STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, June 3, 2016

Mkwasa aahidi raha Taifa, tunasubiri nini twendeni uwanjani

Kocha wa Stars, Boniface Mkwasa

TWENDENI Taifa kesho Jumamosi, kwani Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa 'Master' ameahidi kuifanyizia Mafarao wa Misri katika pambano lao la kuwania Afcon 2017.
Stars kesho inashuka dimbani kucheza na Misri ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha mabao 3-0 iliyopata kwenye mchezo wa awali uliochezwa mji wa Alexandria, katika ufunguzi wa mechi za Kundi G.
Stars  inahitaji ushindi ili kufufua matumaini ya kufuzu AFCON ya mwakani wakati Misri wao sare itawafanya wafikishe pointi nane ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine kwenye kundi lao.
Endapo Tanzania itashinda mchezo huo itafikisha pointi nne kwani hadi sasa ina pointi moja baada ya sare ya 0-0 na Nigeria nyumbani huku ikibakisha mchezo wa marudiano na Nigeria ugenini baadaye Septemba mwaka huu..
Kundi hili baada ya kujitoa kwa Chad limebaki na timu tatu ambazo ni Misri wenye pointi saba, Nigeria pointi nne na Tanzania yenye inashika mkia ikiwa na  pointi moja lakini Misri na Nigeria zimebakiza mchezo mmoja mmoja, wakati Tanzania ina faida ya mechi mbilim huu wa leo na mwingine ni dhidi ya Nigeria utakaochezwa Septemba.
Akizungumza na Wanahabari Kocha Mkwasa alisema mchezo wa keshoni  mgumu kwani ni sawa na fainali hivyo wanahitaji kushinda ili kujiweka pazuri kwani Misri wanakuja wakihitaji sare.
“Wachezaji wako vizuri, wako kwenye morali nzuri na tumefanya mazoezi na wachezaji wote 26 na mimi nimefanya marekebisho kwa makosa yaliyojitokeza kwenye mchezo dhidi ya Kenya na kinachosubiriwa ni dakika 90 tu”, alisema Mkwasa.
Pia Mkwasa alisema anatambua Misri ni timu nzuri kwani waliifunga Tanzania mabao 3-0 kwao na anajua wanakuja kucheza mfumo wa kujilinda kuliko kushambulia kama ilivyo desturi kwa timu za kiarabu lakini wao wamejiandaa kushambulia.
“Tuna deni kubwa kwa watanzania hivyo tunajua tunatakiwa kupata matokeo mazuri ili kuwapa faraja na kufufua matumaini ya kwenda AFCON hivyo tutashambulia sana”, alisema Mkwasa
Mkwasa aliwashukia watu wanaojiita wachambuzi wa soka akisema wamekuwa wakiwavunja moyo wachezaji na kuwataka waangalie namna wanavyofanya uchambuzi kwani wanawakatisha tamaa wachezaji na kuwaasa uchambuzi mzuri ni ule ambao unafanywa baada ya mchezo.

No comments:

Post a Comment