STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, February 13, 2014

Yanga kupaa leo bila Kaseja wala Tegete


Mabingwa wa Tanzania, Yanga wanaotarajiwa kuondoka leo mchana kwenda Comoro
KIKOSI cha wachezaji 19 wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara wanaondoka nchini leo mchana kuelekea Comoro kwa ajili ya mechi ya marudiano ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika dhidi ya Komorozine huku nyota kadhaa wakiachwa akiwamo kipa Juma Kaseja na mshambuliaji Jerryson Tegete.
Kaseja, ambaye mwanzoni mwa wiki alifanya mazoezi na wenzake na kisha kubaki kuendelea kujifua na timu ya taifa ya wanawake (Twiga Stars), ameachwa kwa sababu ni mgonjwa na tangu juzi hajafanya mazoezi na wachezaji wenzake, wakati Tegete anauguliwa na mama yake mzazi ambaye yuko jijini Mwanza.
Habari ambazo zimepatikana jijini Dar es Salaam zinaeleza kwamba kipa huyo aliyedaka dakika 90 katika mechi ya kwanza iliyofanyika Jumamosi iliyopita ana matatizo ambayo hawakutaka kuyaweka wazi.
Kwa mujibu wa chanzo cha gazeti hili, wachezaji wengine watakaoachwa katika safari hiyo ni pamoja na Nizar Khalfan, Salum Telela, Hussein Javu, Renatus Lusajo, Shabani Kondo, Bakari Masoud, Ibrahim Job na Emmanuel Okwi ambaye bado amesimamishwa na Shirikisho la Soka Nchini (TFF).
Wachezaji wanaotarajiwa kuondoka leo ni pamoja na Deogratius Munishi 'Dida', Ally Mustapha 'Barthez', Juma Abdul, Oscar Joshua, David Luhende, Nadir Haroub 'Cannavaro', Haruna Niyonzima 'Fabregas', Simon Msuva, Didier Kavumbagu,  Hamis Kizza, Mrisho Ngasa, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Frank Domayo, Athumani Iddi 'Chuji' na Hassan Dilunga.
Benchi la Ufundi linaongozwa na Pluijm na msaidizi wake, Charles Mkwasa, kocha wa makipa, Juma Pondamali, daktari wa timu, Suphian Juma, meneja wa timu, Hafidh Saleh, mtunza vifaa, Mahmoud Omar 'Mpogolo' na mchua misuli, Jacob Onyango.
Viongozi ni Aaron Nyanda na Mohamed Bhinda (Kamati ya Utendaji), Ofisa Habari, Kizuguto na Ramadhan Nassib ambaye ni mkuu wa msafara kutoka Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka (TFF).
Afisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema jana kuwa maandalizi ya safari yamekamilika na timu hiyo itaondoka leo alfajiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Precession.
Hadi jana mchana Kizuguto alisema kuwa taratibu zote za safari zimekamilika ila idadi ya wachezaji wanaondoka bado hawajaipokea kutoka benchi la ufundi.
Wawakilishi hao wa Bara wanaondoka nchini wakiwa na nafasi nzuri ya kusonga mbele kutokana na ushindi mnono wa mabao 7-0 walioupata kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika Jumamosi iliyopita kwenye uwanja wa Taifa.
Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm, amesema kwamba wanakwenda Comoro kusaka ushindi wa pili na hawatabweteka na matokeo waliyopata hapa nyumbani.
Alisema pia wanapaswa kusaka mbinu kali za kuikabili Al Ahly katika raundi ya pili ya mashindano hayo.
Baada ya mazoezi ya timu yake kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam jana asubuhi, Pluijm alisema anaamini timu yake itavuka hatua ya awali kwani iliibuka na ushindi mnono wa kutosha katika mechi yao ya kwanza, hivyo kazi iliyopo mbele yao kwa sasa ni kutafuta mbinu za kuwaua mabingwa hao wa Afrika, Al Ahly ambao watakutana nao baada ya kuing'oa Komorozine.
Raia huyo wa Uholanzi alisema timu yake kwa sasa iko vizuri na ilionyesha kiwango cha juu katika mechi iliyopita lakini bado inahitaji kupikwa zaidi kabla ya kuwavaa Al Ahly ambao walituma mashushushu katika mechi ya Jumamosi kwa ajili ya kuzisoma mbinu za Yanga.
Alisema wapinzani wao katika hatua ya pili ya mashindano hayo, Al Ahly ya Misri wana kikosi kizuri na wana uzoefu mkubwa wa mashindano hayo.
“Tumeonyesha kiwango kizuri katika mechi ya nyumbani, ingawa bado tunatakiwa kwenda Comoro kurudiana na baada ya hapo tunakutana na Al Ahly ya Misri. Naifahamu vizuri timu hiyo maana niliwahi kukutana nayo, lazima ujipange vizuri kabla ya kucheza nao," alisema Pluijm.
“Timu yetu kwa sasa ni nzuri na tunandelea kujipanga vizuri kwa ajili ya mchezo huo kwa sababu lengo letu kubwa ni timu kufika mbali katika mashindano hayo. Nafikiri hayo ndiyo matarajio ya wapenzi wa Yanga na Watanzania kwa ujumla.
“Lakini kwa sasa nafikiri tunapaswa kuelekeza nguvu zetu katika mchezo uliopo mbele yetu dhidi ya Komorozine na baada ya hapo tutawageukia Al Ahly," alisema zaidi kocha huyo ambaye aliwahi kuvaana na Al Ahly wakati akikinoa kikosi cha timu ya Berekum Chelsea ya Ghana.
Endapo Yanga itasonga mbele itakutana na mabingwa wa zamani wa michuano hiyo, Al Ahly ya Misri mapema mwezi ujao.
NIPASHE

No comments:

Post a Comment