STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, September 8, 2014

Yanga waendelea kumkomalia Emmanuel Okwi, sasa wamshtaki FIFA

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe (kulia) akimtambulisha mshambuliaji Emmanuel Okwi kurejea katika klabu hiyo jijini Dar es Salaam jana. Picha: Halima Kambi 
SIKU moja baada ya Shirikisho la soka Tanzania, TFF kumtangaza mchezaji Emmanuel Okwi kuwa huru na hivyo anaweza kusajiliwa na klabu ya Simba, uongozi wa Yanga umesema haujakubali.
Uongozi wa Yanga umesema utatinga katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kupinga maamuzi ya Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kumtangaza Emmanuel Okwi kuwa ni mchezaji huru na anaweza kuichezea Simba.
Baada ya kukutana jijini Dar es Salaam juzi kupitia masuala mbalimbali ukiwamo mgogoro wa kimkataba kati ya Yanga na Okwi, kamati hiyo ilisema imebaini kwamba mkataba kati ya pande hizo mbili ulikuwa umevunjika.
Hata hivyo, Yanga wamepinga maamuzi hayo na katika taarifa yao iliyotolewa na Kaimu Ofisa Habari, Baraka Kizuguto jana saa 7:08 mchana, klabu hiyo ya Jangwani imejipanga kuyakatia rufaa maamuzi hayo.
Kizuguto alisema Mwenyekiti wa Kamati  ya Sheria ya Yanga, Sam Mapande amesema hawajaridhishwa na maamuzi ya TFF huku akidai yanakinzana na shitaka zima la mchezaji huyo.
Katika maelezo yake yaliyochapishwa kwenye mtandao wa klabu ya Yanga jana mchana, Mapande alidai kuwa Kamati ya TFF imeamua sakata la Okwi kinyume cha malalamiko yao kwani hakukuwa na lalamiko la mchezaji huyo kuhusiana na malipo ya fedha zake za usajili.
Alisema wameshangaa kuona kamati hiyo ya TFF inaamua kusikiliza kesi ambayo haikuwa mbele yao na kutoa maamuzi yanayoshangaza.
“Kwanza, kesi yenyewe ilikuwa haijamalizika, walituambia tuwasilishe vielelezo kuhusiana na kitendo cha mchezaji huyo kufanya mazungumzo na klabu ya Misri, lakini cha kushangaza maamuzi yametolewa, hili limetushangaza sana,” alisema Mapande katika taarifa hiyo.
Alisema mazingira yalikuwa yameandaliwa kuibeba Simba na Okwi kwani hata malalamiko yao kwa Simba hayakusikilizwa. “Malalamiko yetu yalikuwa wazi kabisa, yapo kimaandishi, hatukuwahi kulalamikiwa, suala la fedha za usajili la Okwi limetoka wapi, kama lilikuwapo, mbona hatujajulishwa kimaandishi kama utaratibu ulivyo?” Alihoji Mapande.
Alisema kamati hiyo kumruhusu mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo Zacharia Hanspoppe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba kuwamo katika kikao hicho ni kinyume cha taratibu za Fifa kupitia kifungu namba 19 kinachoeleza mgongano wa kimaslahi.
Lakini, katika maelezo ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, yaliyotolewa juzi usiku kupitia kwa Kaimu Karibu Mkuu wa TFF, Boniface Wambura, Yanga ilikiuka kipengele namba 8 kuhusu malipo ya ada ya usajili katika mkataba huo wa pande mbili.
Wambura alieleza kuwa Yanga ikiwa mwajiri, haikutekeleza kipengele hicho cha kimkataba hadi kufikia Juni 27, mwaka huu ilipoandika barua TFF kuomba mkataba huo uvunjwe. Kwa maana hiyo Okwi ni mchezaji huru, hivyo yuko huru kujiunga na timu yoyote.
"Mkataba ni uhusiano kati ya mwajiri (Yanga) na mwajiriwa (Okwi), kamati imebaini kuwa uhusiano huo haupo, hivyo hakuna mazingira ya pande hizo mbili kuendelea kufanya kazi pamoja," inasomeka sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na Wambura juzi.
Wambura ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, alisema kuwa pamoja na Yanga kuwasilisha pingamizi la kuwapo mmoja wa wajumbe katika kikao kwa sababu za kimaslahi (conflict of interests) (Hanspoppe), walifahamishwa kuwa kilichokuwapo mbele ya kamati ni mgogoro wa kimkataba kati ya Yanga na Okwi, na si usajili.
Pia lilijitokeza suala la Okwi kutakiwa na klabu ya Wadi Degla ya Misri. Kamati imeiagiza Sekretarieti ya TFF kulifanyia uchunguzi suala hilo na kulitolea taarifa katika kikao kijacho.
Wambura alidai kuiwa mjumbe huyo (Hanspoppe) hakushiriki katika kuchangia hoja na kutoa maamuzi na kwamba uamuzi wa kamati ulifanyika baada ya majadiliano, hivyo hakukuwa na suala la kupiga kura.
Okwi raia wa Uganda, ambaye juzi alikuwapo wakati mkataba huo ukipitiwa na kamati pamoja na wawakilishi wa Yanga, alisaini mkataba wa miaka miwili na nusu kuitumikia timu hiyo ya Jangwani akitokea SC Villa ya Uganda.

No comments:

Post a Comment