KIUNGO Yohan Cabaye nyota wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Ufaransa PSG, Yohan Cabaye anajiandaa kunyakua taji lake la pili la ligi hiyo iwapo timu yake hiyo itapata ushindi katika pambano lao dhidi ya Sochaux litakalochezwa Jumapili.
PSG imebakisha pointi tatu tu kutetea taji hilo baada ya jana kupata ushindi mwembamba dhidi ya Evian TG na kuzidi kuikimbia Monaco, wapinzani wao wa karibu waliopo nafasi ya pili na waliowaacha kwa pointi 10 huku ligi ikisaliwa na mechi nne kabla msimu haujafungwa.
Cabaye aliyesajiliwa kwenye usajili wa majira ya baridi akitokea Newcastle United ya Uingereza anasema atakuwa mwenye furaha iwapo PSG itatwaa taji hilo ambalo kwake itakuwa ni mara ya pili baada ya kunyakua mara ya kwanza mwaka 2011 akiwa na Lille.
Mkali huyo anayeichezea pia timu ya taifa ya Ufaransa, anasema angependa kuongeza medali nyingine ya dhahabu katika chumba chake kupitia PSG.
"Tuna hamu kubwa ya kupata mafanikio ya kunyakua taji hilo na kitu hicho ni muhimu sana kwangu," alisema Cabaye, 28 na kuongeza; "Itakuwa vyema kama nitanyakua ubingwa huo nikiwa na PSG."
Mwishoni mwa wiki Cabaye alifanikiwa kunyakua Kombe la Ligi wakati PSG ilipoicharaza Olympique Lyon mabao 2-1 kwa mabao la Edinson Cavani na kudai ingawa hajawahi kunyakua Kombe la Ligi au Kombe la Mfalme mara mbili, lakini katika ligi anaamini itafanikiwa na anajiandaa kushangilia furaha ya ushindi huo anaousubiri kwa hamu.
No comments:
Post a Comment