STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, March 16, 2013

Yanga bila Yondani kuivaa Ruvu Shooting leo

Wachezaji wa Yanga wataendelea kushangilia mabao leo kwa Ruvu kama hivi?

VINARA wa Ligi Kuu nchini Yanga chini ya Kocha wake, Ernst Brandts wanatarajiwa kushuka dimbani jioni ya leo kuvaana na Ruvu Shooting, bila beki wake mahiri wa kati, Kelvin Yondani.
 Hata hivyo Brandts amesema licha ya kumkosa beki huyo, bado anaamini Yanga itaibuka na ushindi katika mechi hiyo itakayochezwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Yanga wanaongoza msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 45 baada ya mechi 19 wakifuatwa na mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, Azam (37) na mabingwa watetezi wa Simba walio katika nafasi ya tatu (34).
Akizungumza jana baada ya kumalizika kwa mazoezi ya timu yake kwenye uwanja wa Bora wa Kijitonyama, jijini Dar es Salaam jana, Brandts alisema atawatumia mabeki waliopo kuziba pengo la beki huyo tegemeo kwa Yanga na timu ya taifa, 'Taifa Stars'.
Hata hivyo, ni wazi kwamba safu ya ulinzi ya Yanga haipo vizuri kwa sasa kutokana na kukosekana kwa mabeki watatu.
Ladislaus Mbogo ni mgonjwa baada ya kufanyiwa upasuaji wa uvimbe shavuni, Yondani anasumbuliwa na tatizo la uvimbe wa kidole gumba cha mguu na Stephano Mwasika ana maumivu ya misuli ya mguu.
“Naamini tutacheza vizuri licha ya kuwakosa mabeki wetu hao kwa sababu wachezaji wengine wako safi kiafya, kiakili na wana morali ya hali ya juu katika kuhakikisha timu inapata ushindi katika mechi ya Jumamosi (leo),” alisema Brandts.
Ruvu Shooting inayonolewa na Boniface Mkwasa inakamata nafasi ya saba katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kucheza mechi 18, na imekuwa na historia ya kuikamia Yanga katika mechi baina yao.
Katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, Yanga waliokuwa nyuma kwa magoli mawili hadi mapumziko, walizinduka na kuibuka na ushindi wa 3-2 katika kipindi cha pili.
Tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi kuu Januari 26, Yanga ambao ni mabingwa wa soka Afrika Mashariki na Kati, wameshacheza mechi sita wakishinda tano na kutoka sare moja.
Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa Sh. 5,000, Sh. 8,000, Sh. 15,000 na Sh. 20,000, kwa mujibu wa taarifa ya shirikisho la soka (TFF).

Azam ni kufa na kupona kesho Liberia

Kikosi cha Azam

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho, Azam kesho ni kufa ama kupona wakati watakaposhuka dimbani ugenini nchini Liberia kuwakabilia wenyeji wao Barrack YC II katika merchi ya kwanza ya mzunguko wa kwanza wa michuano hiyo ya Afrika.

Azam itavaana na Barrack majira ya saa 10 jioni mjini Monravia, ikiwa ina kumbukumbu ya ushindi mnono wa ugenini iliyopata dhidi ya Al Nasir JUba ya Sudan Kusini wiki mbili zilizopita.
Klabu hiyo ambayo ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania waliobaki kwenye michuano ya kimataifa baada ya Simba kutolewa katika Ligi ya Klabu Bingwa Afrika na Recreativo de Libolo ya Angola, wanahitaji ushindio wa aina yoyote kesho ili kujiweka vyema kwa mechi ya marudiano nyumbani wiki mbili zijazo.
Msemaji wa Azam FC, Jafar Idd alisema jana kuwa kikosi chao kinaendelea vyema na mazoezi kwa ajili ya mechi hiyo ya raundi ya kwanza.
Alisema kuwa kikosi chao kinachonolewa na kocha Muingereza Stewart Hall kina morali ya hali ya juu na wanaamini watafanya vizurui katika mechi hiyo na kuendelea kuiwakilisha vyema Tanzania katika michuano ya kimataifa.

Kikosi kitakachoshuka dimbani kesho kinatarajiwa kutajwa baada ya mazoezi ya leo jioni lakini ni wazi golini atasimama Mwadini Ally kama kawaida.

Aden Rage kupinduliwa Simba akiwa ughaibuni?

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage

SIKU za mwenyekiti Ismail Aden Rage kuongoza Simba zipo hatarini kumalizika kesho baada ya wanachama karibu 700 wa klabu hiyo kuitisha mkutano mkuu ambao utajadili, pamoja na jingine, kutokuwa na imani na uongozi uliopo madarakani.
Mkutano huo unakuja siku chache baada ya makamu mwenyekiti Geofrey Nyange 'Kaburu' na mjumbe wa kamati ya utendaji Zakaria Hans Pope kujiuzulu wiki iliyopita.
Rage yupo kwenye matibabu nchini India kwa gharama za Bunge akiwakilisha jimbo la Tabora Mjini (CCM).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana, mratibu wa mkutano huo, Mohamed Wandi alisema utafanyika Mnazimmoja "kujadili namna ya kuinusuru" klabu hiyo inayosumbuliwa na migogoro.
Alisema wanachama 698 wameitisha mkutano huo kwa sababu ni haki yao kikatiba na kwamba wamezitaarifa mamlaka mbalimbali zikiwamo polisi, Shirikisho la Soka (TFF) na uongozi wa Simba kuhusu kufanyika kwa mkutano huo.
“Tulishamwandikia barua (siku nyingi) mwenyekiti tukimwomba aitishe mkutano mkuu wa dharura lakini hataki," alisema Wandi.
"Tumeamua kuuitisha wenyewe kwa sababu ibara ya 22 ya katiba yetu inatamka wazi kwamba wanachama wasiopungua 500 wana haki ya kuandaa mkutano mkuu kama mwenyekiti hayuko tayari kuuitisha ndani ya siku 30.”
Alisema mkutano huo utakuwa na agenda mbili ambazo ni mwenendo wa timu katika michuano inayoshiriki na kutokuwa na imani na uongozi wa Rage.
Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema jana jijini Dar es Salaam jana kuwa uongozi umepata taarifa za kuitishwa kwa mkutano huo lakini umejipanga kuhakikisha kuwa haufanyiki kwa sababu ni batili.
“Katiba yetu iko wazi, mwenyekiti pekee ndiye mwenye mamlaka ya kuitisha mkutano mkuu na mkutano mkuu wa dharura," alisema na kueleza zaidi:
"Mwenyekiti wetu hajakataa kuitisha mkutano. Tangu aiingie madarakani amekuwa akiitisha mkutano mkuu wa kila mwaka na tayari alishasema ataitisha mkutano mkuuu wa dharura.
“Mkutano wa Jumapili (kesho) ulioitishwa na wanachama hautafanyika kwa sababu ni batili. Uongozi tayari umesharipoti kwenye kituo cha Polisi Msimbazi kuuzuia."


CHANZO:NIPASHE