATI ya Yanga na Chuoni yameshafahamika baada ya kucheza jioni ya leo, wawakilishi wengine wa Tanzania, Azam na KMKM zitakuwa kibaruani kesho kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho katika viwanja viwili tofauti.
Azam wenyewe watakuwa ugenini mjini Beira, Msumbiji kukabiliana na wenyeji wao, Ferroviario de Beira katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika wakati KMKM watakuwa uwanja wa Amaan Zanzibar dhidi ya wageni wao kutoka Ethiopia, Dedebit.
Katika mechi zao za awali wiki iliyopita Azam ilipata ushindi mwembamba nyumbani wa bao 1-0 wakati KMKM inayoiwakiliza Zanzibar kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ilifungwa mabao 3-0.
Msemaji wa Azam, Jafar Idd amesema kikosi chao kipo imara kwa ajili ya mechi ya kesho ambapo wanatarajiwa kupata sapoti kubwa ya mashabiki wa Kitanzania kutoka miji mingine ya nchi hiyo iliyopo Kusini mwa Tanzania.
Jafar alisema jiji la Beira kwa sasa gumzo kubwa ji nyota wa Azam, Salum Abubakar, John Bocco 'Adebayor' na Kipre Tchetche ambao kesho watashuka dimbani kuihakikishia Azam ikitinga raundi ya kwanza ya michuano hiyo inayoishiriki kwa mara ya pili mfululizo.
Katika mechi nyingine za michuano hiyo ya Afrika timu ya KCCA ya Uganda imesonga mbele licha ya kulala nyumbani kwa mabao 2-1 dhidi ya El Merreikh ya Sudan baada ya mechi ya awali kushinda ugenini 2-0, Kabuscop ya Angola imeing'oa Cote d'Or ya Seychelles kwa jumla ya mabao 7-2 baada ya leo kuilaza 2-1 wiki moja baada ya kuikung'uta mabao 5-1 mjini Luanda.
Nkana Red Devils ya Zambia iitandika Mbabane Swallows ya Swaziland kwa jumla ya mabao 5-4 baa ya leo kuilaza 5-2, wiki moja baada ya kulazwa 2-0 ikiwa ugenini, huku Rayon Sports ya Rwanda ikishindwa kutamba nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 na AC Leopards ya Congo na kung'olewa kwa faida ya mabao ya ugenini kwani wiki iliyopita walitoka suluhu ya 0-0 ugenini.Hizo ni mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika wakati mechi za Kombe la Shirikisho ukiacha Chuoni kung'oka pia Gaborone United ya Botswana imetolewa na Super Sports kwa jumla ya mabao 3-0 baada ya leo kulala nyumbani bao 1-0 wiki moja baada ya kufungwa ugenini 2-0, Club Kamsar ya Guinea imelazimishwa sare ya 1-1 na Douanes ya Togo na kung'olewa kwa jumla ya mabao 3-1 baada ya wiki iliyopita kulazwa 2-0 ugenini.
Nayo Cob ya Mali imefanikiwa kusonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya leo kushinda 1-0 baada ya sare ya awali ya 1-1 dhidi ya Al Ahli Tripoli, mechi nyingine zinazochezwa leo bado matokeo yake hayajapatikana mpaka sasa, ila MICHARAZO itawaeletea matokeo mara yatakapopatikana.

No comments:

Post a Comment