STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, January 8, 2017

Yanga yakumbana na dhahama mbele ya Azam

Sure Boy aliyekuwa mpishi katika maangamizi ya Yanga jana mjini Zanzibar
Na Rahma White, Z'Bar
BADO hawaamini. Yanga na kikosi chake bora. Ikiwa na Kocha Mzambia George Lwandamina usiku wa jana wamepigwa mabao 4-0 na Azam katika mechi ya kufungia dimba ya Kundi B kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2017.
Sio makocha tu, bali hata mashabiki wa klabu hiyo mpaka sasa hawaamini kile kilichowakuta kwa sababu waliamini Azam walikuwa wepesi kwao.
Hata hivyo kwa kuwa soka ni mchezo wenye matokeo ya kikatili, Yanga imelala bao 4-0 na kuweka rekodi ya kupokea kipigo kikubwa tangu mwaka 2012 walipotunguliwa na watani zao wa Simba katika mechi ya Ligi Kuu 2011-2012.
Katika pambano hilo Yanga ilikandikwa mabao 5-0, lakini Azam jana usiku ilisamehe moja na kufunga mabao hayo ikiwa ni mengi kuwahi kuifunga timu kongwe nchini Simba na Yanga na kumaliza kama kinara wa kundi lao.
Mabao ya John Bocco 'Adebayor' lililokuwa la 14 kwake kuitungua Yanga, na mengine ya Waghana Yahya Mohammed na Enoch Agyei-Atta na lile la Joseph Mahundi yalityosha kuinyoosha Yanga iliyocheza ovyo eneo lake la ulinzi.
Mabadiliko ya kutolewa kwa Haji Mwinyi na kuingizwa Geofrey Mwashiuya yaliigharimu Yanga ambayo sasa inasubiri kujua itaumana na Simba au klabu gani katika mechi ya nusu fainali Jumanne ijayo.
Simba itakabiliana na Jang'ombe Boys katika mechi ya kukamilisha ratiba, huku URA na Taifa Jang'ombe zikipapetuana kusaka tiketi za kucheza nusu fainali. Mechi hizo zinapigwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Amaan.
Baadhi ya wachezaji wa Yanga wamesema hawajui mpaka sasa kilichoikuta timu yao kwani walijiandaa kuvaana na Azam, ingawa wamekiri kucheza mfululizo bila mapumziko ni tatizo la kupoteza umakini usiku wa jana.

No comments:

Post a Comment