Abdi Banda kazini |
Abdi Banda akichuana na Salim Kinje wa Simba katiuka ligi ya msimu uliopita |
Beki huyo chipukizi aliyejaliwa umbile refu lenye nguvu na lililojengeka kimichezo, amekuwa gumzo tangu aanze kuonekana kwenye ligi kuu ya Bara msimu uliopita.
Kipaji kikubwa cha soka, uwezo wa kupiga chenga, mbio na umahiri wa kukaba washambuliaji wasumbufu imemfanya beki huyo kutokosekana kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo kilichosheheni nyota.
Cha ziada alichonacho beki huyo ambaye huenda Simba inaendelea kumuota baada ya kipigo cha cha 1-0 kutoka kwa Coastal wiki iliyopita, ni kipaji cha kufumania nyavu.
Msimu huu nyota huyo mwenye ndoto za kucheza soka la kulipwa nje ya nchi amefunga bao moja na msimu uliopita alifunga mabao mawili.
Katika pambano dhidi ya Simba, Banda alishirikiana na mabeki wenzake kuwafunika nyota wa Msimbazi walioongozwa na Amissi Tambwe, Haruna Chanongo na Ramadhani Singano 'Messi'.
Licha ya kuwazima Simba, Banda anasema mechi anayoikumbuka ni ile ya duru la kwanza dhidi ya Yanga iliyochezwa Uwanja wa Taifa na Coastal kuchomoa bao 'jioni' kwa penalti, na kuibua vurugu kubwa kutoka kwa mashabiki wa mabingwa watetezi hao.
"Tukio lile la kuchomoa bao na kuwakera mashabiki wa Yanga kiasi cha kulishambulia gari letu na kulivunja kioo linanifanya niikumbuke mechi ile iliyoisha kwa sare ya 1-1," anasema.
Banda, 19, anasema soka la Tanzania linaweza kupanda kama vijana wakipewa nafasi.
Beki huyo aliyekuwa akivutiwa kisoka na marehemu Patrick Mafisango, anasema mfumo wa soka la vijana ukipewa nafasi zaidi utaleta ukombozi na kurejesha heshima kimataifa.
Pia aliwataka viongozi wa soka nchini kuwathamini wachezaji wazawa badala ya kuendekeza tabia za kuwazimia 'mapro' hata kama wana viwango ambavyo havitofautiani na vya wachezaji wa nyumbani.
Banda alipitia katika mfumo wa ukuzaji soka kwa vijana akianzia Kombez Academy na Africans Sports kabla ya kutua Coastal.
Anasema akiwa Africans Sports ndiyo alipopewa misingi imara ya soka, hasa baada ya kuwa chini ya ulezi na umeneja wa Abdul Bosnia.
"Siwezi kumsahau Abdul Bosnia, kocha Khalfan aliyeninoa Kombez na familia yangu ambayo imekuwa ikinipa sapoti; wakinitia moyo katika mbio zangu za kufika mbali kisoka," anasema.
Banda anawataka wachezaji wenzake kuzingatia nidhamu ndani na nje ya uwanja, kupenda kufanya mazoezi na kupigana 'jihad' uwanjani ili kuzisaidia timu na kujitangaza wenyewe sokoni.
Banda anasema Taifa Stars inaweza kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwakani kama ikitafutiwa mechi nyingi za kujipima nguvu za ndani na nje ya nchi.
Mchezaji wa kimataifa huyo alikuwemo katika kikosi cha timu ya taifa ya shirikisho la soka, 'TFF Stars', kilichocheza mechi ya kirafiki dhidi ya Namibia na kutoka sare 1-1 jijini Windhoek mapema mwezi huu.
Anasema uteuzi huo wa 'TFF Stars' ndilo tukio la furaha kwake kwani kabla ya hapo hakuwahi kuitwa hata timu za taifa za vijana na kuwashukuru viongozi wa TFF waliotambua kipaji chake na kumpa nafasi hiyo.
No comments:
Post a Comment