STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, April 1, 2014

Ulaya ni vita leo Man Utt vs Bavarians, Barca vs A. Madrid

Lionel Messi kufanya nini leo kwa Atletico Madrid>
Watetezi Bayern Munic watavuna nini Old Trafford

Mashetani Wekundu watawamudu Bavarians leo nyumbani kwao>
KIVUMBI cha Ligi ya Mabingwa kinatarajiwa kuendelea tena leo kwa michezo ya hatua ya Roibo Fainali kuanza ambapo mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Bayern Munich ya Ujerumani itakuwa ugenini kuvaana na Manchester United.
Wakichechemea kwenye nafasi ya saba ya msimamo wa Ligi Kuu ya England kufuatia msimu mbaya wa kwanza chini ya kocha David Moyes, Man U hawapewi nafasi katika mechi zao mbili za robo fainali dhidi ya miamba hao wa Ujerumani ambao tayari wameshatwaa ubingwa wa msimu huu wa Bundesliga.
Moyes atakuwa na matumaini kidogo kufuatia matokeo ya wikiendi wakati mwendo wa Bayern wa kushinda mechi 19 uliposimamishwa na sare ya 3-3 nyumbani dhidi ya Hoffenheim baada ya kupoteza uongozi wao wa magoli 3-1 huku Man U ikiisambaratisha Aston Villa 4-1 kwenye Ligi Kuu.
Man U haifanani kabisa na timu ambayo ilikuwa ikitisha Ulaya chini ya utawala wa Alex Ferguson lakini kiwango chao cha nyumbani katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu huu kimekuwa cha kuvutia, tofauti na rekodi yao mbaya Old Trafford kwenye ligi kuu ya England.
Mabingwa hao wa England wameshinda mechi zao nne za kwanza katika michuano hiyo ya Ulaya msimu huu, jambo ambalo walilifanya mara ya mwisho katika msimu wa 2007-08 wakati waliposhinda mechi nne kati ya sita na kwenda kutwaa kombe hilo mjini Moscow.
Lakini Bayern, inayofundishwa na Pep Guardiola ambaye aliisambaratisha Man U katika mechi za fainali mwaka 2009 na 2011 akiwa kocha wa Barcelona, imeshinda mechi zao saba zilizopita za ugenini katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya. Pia waliwang'oa Man U kwa sheria ya magoli ya ugenini katika hatua kama hiyo 2010.
"Hatuwezi kuruhusu hali waliyonayo Manchester United kwenye ligi kuu kwa sasa iathiri mtazamo wetu kwenye mechi hii," nahodha Bayern, Philipp Lahm aliiambia uefa.com.
"Tutaenda Manchester ili kucheza mpira wa kushambulia na kufunga magoli. Sidhani kama inajalisha kwamba umecheza kwanza mechi ya ugenini. Mwaka jana tulicheza mechi zetu nyingi za kwanza nyumbani na bado tukatwaa kombe.
"Jambo la muhimu zaidi kwetu ni kufunga magoli katika mechi ya ugenini," aliongeza Lahm, ambaye kikosi chake iliwang'oa Arsenal kwa kutumia magoli ya ugenini katika hatua ya 16-Bora msimu huu.
Moyes anaweza kubeba ushujaa waliouonyesha katika hatua iliyotangulia ya 16-Bora wakati walipolala 2-0 ugenini dhidi ya Olympiakos Piraeus kabla ya kushinda 3-0 nyumbani Old Trafford, shukrani kwa 'hat-trick' ya Robin van Persie.
Van Persie atakosa mechi zote mbili dhidi ya Bayern kutokana na kuwa majeruhi lakini Wayne Rooney amekuwa katika kiwango kizuri, kilichomshuhudia mshambuliaji huyo Muingereza akifunga magoli mawili dhidi ya Villa na kufikisha jumla ya mabao matano mwezi uliopita na 15 katika ligi msimu huu.
Moyes haoni kama kucheza mechi ya kwanza nyumbani kama ni faida kwa wapinzani.
"Kwa mechi zinavyokwenda sasa kwa soka la mashambulizi ya kustukiza na mbinu tofauti za kukabili mchezo zinazotumiwa na timu zinazocheza ugenini (inamaanisha hamna umuhimu)," alisema.
Mechi hiyo inazikutanisha timu mbili ambazo zimetwaa ubingwa wa Ulaya mara nane jumla na walikutana katika fainali ya 1999 mjini Barcelona ambako Man U walipata ushindi wa kukumbukwa wa 2-1 kwa magoli ya dakika za lala-salama.
Kipigo hicho kiliwatafuna Bayern kwa miaka mingi lakini wamekuwa wakiwafunga Man U kila walipokutana nao tangu wakati huo na itakuwa ni miujiza kama Wajerumani hao watashindwa kutinga nusu fainali.

BARCA v ATLETICO MADRID
Mechi nyingine ya robo fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya leo itakuwa ni baina ya Barcelona na Atletico Madrid, itakayokumbushia upinzani wa kocha Gerardo Martino na Diego Simeone waliokuwa nao wakati wote wakicheza soka kwao Argentina.
Simeone alikuwa hajafikisha umri wa miaka 18 wakati alipokabiliana na Martino, ambaye amemzidi umri kwa takriban miaka 10, katika mechi ya ligi baina ya timu ya Velez Sarsfield na Newell's Old Boys Januari 1988, na kumshuhudia Martino akitolewa kwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu kiungo mwenzake Simeone, ambaye naye pia alitolewa kwa kadi nyekundu dakika 10 baadaye.
Simeone ambaye si mgeni katika matukio ya utata wakati akicheza soka -- kumbuka alivyohusika katika kumfanya kiungo wa timu ya taifa ya England, David Beckham atolewe kwa kadi nyekundu katika mechi ya Kombe la Dunia 1998 -- alikiri mwaka jana kwamba alidanganya kaumia ili kumsababishia kadi nyekundu Martino.
Takriban miongo mitatu baadaye, Martino na Simeone wanaziongoza timu mbili za Hispania zenye nafasi adimu ya kutwaa mataji mawili ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya na La Liga.
Atletico wako pointi moja juu ya Barca kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Hispania huku mechi saba zikiwa zimesalia ligi kumalizika na mechi yao mwisho msimu huu ni safari nyingine ya kwenda kuwakabili Barca kwenye Uwanja wa Nou Camp mwezi Mei.
Tayari timu hizo zimeshakutana mara tatu msimu huu, huku matokeo yote yakiwa ni sare.
Barca waliwashinda Atletico katika mechi ya ufunguzi wa msimu ya Kombe la Super Cup wakati goli la Neymar katika sare ya 1-1 katika mechi ya kwanza mjini Madrid lilipotosha kuwapa taji Barca baada ya timu hizo kutoka sare ya 0-0 katika mechi ya marudiano Nou Camp. Mechi yao ya La Liga kwenye Uwanja wa Calderon mwezi Januari pia ilimalizika kwa sare ya bila magoli.
Wakati Diego Costa yuko katika kiwango cha juu, kikosi cha Diego Simeone kitalazimika kumchunga vyema Lione Messi ambaye amewafunga magoli 20 katika mechi 19 dhidi Atletico, zikiwamo 'hat-trick' tatu.
Washindi wa raundi hii baada ya mechi za marudiano zitakazopigwa wiki ijayo, wataingia katika 'droo' ya nusu fainali itakayopangwa Aprili 11.
Kesho, Real Madrid watawavaa Borussia Dortmund, wakati PSG watawakaribisha Chelsea.

No comments:

Post a Comment