STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, January 28, 2015

Bale asisitiza hana 'bifu' na Ronaldo, achekeea maisha Bernabeu

Ronaldo akiwa na Bale
MCHEZAJI ghali wa Real Madrid, Gareth Bale amesema hana mpango wa kuihama klabu hiyo akisisitiza kuwa ana uhusiano nzuri na nyota wa klabu hiyo, Cristiano Ronaldo na pia anapendwa na mashabiki.
Mshambuliaji huyo kutoka Wales, akihojiwa na kituo kimoja cha redio nchini Hispania, alisema uhusiano wake na Ronaldo ni nzuri na wenye nguvu na kudai hajawahi kuambiwa lolote na Ronaldo juu ya taarifa kwamba alimnyima pasi wakati wakiumana na Espanyol.
Bale alisema uhusiano wake na Ronaldo haujabadilika tofauti na inavyoelezwa, huku akisema anakumbuka kila kitu katika pambano hilo na kukiri kwamba hakumuona Ronaldo kiasi cha kumnyima pasi.
"Nakumbuka kila  kitu wakati nilipochukua mpira na nilikuwa katika kuhakikisha najaribu kufunga bao. Sikumuona, nafikiri ingeweza kuwa pasi ngumu kwake. Sijawahi kuzungumza na Ronaldo kuhusu habari hizo za  kumnyima pasi," alisema Bale.
Bale alisema kwa vyovyote anavyojua yanayotokea uwanjani huishia uwanjani ndiyo maana hawakuweza kujadili suala hilo, licha ya kwamba alijikuta akizomewa na mashabiki wa Santiago Bernabeu.
Nyota huyo mwenye miaka 25, alisema anajisikia furaha kucheza Bernabeu kutokana na sapoti ya mashabiki wa klabu hiyo na kudai hufanya kila linalowezekana ili kuonyesha uwezo wake na kuwapa furaha mashabiki hao.
Bale ameifungia Madrid jumla ya mabao 36 katika mechi 72 alizoichezea tangu ilipomsajili kwa kitita kilichoweka rekodi duniani akitokea Tottenham Hotspur, miongoni mwa mabao hayo 25 ameyafunga katika mechi 43 za La Liga.
Hata hivyo mchezaji huyo amekuwa akihusishwa na mipango ya kutaka kuihama klabu hiyo ili kujiunga na Mashetani Wekundu kwa kile kilichoelezwa kutokuwa na furaha klabuni hapo, japo mwenyewe amesisitiza anafurahia maisha Madrid pamoja na familia yake.

No comments:

Post a Comment