STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, February 15, 2014

Yanga na kazi nyepesi Comoro leo


WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga leo inatarajiwa kushuka dimbani ikiwa ughaibuni kwa kuumana na Komorozine ya Comoro katika pambano la marudiano la michuano hiyo.
Mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa kwenye uwanja wa Sheikh Said Mohamed International uliopo mji wa Mitsamihuli na Yanga ina kazi nyepesi ya kukamilisha ushindi mnono iliyopata katika mechi yao ya nyumbani ilipoisasambua Komorozine mabao 7-0.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Comoro zilizoripotiwa na mtandao wa klabu hiyo ni kwamba mara baada ya juzi jioni kufanya mazoezi mepesi katika uwanja mdogo wa hotel ya Retaj, Yanga ilijifua tena jana  asubuhi majira ya saa 5 ausbuhi katika Uwanja wa Sheikh Said kwa ajili ya kuuzoea tayari kwa ajili ya mchezo wa leo.
Kocha mkuu wa Young Africans Hans Van der Pluijm amesema anashukuru kikosi chake kipo vizuri kuelekea mchezo huo na hakuna mchezaji majeruhi hata mmoja hivyo anapata fursa ya kuchagua amtumie nani katika mchezo huo.
Akiongelea wapinzani timu ya Komorozine de Domoni amesema hawajaidharau kwa mechi ya leo kama watu wengi wanavyofikiria, kikubwa amewaandaa vijana wake waeze kufanya vizuri na kupata ushindi, "Kwangu mie hakuna mechi ndogo wala mchezo wa kirafiki" alisema Hans.
Young Africans itashuka dimbani kucheza mchezo huo wa marudiano ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 7-0 iliyoupata katika mchezo wa awali uliofanyika jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika mechi hiyo Mrisho Ngassa alitupia mabao matatu na kushika nafasi ya pili kwa wachezaji wanaoongoza kwa kufunga mabao mengi katika michuano hiyo, ambapo kama leo ataongeza jingine anaweza kujiweka pazuri katika kuwania kiatu cha dhahabu mwishoni ila kama Yanga itasonga mbele mbele ya Al Ahly ya Misri watakaoumana nao kwenye raundi ya kwanza.

No comments:

Post a Comment