MWISHO wa tambo na mikwara baina ya Azam na Yanga ni leo wakati klabu hizo mbili zitakapopepetana kwenye mechi ya Nf\gao ya Jamii kuashiria kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Timu hizo zitapambana kwenye uwanja wa Taifa, huku zote zikiwakosa baadhi ya nyota wake kutokana na kuwa majeruhi.
Yanga inatarajiwa kumkosa kiungo wake mahiri, Andrey Coutinho aliyeumia katika mechi ya kirafiki dhidi ya Polisi Dar es Salaam kwenye uwanja wa sekondari ya Loyola.
Mshambuliaji huyo alipatwa na maumivu hayo wakati alipokuwa akijaribu
kupiga mpira na hivyo kushindwa kuendelea na mchezo. Timu hizo zilitoka
suluhu.
Azam ambao walilala bao 1-0 katika mechi kama hiyo kwa msimu uliopita, haitakuwa na huduma ya nahodha wake, John Bocco Adebayor aliye majeruhi pia, kwa mujibu wa Meneja wa Azam Said Jemedari.
“Tunao majeruhi wawili, ambao hawatakuwepo kwenye programu ya mchezo wa
Ngao ya Jamii, ambao ni beki Waziri Salum na nahodha wetu, John
Bocco,”alisema Jemedari.
Timu hizo zinakutana baada ya mwaka jana kushuhudia Azam wakiipindua Yanga na kuwanyang'anya ubingwa wakiwa hawajapoteza mchezo wowote.
Mechi hiyo itaanza saa 10 kamili jioni, na kiingilio hicho cha sh. 5,000
ni kwa viti vya rangi ya kijani na bluu vitakavyochukua jumla ya
watazamaji 36,000 katika uwanja huo wenye viti 57,558.
Viingilio vingine katika mechi hiyo ambayo itatumia tiketi za
elektroniki ni sh. 10,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 20,000 kwa
viti vya VIP C na B wakati viti vya VIP A kiingilio ni sh. 30,000.
No comments:
Post a Comment