STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, August 9, 2013

Nizar, Twite, Dumayo, Msuva warejea kikosini Yanga, Minziro anachekaa

Kocha Msaidizi wa Yanga, Fred Felix Minziro
Mbuyu Twite (kati) na Msuva wakimpongeza Cannavaro katika moja ya mechi ya timu yao ya Yanga.
NYOTA wanne wa Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Mbuyu Twite, Frank Dumayo, Simon Msuva na Nizar Khalfan waliokuwa majeruhi wameanza kujifua na wenzao na kulipa matumaini benchi ya ufundi la klabu hiyo katika kuelekea kwenye pambano lao la Ngao ya Hisani dhidi ya Azam.
Yanga na Azam zinatarajiwa kuvaana  Agosti 17 katika pambano la Ngao ya Hisani kufungulia pazia la msimu mpya wa ligi nchini, litakalochezwa kwenye uwanja wa Taifa kabla ya kuanza kwa kipute cha ligi hiyo wiki moja baadaye.
Akizungumza na MICHARAZO mapema asubuhi hii, Kocha Msaidizi wa Yanga, Fred Minziro alisema kurejea dimbani kwa nyota hao kumewapa faraja na kuamini kuwa watavaana na wapinzani wao wakiwa wamekamilika.
Minziro alisema benchi lao la ufundi linaamini wachezaji hao watakuwa fiti kabla ya pambano hilo na mchezo wao wa kufungua dimba ya Ligi Kuu dhidi ya Ashanti United.
"Kurejea kwa wachewzaji wetu waliokuwa majeruhi kumetufa faraja kubwa kwa kuamini kuwa watakuwa fiti kabla ya mechi yetu ya Ngao ya Hisani na ile ya Ligi dhidi ya Ashanti United," alisema Minziro.
Aidha kocha huyo alisema anafurahishwa na namna wachezaji wao wanavyozidi kushika maelekezo yao kiasi cha kufanya vyema kwenye michezo yao ya kirafiki ya kujipima nguvu wakiamini wataendelea hivyo hata ligi itapoanza Agosti 24.
Minziro alisema pamoja na kikosi chaao kuifanya vyema bado wanazidi kuendelea kuwanoa kuhakikisha wanakuwa wakali zaidi ili kurejea mafanikio ya msimu uliopita wa kunyakua tena taji la Ligi Kuu kwa mara ya 25.
Alisema katika kujiweka fiti zaidi kesho wanatarajiwa kushuka dimbani tena kuvaana na Bandari Mombasa, mchezo aliodai huenda ukawa wa mwisho kwao kabla ya kujichimbia kambini kusibiri Azam na mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kikisi hicho juzi liliifumua timu isiyojulikana ya 3 Pillars inayodaiwa kutoka Lagos, Nigeria kwa bao 1-0 siku chache baada ya kuilaza Mtibwa Sugar kwa mabao 3-1.

Twanga Pepeta kumtambulisha Ige Moyaba, warembo wa Miss Ilala kesho


BENDI ya muziki wa dansi ya African Stars 'Twanga Pepeta' kesho itawatambulisha wanamuziki wake wapya akiwemo muimbaji wao wa zamani Ige Moyaba na warembo watakaoshiriki Miss Ilala 2013.
Utambulisho huo ambao  ni sehemu ya shamrashamra za sikukuu ya Idd el Fitri utafanyika katika ukumbi  wa Mango Garden, Kinondoni.
Mratibu wa onyesho hilo, Joseph Kapinga alisema maandalizi yote ya onyesho hilo yamekamilika.
"Ige Moyaba aliyekuwa Ufaransa amewasili nchini tangu juzi usiku na alishajiunga na wanamuziki wenzake," Kapinga alisema.
Kapinga alisema warembo watakaoshiriki shindano la kumtafuta Miss Ilala pia watatambulishwa kwenye onyesho hilo linaloandaliwa na Bob Entertainment na Keen Arts chini ya udhamini wa Konyagi, Freddito Entertainment, Saluti5 na Twitter Pub.
Pia bendi hiyo itaambulisha wanenguaji wake wapya wa kike kwenye onyesho hilo maalum ya kusherekea Idd Pili.
 "Tumeamua kuleta wanenguaji wapya kabisa, wenye damu changa ili kuleta mapinduzi kwenye muziki wa dansi. Madansa wetu ni mabinti warembo, pia tuna  wanenguaji watanashati," alisema Mkurugenzi wa bendi hiyo Asha Baraka  na kuongeza kuwa;
"Tumebadilisha na kuongeza safu mpya ya unenguaji ili kwenda na wakati pamoja na soko la muziki linavyotaka."
Kwa upande wa Ige Moyaba aliyetamba kwenye albamu ya 'Mtu Pesa' ya mwaka wa 2004, Asha alisema ameandaa vitu vipya kuwapa mashabiki wa bendi hiyo inayotamba kwa staili ya 'Kisigino'.
"Kwa kweli hi siyo onyesho la kukosa kwani itakuwa ni zawadi yetu ya Idd kwa mashabiki wetu," mkurugenzi huyo alisema.
Mwezi uliyopita Twanga Pepeta walizindua albamu yao ya 10 iitwayo 'Nyumbani ni Nyumbani', ambapo nyimbo zake zitapigwa katika onyesho hilo la leo.
Nyimbo nyingine zitakazopigwa katika onyesho hilo ni zila za albamu za nyuma kama 'Jirani', 'Fainali Uzeeni', 'Chuki Binafsi', 'Ukubwa Jiwe', 'Mtu Pesa', 'Safari', 'Password', 'Mtaa wa Kwanza', 'Mwana Dar es Salaam' na 'Dunia Daraja'.