STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, February 15, 2014

Simba, Mbeya City hapatoshi leo Sokoine

* Mbeya City kukalia kiti cha uongozi leo?
* viwanja vingine vitano kuwaka moto wikiendi hii
Ilivyokuwa hekaheka ya mechi ya kwanza kati ya Simba na Mbeya City

Simba
Mbeya City

Ashanti Utd
JKT Ruvu wapo ugenini jijini Arusha
 
Kagera Sugar watakuwa jiji Dar kuivaa Ashanti
Prisons wageni wa Mtibwa mjini Manungu

Mgambo JKT wapo Tabora kuvaana na Rhino Rangers
Oljoro JKT kuvuna nini kwa JKT Ruvu jijini Arusha?
Ruvu Shooting kuifanyia nini Coastal Union
JIJI la Mbeya leo litasimama kwa muda wakati wenyeji Mbeya City watakapoikaribisha Simba kwenye uwanja wa Sokoine likiwa ni moja ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara inayochezwa leo nchini.
Mechi hiyo inavuta hisia kubwa kuliko hata mechi za kimataifa ambazo timu za Yanga na Azam zilizopo ugenini zitakuwa zikiiwakilisha Tanzania katika kutafuta nafasi ya kufuzu raundi ya kwanza.
Mvuto wa mechi hiyo ya Mbeya unatokana na ukweli kuwa Simba katika mechi zake mbili zilizopita ilionekana kupepesuka, huku Mbeya City inayotajwa kuwa tishio zaidi ikiwa uwanja wa nyumbani ikiwa na kumbukumbu ya kupata sare dhidi ya Mnyama katika mechi yao ya duru la kwanza jijini Dar es Salaam.
Mashabiki wa Mbeya wanaamini Simba leo haitatoka kama walivyoifanyia Mtibwa Sugar au ilipoibana Yanga ilipoenda kucheza nao kwenye uwanja huo mwaka jana.
Hata hivyo mashabiki wa Simba wenyewe wanaamini wameenda Mbeya ili kukata mzizi wa fitina wa kutofungika kwa timu hiyo kwenye uwanja wao wa nyumbani na kutaka kuendeleza ilichokifanya Yanga kwa 'kuitengua udhu' walipoumana nao wiki mbili zilizopita jijini Dar na kuzima rekodi ya kutofungika kabisa licha ya kucheza Ligi Kuu kwa maraya kwanza msimu huu.
Makocha wa timu zote mbili wamenukuliwa wakitambiana kwamba leo ni leo, lakini kwa kuwa mpira ni dakika 90 mashabiki watakuwa na hamu ya kuona mechi hiyo itaishaje.
Simba chini ya makocha Zdrakov Lugarusic na msaidizi wake, Seleman Matola wameapa kupata ushindi ili kurejea kwenye nafasi ya tatu waliyoikalia kwa muda kabla ya Mbeya City kuirejea na kuirudisha Simba nafasi ya nne iliyokuwa inaikamata tangu duru la kwanza lilipoisha.
Kupoteza mchezo huo kunaweza kuitoa Simba kwenye kinyang'anyiro cha ubingwa msimu huu kazi inayowapa wakati mgumu vijana wa Logarusic kukaza msuli Sokoine.
Mbeya City nayo chini ya kocha Juma Mwambusi wameapa kutaka kuizima Simba ili kunyakua pointi tatu na kuzidi kusonga nafasi za juu ili kutimiza ndoto za kutaka kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu katika msimu wao wa kwanza kama walivyowahi kufanya 'kaka' zao Tukuyu Stars mwaka 1987.
Pia ushindi wowote kwa vijana wa Mwmbusi itamaanisha wanaziengua Azam na Yanga zilizopo juu yao na kukalia kiti cha uongozi angalau wiki nzima kwa kuwa itafikisha pointi 37 moja zaidi ya za Azam wanaoongoza sasa na pointi 36 na mbili zaidi ya Yanga wanaokamata nafasi ya pili kwa sasa.
Timu zote zinawategemea nyota wao kadhaa, Simba ikimtambia kinara wa mabao Amissi Tambwe, Ramadhani Singano 'Mess' na Haruna Chanongo, wakati Mbeya City inayoundwa na vijana zaidi ikiwategemea 'wauaji' wao Mwagani Yeya, Paul Nonga, Jeremiah Michael na mkongwe Stephen Mazamba.
Mbali na mechi hiyo iliyo gumzo kwa mashabiki wa soka nchini kote kwa sasa, leo pia kutakuwa na mechi nyingine tano, ambapo Ruvu Shooting itaikaribisha Coastal Union kwenye uwanja wa Mabatini-Mlandizi Pwani, huku Mgambo JKT itakuwa ugenini dhidi ya Rhino Rangers.
Mechi nyingine itazikutanisha timu za Oljoro JKT itakayokuwa uwanja wake wa nyumbani wa Sheikh Amri Abeid kuvaana na maafande wenzao wa JKT Ruvu, huku Ashanti Utd wataialika Kagera Sugar kwenye dimba la Chamazi  jijini Dar es Salaam na Mtibwa Sugar itaikaribisha Prisons-Mbeya uwanja wa Manungu.

No comments:

Post a Comment