STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, April 22, 2014

Wanaoibeza Azam wana wivu-Himid Mao

Himid Mao
BAADHI ya nyota wa klabu ya Azam wamesema wanaowaponda kwa kufanikiwa kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania ni wasiokubali kushindwa na wenye dhana kuwa nje ya Simba na Yanga hakuna bingwa.
Azam iliweka rekodi ya kunyakua taji hilo baada ya misimu miwili mfululizo ikiishia kuambulia nafasi ya pili nyuma ya Simba na Yanga na kuwa klabu ya tisa kunyakua ubingwa huo tangu mwaka 1965.
Hata hivyo kabla na hata baada ya kunyakua taji hilo kumekuwa na kauli za kejeli dhidi ya mafanikio ya klabu hiyo, kitu kilichowakera baadhi ya nyota wa Azam waliodai wanaoponda wanawaonea gere.
Nahodha msaidizi wa klabu hiyo, Himid Mao, alisema mashabiki wa soka walipaswa kuipongeza Azam kwa kuonyesha ushindani wa kweli na kuweza kuzisimamisha Simba na Yanga na kuleta mapinduzi.
Mao, alisema Azam imechangia kuzika 'ligi ya klabu mbili' na kuonyesha kuwa kumbe hata timu nyingine zinaweza kuwa mabingwa kama zikijipanga, hivyo kupondwa kwao ni kuwakatisha tamaa.
"Nadhani wanaofanya hivyo wanasumbuliwa na wivu wa mafanikio yetu na pia kushindwa kuamini kuwa nje ya Simba na Yanga bingwa anaweza kupatikana tena kwa kuweka rekodi kama wao," alisema.
Alisema anaamini kuwepo kwa Mbeya City na kuongezeka kwa timu kama Ndanda Fc na Stand United kunaweza kuongeza chachu iliyoanzishwa na Azam ili kuifanya ligi iwe na utamu wa kusisimua.
"Ligi ya timu chache haivutii, ndiyo maana leo ligi ya England inavutia na kufuatiliwa kwa sababu haitabiriki kwa ushindani uliopo bila hadhi ya klabu, tumeonyesha uwezo tuungwe mkono tusikatishwe tamaa," alisema Mao mmoja wa 'nguzo' ya Azam tangu ipande daraja.

No comments:

Post a Comment