STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, September 8, 2014

Huzuni! Watoto wa3 wateketezwa moto kinyama

http://zanzibardaima.files.wordpress.com/2013/01/moto.jpg?w=400&h=369&crop=1

WATOTO watatu wa familia moja wamekufa na wengine wanne kujeruhiwa baada ya nyumba yao kumwagiwa petroli kisha kuteketezwa kwa kuchomwa moto na watu wasiojulikana usiku wa kumkia jana.Tukio hilo lililotokea katika mtaa wa Elimu kata ya Kalangala wilayani Geita.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya wilaya, Dk. Adam Sijaona, amethibitisha kupokea miili ya watu hao, Mwanafunzi wa darasa la nne Shule ya Msingi Ukombozi Reginald Robert (9), Sophia Robert (6) (darasa la kwanza)na Remijius Robert (4).Dk. Sijaona aliwataja waliojeruhiwa sehemu za kifua, kichwani, mikono na miguu na makalio kuwa ni baba wa familia hiyo, Robert Remijius (45), mkewe, Angelina Gaspar (42) na mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Mwatulole, Scolastica Robert (15), aliyehamishiwa hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza kutokana na kuungua vibaya.

Alisema Salvance Reginald (47), ambaye ni dada wa Remijius amelazwa baada ya kupatwa na mshtuko kutokana na kushuhudia miili ya marehemu hao, akiwa miongoni mwa akinamama wengi waliokumbwa na mshtuko. Wakisimulia tukio hilo, baadhi ya wananchi wakiwamo viongozi wa serikali za mitaa na kata, walisema limetokea usiku wa manane baada ya walinzi wa jadi na mgambo wa doria kupiga filimbi za utambulisho, hivyo kwenda eneo la tukio na kusaidia uokoaji.

Ofisa Mtendaji wa kata ya Kalangalala, Hamad Hussein, alisema chanzo cha ‘wauaji’ kumwaga petroli milangoni na madirishani, huenda ni chuki za mgogoro wa ardhi.

Mwenyekiti wa mtaa wa Elimu na Ofisa Mtendaji wa mtaa huo, Simfukwe Ally, alisema kwa nyakati tofauti katika eneo la tukio kuwa taarifa za awali zinahusisha unyama huo na mgogoro wa ardhi uliokuwapo kwa muda mrefu bila kumtaja mtuhumiwa.

Akitoa pole eneo la tukio kwa niaba ya serikali ya wilaya Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Omary Mangochie, alieleza kusikitishwa na unyama huo na kuagiza ngazi ya mtaa hadi wilaya washirikiane kuhakikisha waliohusika wanakamatwa.

''Naagiza waliohusika wote wamekamatwe na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria, kamwe serikali na jamii haiwezi kuona unyama wa aina hiyo wala kuuvumilia nafahamu jamii itakuwa inawatambua maana wanatoka na wanaishi ndani ya jamii yenyewe,” alisema Mangochie.

Awali shuhuda wa tukio hilo, Lunyili Tekamisa, aliyeongoza walinzi wenzake wa doria kufika eneo la tukio, alisema walikuta moto mkali ukiwaka katika milango na madirisha yote.

''Tulichofanya ni kuvunja milango na madirisha...kwa tahadhari na pembeni kulikuwa na kindoo kidogo chenye ujazo wa lita tano kikiwa na mabaki ya mafuta ya petroli ambacho baadaye tulikikabidhi kwa polisi,” alisema Tekamisa.

Tukio hilo limeutikisa mji wa Geita na viunga vyake na pia kuzua hofu kubwa huku likileta majonzi makubwa na vilio kila kona likifananishwa na wale wanaotumia tindikali kutekeleza uhalifu wao.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment