STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, April 9, 2013

MASHETANI WEKUNDU WAFA NYUMBANI, KUN AGUERO AWAZIMA

Robin Van Persie akijaribu kukukuruka langoni mwa Manchester City jana usiku 

Sergio Kun Aguero akishangilia bao lililoizamisha Manchester United kwao jana usiku
VINARA wa Ligi Kuu ya England, Manchester United 'Red Devils' usiku wa kuamkia leo walikiona cha moto baada ya kunyukwa mabao 2-1 na wapinzani wao wa jadi, Manchester City kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Old Trafford.
Ushindi huo ambao ulishuhudia mabingwa watetezi wa ligi hiyo wakifunga mabao yote katika mechi hiyo, imeifanya Man City kupungua pengo la pointi  kati yake ya wapinzani hao wao kutoka 15 hadi 12.
Bao lililowazima Mashetani Wekundu ambao wanajiandaa kusherehekea ubingwa msimu huu, lilifungwa na Sergio Kun Aguero zikiwa zimesaliwa dakika 11 kabla ya pambano hilo kumalizika huku matokeo yakiwa bao 1-1.
City walitangulia kupata bao mara baada ya timu kutoka mapumziko kupitia kwa James Milner katika dakika ya 51 kabla ya Vincent Kompany kuizawadia Man Utd bao dakika nane baadaye.

Superspot yapangua ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara



RATIBA ya mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara imefanyiwa marekebisho mbalimbali  ambapo baadhi ya mechi hizo zimesogezwa mbele zikiwamo zinazozihusu klabu za Simba na Yanga.
Mechi baina ya Yanga na JKT Oljoro iliyokuwa ichezwe kesho Jumatano itapigwa Jumamosi Aprili 13 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wakati mchezo unaosubiriwa kwa hamu baina ya Azam na Simba uliokuwa ufanyike Jumamosi ya Aprili 13 sasa utakuwa Jumapili (Aprili 14) kwenye uwanja huo huo.
Mabadiliko hayo yanalenga kutoa nafasi kwa mechi hizo za Ligi Kuu ya Bara kuonekana moja kwa moja katika kituo cha televisheni cha kulipia cha Super Sport chenye lengo cha kuja kuidhamini ligi hiyo.
Akizungumza jana jijini, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alizitaja mechi nyingine zilizofanyiwa marekebisho katika ligi hiyo kuwa ni Azam dhidi ya African Lyon sasa watachuana Alhamisi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi badala ya kesho.
Wambura alisema mchezo mwingine uliosogezwa mbele ni kati ya Mgambo JKT dhidi ya Yanga ambao sasa utafanyika Aprili 17 mwaka huu badala ya Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Aliitaja mechi nyingine itakayorushwa hewani kuwa ni ya Coastal Union dhidi ya JKT Ruvu itakayochezwa Aprili 16 badala ya Aprili 10 na kuongeza kuwa mchezo mwingine uliofanyiwa marekebisho ni kati ya Mtibwa Sugar dhidi ya JKT Oljoro ambao sasa utafanyika Aprili 17 badala ya Aprili 13.
Aliongeza kuwa mechi nyingine zitabaki kama zilivyopangwa awali ikiwamo ya Yanga dhidi ya Simba itakayofanyika siku ya funga dimba ya ligi hiyo kwa timu zote 14 zinazoshiriki ligi hiyo kushuka dimbani.
Hata hivyo, afisa habari wa Yanga, Baraka Kizuguto alisema jioni jana kuwa wamepeleka barua TFF ya kupinga mabadiliko hayo kwa kuwa yameganyika bila ya kuwashirikisha.
Yanga wanaongoza ligi hiyo kwa pointi 49 wakifuatiwa na Azam wenye pointi  43, Kagera Sugar (pointi  37) na mabingwa watetezi Simba walio katika nafasi ya nne kwa kuwa na pointi 35.

NSA JOB MATATANI, MWENYEWE AAHIDI KUFICHUA SIRI

 
Nsa Job (kulia) alipokuwa Yanga

MSHAMBULIAJI wa Coastal Union ya jijini Tanga inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Nsa Job, ambaye wiki iliyopita alikiri hadharani kuwahi kupokea rushwa ya Sh. milioni 2 ili asiifunge moja ya timu kongwe nchini, amesema kwamba yupo tayari kutoa ushirikiano kama alivyoombwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili hatua zaidi zichukuliwe katika kukomesha rushwa kwenye mchezo huo nchini.
Hata hivyo, Job ambaye kwa sasa yuko nje ya timu yake baada ya kufanyiwa upasuaji katika goti lake, hakuwa tayari kueleza rushwa hiyo aliipokea wakati anaichezea timu ipi au mashindano gani.
Katika mechi hiyo, Job alifunga goli na timu yake hiyo aliyokuwa anaichezea ilishinda bao 1-0 na kupata pointi tatu muhimu.
Nyota huyo ameshawahi kuchezea timu mbalimbali za Ligi Kuu zikiwamo Simba, Yanga, Moro United, Villa Squad na sasa Coastal Union.
Akizungumza jana, Job alisema kuwa tayari ameshapokea barua kutoka TFF inayomtaka atoe maelezo kuhusiana na tuhuma hizo na yeye ameahidi atatoa ushirikiano bila kikwazo.
Job alisema kuwa ameamua kufanya hivyo ili kuonyesha ni jinsi gani soka la Tanzania linavyoendeshwa licha ya kuwapo kwa mipango mbalimbali ya maendeleo ya mchezo huo.
"Niko tayari kutoa ushirikiano wanaouhitaji na barua ya TFF niliipata tangu Ijumaa," alisema kwa kifupi nyota huyo ambaye alikataa kueleza ni wakati gani alipokea rushwa hiyo.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, jana alisema kuwa wanamtaka Job atoe maelezo kuhusiana na suala hilo pamoja na kituo cha redio cha Clouds ambacho kilirusha hewani mahijiano hayo Aprili 3 mwaka huu kupitia kipindi chake cha 'Amplifier' ili kupata nakala ya ushahidi.
Osiah alisema kuwa endapo Job hatatoa ushirikiano hatua kali dhidi yake zitachukuliwa na lengo ni kutaka kupambana kikamilifu na vitendo vya rushwa kwenye soka.
Alisema baada ya kupata vielelezo katika pande zote ambapo pia wanaomba wadau watoe ushirikiano ili kukomesha rushwa watalipeleka katika Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya hatua za kinidhamu.
Osiah alisema kwamba licha ya nyota huyo kutoweka wazi ni kiongozi yupi alimpa fedha hizo, timu gani alikuwa akiichezea dhidi ya timu ipi, TFF imefikia hatua hiyo ili kutaka nidhamu iwepo na makosa yaliyowahi kufanyika huko nyuma yasirudiwe.
Nsa alidai kuwa baada ya kufunga goli katika mchezo huo kiongozi huyo ambaye hakuwa tayari kumtaja hadharani kwenye mahojiano hayo alikuwa akimfuata na kumtaka arudishe fedha alizopokea.