Juma Mwambusi |
Hans Van der Pluijm |
Joseph Omog |
Azam imetwaa taji hilo kwa mara ya kwanza baada ya kufikisha pointi 62 na kuingia kwenye rekodi ya kuwa klabu ya tisa nchini kunyakua ubingwa nchini.
Baada ya ligi hiyo kumalizika, mashabiki wa soka wana hamu kubwa ya kutaka kujua nani atakayeibuka kuwa Mfungaji Bora, Mchezaji Bora na Kipa Bora wa ligi ya msimu huu.
Makocha Juma Mwambusi wa Mbeya City, Hans van der Pluijm wa Yanga na kocha wa Azam Joseph Omog walioziongoza timu zao kushika nafasi tatu za juu wanapewa nafasi kubwa kutwaa tuzo hiyo.
Katika msimu uliopita, kocha Abdallah Kibadeni aliyekuwa akiinoa Kagera Sugar aliibuka kidedea na kunyakua tuzo hiyo baada ya kuiwezesha Kagera Sugar kushika nafasi ya nne, ingawa msimu huu nafasi ya kuitetea inaonekana kuwa ndogo kwa hali ilivyo.
Kocha huyo aliyekuwa akiifundisha Simba, alitimuliwa na kuhamia Ashanti United ambayo ameshindwa kuikoa isirejee Ligi Daraja la Kwanza.
Mwambusi anapewa nafasi zaidi kwa kuipandisha daraja Mbeya City na kuifanya iwe tishio katika ligi licha ya ugeni wake na kumaliza katika nafasi ya tatu ikizidiwa na klabu za Azam na Yanga tu.
Omog aliyechukua nafasi ya Stewart Hall aliyetimuliwa na Azam baada ya kumalizika kwa duru la kwanza naye anapigiwa chapuo kama ilivyo kwa Pluijm wa Yanga aliyeinoa pia duru la pili tu.
Kabla ya hapo Yanga ilikuwa chini ya Mholanzi mwingine, Ernie Brandts aliyetimuliwa baada ya Yanga kufungwa kwenye mechi ya 'bonanza' ya Nani Mtaji Jembe.
Kwa upande wa Mchezaji Bora msimu uliopita alikuwa Kelvin Yondani na kipa akiwa Burhan aliyekuwa Prisons, je msimu huu tuzo hizo zitaenda wapi miongoni mwa wachezaji waliong'ara katika ligi hiyo?
Bila shaka mashabiki wana hamu kubwa ya kuona wachezaji wanaoamini walifanya vyema msimu huu wakinyakua tuzo hizo kama ilivyo kwa makocha na wachezaji chipukizi waliong'ara msimu huu.
Kwenye tuzo ya Mfungaji Bora nafasi ilikuwa ikionekana wazi ikielekea mikononi mwa Mrundi, Amissi Tambwe wa Simba aliyemaliza na mabao 19.
Je, Joseph Kimwaga atatetea tuzo yake ya Mchezaji Bora chipukizi katika msimu huu?Tusubiri tuone baada ya Bodi ya Ligi Tanzania pamoja na wadhamini wake kampuni ya Vodacom watakapoweka bayana orodha katika tuzo hizo kwa msimu wa 2013-2014.
No comments:
Post a Comment