STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, April 1, 2014

Maria Soloma; Kimwana wa Manywele anayetamba Extra Bongo

Maria Soloma

Akiwajibika jukwaani
SHINDANO la Kimwana wa Manywele wa Twanga Pepeta la 2006-2007 ndilo lililomuibua mwanadada Maria Joseph Soloma.
Katika shindano hilo, Maria alifanikiwa kushika nafasi ya pili nyuma ya Lulu Mathias Semagongo maarufu kama Aunty Lulu na kuacha gumzo kubwa kwa umahiri wake wa kuzungusha nyonga jukwaani.
Licha ya kutoibuka kidedea katika shindano hilo, lakini kipaji kikubwa alichokuwa nacho kilimsaidia kupata 'ulaji' mwanadada huyo baada ya  bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' kumpa ajira ya kudumu.
Maria alichukuliwa na Twanga Pepeta kama mnenguaji na kukaa na bendi hiyo mpaka hivi karibuni alipoamua kuhama na kutua Extra Bongo 'Wana Kimbembe'.
Kisura huyo aliyejiwekea malengo ya kuja kuwa muimbaji mara baada ya viungo vyake kuchoka kunengua, anasema masilahi na kutaka kubadilisha hali ya hewa ndicho kilichomhamisha Twanga Pepeta.
"Masilahi na kutaka kubadili hali ya hewa vilinifanya niondoke Twanga na kutua Extra Bongo. Nafurahi maisha ndani ya Extra ni mazuri, kuna ushirikiano wa kutosha na tunaishi kama ndugu," anasema.

DHANA
Maria anayefurahishwa na tukio la kujifungua mwanae kipenzi, Zahra aliyezaa na muimbaji nyota nchini, Mwinjuma Muumin, anasema hujisikia vibaya jinsi jamii inavyojenga dhana mbaya dhidi ya wasanii.
Anasema baadhi ya wanajamii wamekuwa wakiwadharau wasanii wa kike na kuwachukulia kama watu wanaojiuza bila kujua kwamba sanaa ni kazi yao kama kazi nyingine zinazowaingizia watu riziki zao.
"Kwa kweli jambo hilo huwa silifurahii kwani ni sawa na udhalilishaji, hata kama kuna watu wachache kati yetu wanafanya uhuni, hiyo isichukuliwe ni tabia ya watu wote," anasema.
Anasema suala la wahuni kama kwenye maofisi wapo kutokana na hulka ya mtu na kusisitiza sanaa ni kazi kama kazi nyingine na yeye anaiheshimu kwa vile imemsaidia kwa mengi kimaisha.
Maria anayelizwa na vifo mfululizo vya familia yake ikiwamo cha baba yake na dada zake wawili, anasema hata hivyo kuna haja ya wasanii wenzake kujiheshimu na kuepuka mambo ya upuuzi ili waheshimiwe.
"Kama tusipojiheshimu sisi wenyewe ni vigumu kuheshimiwa, baadhi ya matendo ya wenzetu kwa kutojiheshimu imefanya tudharauliwe na kuonekana wote ni wahuni kitu ambacho siyo cha kweli," anasema.
Anasema kutojiheshimu kwa wasanii na kujihusisha na mambo ya hovyo imechangia wazazi na walezi kuwabania watoto wao wenye vipaji kujiingiza kwenye sanaa kwa hofu ya kuharibikiwa.

KIPAJI
Maria ambaye ni shabiki mkubwa wa Simba anayependa kula ugali kwa mlenda, anasema kipaji cha sanaa alianza kukidhihirisha tangu akiwa shule ya msingi.
Anasema alikuwa akiimba na kucheza ngoma, kuimba kwaya na kuigiza, lakini alikuja kujikita kwenye unenguaji kwa kuvutiwa na Lilian Internet na Aisha Madinda aliwahi kufanya nao kazi Twanga Pepeta.
"Hawa ndiyo waliochochea mimi kujikita kwenye unenguaji, ndipo mwaka 2006 nilipoingia kwenye shindano la Manywele na kuanzisha safari ndefu mpaka hapa nilipo," anasema.
Anasema kiu yake kubwa ni kufika mbali kisanii na hasa kuja kuwa muimbaji akidai ameanza kujifunza taratibu ndani ya bendi yake ya Extra Bongo.
Maria, anayewashukuru watu wote waliomsaidia kufika alipo anasema muziki wa Tanzania unazidi kupiga hatua kubwa, jambo bado kuna tatizo la kukosekana ubunifu unaoweza kuutrangaza kimataifa.
"Lazima wasanii na wanamuziki wawe wabunifu zaidi ili kuhimili ushindani wa soko la kimataifa," anasema.
Pia anavitaka vyombo vya habari kutoa nafasi sawa kwa miondoko yote ya muziki badala ya kuegemea kwenye muziki wa kizazi kipya tu na taarab na kuutupa mkono dansi na muziki asilia.
Kadhalika aliiomba serikali kusaidia kuwapigania wasanii kuepukana na unyonyaji na wizi wanaofanyiwa na baadhi ya watu waliohodhi soko la sanaa nchini ili wasanii waweze kunufaika na jasho lao.
===============

No comments:

Post a Comment