STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, June 3, 2016

Samatta akimaliza kazi Taifa, kupewa kiwanja chake Mkuranga

Na Rahma Junior
MBWANA Samatta kesho Jumamosi ataiongoza Taifa Stars kuvaana na Misri, kwenye pambano la kuwania kwenda Gabon katika fainali za Afcon 2017, lakini Jumapili atakuwa katika sherehe moja kamambe.
Nahodha huyo wa Stars, atakuwa anakabidhiwa  kiwanja cha ekari tano kilichopo kijiji cha wasanii Mwanzega, Mkuranga.
Mwenyekiti wa Mtandao wa Wasanii Tanzania (SHIWATA), Cassim Taalib 'Teacher' alisema  jijini Dar es Salaam kuwa maandalizi yamekamilika na Mbwana amewasili nchini kwa mechi ya timu ya TAifa ya Tanzania (Taifa Stars) na Misri utakaochezwa Jumamosi.
Alisema sherehe hizo zitaambatana na ugawaji wa nyumba na misingi ya nyumba kwa wasanii 35 ambao wanafikisha ya wanachama 180 waliokwisha kabidhiwa nyumba zao.
Alisema SHIWATA imemzawadia Mbwana ekari tano ili ajenge kituo cha michezo kwa lengo la kuibua vipaji vya vijana wa Tanzania watakaolitangaza taifa hili kwenye medani ya michezo kimataifa.
Taalib alisema mtandao  huo unaomiliki eneo la ekari 300 za kujenga makazi unawakaribisha wadau wa michezo kuwekeza kwa kujenga kumbi za burudani,shule za michezo, studio za kurekodia, viwanda vya kutengeneza vifaa vya michezo na hosteli za kufikia wachezaji.
Alisema sherehe za kugawa nyumba zinafanyika kwa mara ya tano kutoka ujenzi huo uanze katika kijiji hicho ambapo wanachama 185 wamekabidhiwa nyumba zao walizojengwewa kwa njia ya kuchangishana.
Alisema mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa, Nape Mnauye ambaye atakuwa waziri wa pili kutembelea kijiji hicho baada ya Naibu wake, Anna Wambura kutembelea mapema mwaka huu.
Viongozi wengine waliowahi kutembelea kijiji hicho ni kiongozi wa mbio za mwenge mwaka 2014, Wakuu wa wilaya ya Mkuranga wastaafu, Mercy Silla, Clemency na Mkuu wa wilaya hiyo wa sasa, Abdallah Kihato.
Wageni wengine walioalikwa kwenye sherehe hizo ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi viongozi wa Serikali wa Wilaya ya Mkuranga na wasanii maarufu nchini.

No comments:

Post a Comment