STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, January 30, 2015

KUMEKUCHA SIMBA! WANACHAMA WATAKA MKUTANO

https://4.bp.blogspot.com/-XdhI9sOkyuk/VGNbtl-4WrI/AAAAAAABZ48/icOxk0YsNh0/s1600/hans+poppe+na+aveva.jpg
Rais Evance Aveva akiwa na Mwenyekiti wa kamati ya usajili Zakaria Hanspop
KUFUATIA timu yao kupata kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa wageni Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi, wanachama wa klabu ya soka ya Simba wanautaka uongozi wa klabu yao kuitisha mkutano mkuu wa dharura ili kujadili mwenendo mbaya wa kikosi chao kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Simba juzi ilipoteza mechi yake ya pili msimu huu na kuangukia katika nafasi ya 11 kwenye msimamo ligi hiyo ya timu 14 ikiwa imetoka sare mara saba na kushinda mechi mbili tu.
Akizungumza kwa niaba ya wanachama wenzake, Mwenyekiti wa Tawi la Mpira Pesa lililoko Magomeni jijini Dar es Salaam, Ustadh Masoud, alisema kwamba wanauomba uongozi kuitisha mapema mkutano ili waweze kupata suluhisho kabla ya 'jahazi' halijazidi kuzama.
Masoud alisema kwamba kupitia mkutano wa wanachama, wanaamini watafahamu kinachosababisha timu yao kufanya vibaya kwenye mechi zake za ligi na kupoteza matumaini ya kutwaa ubingwa.
Alisema pia wamebaini ndani ya uongozi hakuna umoja na baadhi yao wanaingilia majukumu ya watu wengine.
"Mwenendo wa timu hauturidhishi kabisa, ndiyo maana tumeomba viongozi waitishe mkutano wa dharura, tayari tumeshapeleka barua kuwaomba mkutano haraka," alisema mwenyekiti huyo wa kundi maarufu na lenye nguvu ndani ya Simba.
Aliongeza kwamba pia hawana imani na baadhi ya viongozi waliopo kwenye benchi la ufundi na kuutaka uongozi ulifanyie kazi.
Mashabiki wa klabu hiyo na wanachama walisikika wakisema baada ya mechi yao ya juzi kuwa Simba si shule ya soka, ni klabu kubwa inayopaswa kupigania mataji hivyo viongozi wanapaswa kusajili wachezaji walioiva tayari na kwamba vijana waingizwe wachache taratibu kupewa uzoefu tofauti na ilivyo sasa.
Simba juzi iliwatumia yosso saba Manyika Peter, Hassan Isihaka, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Jonas Mkude, Twaha Ibrahim, Ibrahim Hajib na Ramadhani Singano.
Rais wa Simba, Evans Aveva, alisema kuwa amepata taarifa za wanachama hao kuomba mkutano na kueleza kwamba mkutano utafanyika kwa kufuata programu iliyoandaliwa na si vinginevyo.
Aveva alisema kwamba Kamati ya Utendaji itakutana kupanga siku ya mkutano si kwa kufuata maelekezo ya wanachama.
"Mkutano utafanyika kwa kufuata programu, tutakutana wakati wowote ili kupitisha tarehe ya mkutano, hatuwezi kufanya kitu kilichoko nje ya utaratibu na kalenda ya mwaka," alisema.
Rais huyo alisema pia yeye binafsi hafurahishwi na matokeo hayo na kuwataka wanachama na mashabiki kuwa watulivu kwenye kipindi hiki.
"Tunawapa wachezaji wetu kila kinachotakiwa, ila matokeo yanayopatikana si mazuri, inatuuma na kutuchanganya sisi pia," alisema Aveva.
Baada ya kichapo cha juzi, Simba inaendelea na mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mechi yake dhidi ya JKT Ruvu itakayofanyika kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

No comments:

Post a Comment