STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, March 2, 2014

Simba katika mtihani mwingine mgumu leo Taifa

* Inaivaa Ruvu Shooting iliyopigwa 7-0 na Yanga
* Ashanti Utd kujiuliza kwa Rhino Rangers
* Tambwe kuendelea kucheka na nyavu
Mshambuliaji nyota wa Simba na kinara wa mabao katika ligi kuu, Amissi Tambwe atawanyamazisha Ruvu Shooting leo
BAADA ya Jumapili iliyopita kuangukia pua mbele ya 'maafande' wa JKT Ruvu kwa kutandikwa mabao 3-2, Wekundu wa Msimbazi, Simba leo wanatarajiwa kuwa na kibarua kingine kigumu pale watakapovaana na maafande wengine wa Ruvu Shooting katika mfululizo wa Ligi Kuu.
Pambano hilo litakalochezwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam ni kati ya mechi nne za ligi hiyo iliyopo raundi ya  ya 20 zitakazochezwa leo katika viwanja tofauti na mashabiki wana hamu kubwa ya kutaka kuona Simba itavuna nini kwa maafande hao waliobugizwa mabao 7-0 na Yanga.
Simba inayokamata nafasi ya nne ikiwa na pointi 32 inahitaji ushindi ili kutuliza hasira za mashabiki wao ambao wamekosa amani baada ya timu yao kupata matokeo yasiyoridhisha katika mechi zao nne zilizopita walizoambulia pointi mbili tu huku ikipoteza michezo miwili na kuambulia sare mbili.
Wanachama na mashabiki wa Simba wanaoushutumu uongozi wa Ismail Aden Rage kwa madai ya kuitelekeza timu, huku baadhi wakihisi kuna hujuma zinazofanywa ili timu ifanye vibaya, kitu ambacho kinaweza kutulizwa iwapo Simba itashinda tu leo vinginevyo moto utawaka Msimbazi.
Kocha Zdrakov Logarusic anayeshutumiwa kwa kuchangia kufanya vibaya kwa timu hiyo kitendo chake cha kuwafokea na kuwatulea maneno machafu wachezaji anaweza kukiweka kibarua chake rehani, iwapo Simba itapoteza mechi yao leo kwa Ruvu Shooting inayonolewa na Tom Olaba.
Logarusic amedaiwa amekuwa mkali kupita kiasi hali inayowafanya wachezaji wasijiamini uwanjani na kufanya timu ipate matokeo mabaya, hali inayoweza kuwa mbaya zaidi kama Ruvu itafuata nyayo za 'kaka' zao wa JKT Ruvu kwa kuisulubu vijana wa Msimbazi.
Wachezaji wa Simba chini ya manahodha wao, Nassor Masoud 'Chollo' na Amri Kiemba wameapa kupigana kiume ili kurekebisha makosa, huku wakijaribu kuficha 'siri' juu ya tatizo ambalo linawakabilia wachezaji kwa kudai hawadai wala kucheza chini ya kiwango kwa kudai posho zao.
"Hali hii inatuhuzunisha hata sisi, lakini ni ugumu wa ligi na tutapigana kiume kuona tunashinda mechi zetu zilizosalia za ligi kuu," alisema Chollo alipozungumza na wanahabari wiki hii.
Hata hivyo Msemaji wa Ruvu, Masau Bwire ametamba kuwa, baada ya kuotewa na Yanga jumamosi iliyopita na kubugizwa mabao 7-0 wasingekubali kuona wakifungwa pia na Simba leo.
Bwire alisema kochao kutoka Kenya, Tom Olaba na wachezaji wameuhakikishia uongozi kuwa leo watakufa na Simba ili kunyakua pointi tatu na kujiweka pazuri kwenye msimamo baada ya wiki iliyopita kuteleza kwa mabingwa watetezi na kudai Simba leo hawaponi Taifa.
"Hawaponi. Hatukubali kufungwa kwa mara nyingine tena. Yanga wametudhalilisha vya kutosha na sasa ni zamu ya kurekebisha makosa kwa kuichabanga Simba kwenye uwanja wa Taifa," alisema.
Ukiondoa mechi hiyo ya Simba na Ruvu, leo pia kutakuwa na mechi nyingine nne zitazikutanisha timu nane ambapo Kagera Sugar itakuwa nyumbani kuikaribisha JKT Ruvu  uwanja wa Kaitaba, Kagera huku Rhino Rangers itakakuwa wageni wa Ashanti United kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam na Prisons Mbeya itaikaribisha Mgambo JKT kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2013-2014     
                                  P    W     D     L    F     A   GD  PTS
01.Azam                    18   11    07   00   35   12   23  40
02.Yanga                   17   11    05   01   41   12   29  38
03.Mbeya City           20   09    09   02   24   16   08  36
04.Simba                   19   08    08   03   35   19   16  32
05.Kagera Sugar        19   06    08   05   16  15   01  26
06.Coastal Union        19   05    10    04  14  09   05  25
07.Mtibwa Sugar       19   06    07    06   23  23   00  25
08.Ruvu Shooting       19  06    07   06    20  26  -06  25
09.JKT Ruvu             19   07    01    11   16  29  -13  22
10.Prisons                  18   04    08    05   17  18  -01  20
11.Mgambo               19   05    05    09   12  27  -15  20
12.Oljoro                   21   02    10    09   15  30  -15  16
13.Ashanti                 19   03    05    11   15  34  -19  14
14.Rhino Rangers      19   02    07    10   12  23  -11  13
 
Wafungaji:

17- Tambwe Amisi (Simba)
10- Kipre Tchetche (Azam)
09- Elias Maguri (Ruvu Shooting) Hamis Kiiza, Didier Kavumbagu (Yanga)
08-Juma Luizio (Mtibwa Sugar), Mrisho Ngassa (Yanga)
07- Peter Michael (Prisons)
06- Themi Felix (Kagera Sugar), Mwegani Yeya (Mbeya City)
05- Tumba Sued (Ashanti Utd), Jerry Santo (Coastal Union)
04- Jerry Tegete (Yanga), Jonas Mkude, Betram Mombeki (Simba), Bakar Kondo, Salum Machaku (JKT Ruvu), Jerome Lambele (Ruvu Shooting), Abdallah Juma (Mtibwa Sugar)

No comments:

Post a Comment