STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, March 2, 2014

Titina: Dansa Extra Bongo anayetamani kuwa kama Mbilia Bel

Titina katika pozi
BAADA ya miaka 14 ya kunengua jukwaani katika bendi mbalimbali, dansa Titi Mwinyiamiri maarufu kama 'Titina' anasema anatamani kwa sasa kuwa muimbaji ili kuupumzisha mwili wake.
Mnenguaji huyo wa bendi ya Extra  Bongo anasema tayari ameanza kujifunza kuimba ili kutimiza ndoto zake kama baadhi ya madansa wa zamani ambao walikuja kutamba kimataifa katika fani ya uimbaji.
"Natamani kuwa muimbaji mkubwa, nataka kuupumzisha mwili baada ya kunengua kwa miaka karibu 14 tangu mwaka 2000 nilipojitosa rasmi katika fani hii," anasema.
Mwanadada huyo anasema kipaji cha uimbaji na sauti nzuri anayo japo hakuitilia maanani kipindi akiwa shuleni wakati alipokuwa akiimba kwaya na bendi ya shule.
Titina anasema kwa miaka ya sasa waimbaji wa kike wapo wachache jambo ambalo linamhamasisha kutamani kuwa muimbaji ili kupunguza pengo lililopo baina ya wanamuziki wa kike na kiume.
"Siku za nyuma asilimia kubwa ya bendi za muziki wa dansi zilizokuwa na waimbaji wa kike, siku hizi ni bendi chache pengine kutokana na uchache wa waimbaji hao, hivyo nataka kupunguza pengo hilo."
Anasema anaamini kwa kipaji alichonacho katika sanaa kitamfikisha mbali kama ilivyokuwa kwa Mbilia Bell, Tshalla Mwana na hata Luiza Mbutu walioanzia katika uneguaji kabla ya kugeuka waimbaji mahiri.
"Naamini bidii yangu itanifikisha kule ilipowafikisha waimbaji kadhaa nyota waliokuja kutamba kimataifa wakitokea kwenye unenguaji kama ilivyokuwa kwa akina Tshalla Mwana au Yondo Kusala," anasema.

MAFANIKIO
Titina anayependa kula wali kwa kuku wa kienyeji na kunywa soda ya Novida, anasema licha ya watu wengi kuidharau fani ya sanaa hasa unenguaji, yeye anaiheshimu kwa mafanikio makubwa aliyoyapata.
KImwana huyo anasema sanaa hiyo imemwezesha kumiliki saluni za kike na ya kiume, kumjengea nyumba mama yake ambaye hata hivyo ameshafariki na pia kumiliki viwanja viwili kitu anachojivunia.
"Kwa kweli nashukuru Mungu kazi hii imenisaidia kwa mengi kiasi kwamba naiheshimu na hata ninapoona watu wanaibeza nashindwa kuwaelewa kwa sababu ni kazi kama kazi nyingine," anasema.
Titina anasema pamoja na mafanikio hayo, lakini bado hajaridhika na badala yake anatamani afike mbali zaidi ili hapo baadaye aje kujikita kwenye biashara wakati umri utakapokuwa umetupa mkono.
"Sijaridhika kabisa, japo nashukuru kwa mafanikio haya ila napenda Mungu anisaidie nifike mbali zaidi," anasema.
nilipofikia,"  kwa vile wapo watu wengine hawana mafanikio kama haya niliyonayo," anasema.
HUZUNI
Titina ambaye pia ni msusi wa nywele na mfumaji wa vitambaa vya uzi, anasema hakuna tukio linalomsikitisha mpaka sasa kama tukio la kufiwa na mama yake wakati akiwa ughaibuni.
"Tukio lenyewe limenitokea mwaka jana baada ya kupata safari ya kwenda kutumbuiza Dubai, Falme za Kiarabu ambapo wiki chache baada ya kupata visa nilifahamishwa mama yangu kadondoka."
"Wiki moja baadaye nikafahamishwa kuwa mama yangu amefariki dunia kwa kweli roho iliniuma, inaniuma na itaendelea kuniuma kwa vile mwanae nilikuwa natafuta riziki kwa ajili yake," anaongeza.
Titina anasema tukio hilo linamliza kila akilikumbuka, huku akisema furaha yake ni jinsi mpenzi wake anavyopenda, kumheshimu na kumjali kama mkewe na huchukia kumsaidia mtu kisha asiwe na shukrani kwa kumsema vibaya mitaani.
Mnenguaji huyo anawataka wasanii wenzake kujiheshimu, kupendana na kusaidiana, anasema sanaa ya muziki Tanzania bado ipo chini kwa kukosa sapoti kubwa toka serikali na hata kwa wadau wake.
"Kwa Bongofleva na taarab kuna nafuu fulani, siyo muziki wa dansi hivyo ni vyema serikali na wadau wakaupiga tafu muziki huo ufike mbali zaidi," anasema.
"Wapo baadhi ya watu hukosa shukrani pale unapowasaidia kwa kukusema vibaya, wananiudhi sana watu wa hivi na kukatisha tamaa kutoa msaada kwa wengine," anasema.

WATOTO WA MBWA

Titina anayewakubali waimbaji Nyoshi el Saadat na Ally Choki, pia anaiangukia serikali juu ya vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na kundi la Watoto wa Mbwa wanaowanyima raha wakazi za maeneo ya Ilala.
"Hili kundi linalojiita 'Watoto wa Mbwa' wanatunyima raha kwa vitendo vyao vya ukabaji na uporaji wakati mwingine mchana kweupe kiasi cha kushindwa kuishi kwa amani, serikali itusaidie," anasema.
Anasema anaamini serikali kwa kutumia jeshi la Polisi wakiwavalia njuga 'wahuni' hao wanaweza kuwafanya waishi kwa uhuru na amani kama wakazi wa maeneo mengine.
"Wanatukosesha raha, yaani kila unapokuwa unatoka kibaruani unakuwa na hofu kurejea nyumbani kwa kuwafikiria vijana hao waliotawala eneo la Kiwalani na wilaya ya Ilala kwa ujumla," anasema.
KIPAJI
Titi Mwinyiamiri, alizaliwa Oktoba 10, 1980 mjini Bagamoyo akiwa ni mtoto wa 10 kati ya 11 wa familia yao. Alisoma Shule ya Msingi Magomeni Makuti ambapo alianza kuonyesha kipaji cha sanaa.
Hata hivyo alijitosa rasmi kwenye fani hiyo mwaka 2000 akianzia bendi ya Double M Sound ya Mwinjuma Muumin, kisha akatua African Stars 'Twanga Pepeta' na baadaye akaenda FM Academia.
Baada ya kutamba FM alihama bendi hiyo na kutumia Extra Bongo alikonako mpaka sasa na kudai ni mahali anapofurahia maisha yake ya sanaa kwa namna wasanii wanavyothaminiwa na 'mabosi' wao.

No comments:

Post a Comment