STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, January 28, 2015

Ndanda yaipiga mkwara Yanga pambano lao la Jumapili

Ndanda Fc
KLABU ya Ndanda imetamba kuwatoa nishai Yanga watakaoumana nao siku ya Jumapili kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ndanda ambayo tayari wameshatua jijini Dar es Salaam wakitokea Mwanza walipoisambaratisha Kagera Sugar kwa kuilaza mabao 2-1, imesema kuwa lengo lao ni kuvuna pointi tatu ili kujiweka pazuri katika msimamo wa ligi hiyo.
Katika Mkuu wa Ndanda, Edmund Njowoka amesema kuwa kikosi chao kinatambua ugumu wa pambano hilo dhidi ya Yanga, lakini wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi uwanja wa ugenini.
Kikosi cha Ndanda kinachocheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza, kipo nafasi ya 11 kikiwa na pointi 13 baada ya kucheza mechi 12 ikishinda michezo minne na kupoteza saba kitavaana na Yanga wanaokamata nafasi ya pili kwenye msimamo wakiwa na pointi 18 baada ya mechi 10.
Njowoka alisema kikosi chao kipo tayari kwa vita na amehakikishiwa na benchi lao la ufundi chini ya Kocha Meja Mstaafu Abdul Mingange kwamba vijana wao watapambana kufa na kupona kuhakikisha wanavuna pointi nyingine tatu.
"Tumekuja kwa ajili ya kuvuna pointi, kama tulivyofanya kwa Kagera ndivyo tunavyotaka kufanya kwa Yanga, licha ya kutambua ugumu wa pambano hilo la Jumapili," alisema Njowoka.
Yanga iliyolazimishwa sare mbili mfululizo na Azam na Ruvu Shooting, ilirekebisha makosa yake mwishoni mwa wiki kwa kuinyuka Polisi Moro kwa bao 1-0 na kuwajongelea watetezi wa ligi hiyo, Azam wanaoongoza wakiwa na pointi 21.
Azam kwa sasa ipo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kushiriki michuano maalum kujiandaa na pambano lake la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya El Marreikh. Michuano hiyo inashirikisha jumla ya timu nne zikiwamo TP Mazembe, Don Bosco na Zesco ya Zambia.
Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm alinukuliwa juzi kwamba kikosi chake kimejiandaa kupata ushindi dhidi ya Ndanda, akiwasisitiza vijana wake kuwa makini uwanjani ili kutopoteza nafasi za wazi kama walivyofanya katika mechi zao zilizopita.

No comments:

Post a Comment