STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, April 1, 2014

Fully Maganga ashukuru kutimiza ahadi kuitungua Yanga

Fully Maganga akiwajibika uwanjani
MSHAMBULIAJI nyota wa Mgambo JKT, Fully Maganga, amesema amefurahi na kumshukuru Mungu kwa kufanikiwa kutimiza ahadi yake ya kuwatungua Yanga kwenye uwanja wa Mkwakwani kama alivyoahidi.
Maganga alinukuliwa na MICHARAZO mara alipotoka kuwatungua Simba katika  pambano lao lililochezwa Februari 9, akidai ni lazima angeifunga Yanga na kufanikiwa kufanya hivyo Jumapili Mgambo walipoilaza Yanga mabao 2-1.
Mchezaji huyo alisema anajiamini kwa uwezo wake mkubwa kisoka na ndiyo maana alitoa onyo mapema na anashukuru kufanikiwa kutimiza ahadi hiyo kwa kuiwezesha Mgambo kuwanyamazisha watetezi hao kama Simba.
"Namshukuru Mungu kwa kunisaidia kutimiza ahadi yangu, niliitahadharisha Yanga kwamba ni lazima nitawatungua, nadhani walipuuza na wamekiona kilichowakura Jumapili. Nimefurahi sana kuwafunga," alisema.
Alisema anaamini bao lake lililokuwa la mapema katika pambano hilo ndilo lililowachanganya watetezi hao na kujikuta wakipoteza mchezo huo uliokuwa wa pili kwao kwa msimu huu baada ya Azam kuwafanyizia duru la kwanza.
"Nadhani bao langu liliwavuruga Yanga na kushindwa kujipanga na hilo lilitusaidia kuwazima na kuwapotezea mipango yao ya ubingwa, ingawa bado wanayo nafasi kama wakijipanga vyema kwa mechi zilizosalia," alisema.
Yanga iliyokuwa ikihitaji ushindi katika mchezo huo wa Jumapili ilijikuta ikilala 2-1 licha ya wapinzani wao kucheza pungufu kwa muda mrefu baada ya mashambuliaji wao Mohammed Netto kulimwa kadi nyekundu kwa tuhuma za kuwa na kitu kwenye jezi yake.

No comments:

Post a Comment