STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, October 8, 2013

Cannavaro atamba Yanga kwenda kupata ushindi Kaitaba

Cannavaro (kushoto) akichuana na mchezaji wa Kagera Sugar ligi ya marudiano msimu uliopita
NAHODHA wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara ,Yanga Nadir  Haroub 'Cannavaro', amesema licha ya kutambua ugumu wa pambano lao lijalo dhidi ya Kagera Sugar, bado anaamini timu yake itaibuka na ushindi ugenini.
Yanga itasafiri hadi mjini Bukoba, mkoani Kagera kuvaana na Kagera Sugar siku ya Jumamosi kwenye uwanja wa Kaitaba katika moja ya mfululizo wa mechi za Ligi Kuu mwishoni mwa wiki hii.
Mabingwa hao watetezi wanaokamata nafasi ya pili kwa sasa katika msimamo huo, walichezea kichapo cha bao 1-0 katika mechi kama hiyo kwa msimu uliopita iliyochezwa Oktoba 8 na kuwa pambano pekee kupoteza kipindi chote hadi hivi karibuni walipolazwa na Azam katika ligi ya msimu huu.
Cannavaro, beki wa kati wa kutumianiwa wa Yanga anafahamu usumbufu wa wapinzani wao wanapokuwa uwanja wao wa Kaitaba, lakini alisema kwa namna kikosi chao kilichojipanga anaamini wanaenda Kagera kuvuna pointi tatu.
"Tunajua litakuwa pambano gumu na lenye upinzani mkali, lakini Yanga tutapigana kiume ili kushinda kuendeleza wimbi la ushindi tulilolianza," alisema.
Cannavaro anayeichezea pia timu ya taifa, alisema wachezaji wote wa Yanga wana ari kubwa ya kuisaidia timu yao kuendeleza ushindi baada ya awali kuchechemea kwa sare na kupoteza mchezo wao na Azam.
Yanga imepata ushindi mara mbili mfululizo dhidi ya timu za Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar na kuwafanya wawasogelee watani zao, Simba wanaoongoza wakiwa na pointi 15, tatu pungufu na ilizonazo Yanga na JKT Ruvu.
Kivumbi cha ligi hiyo kinatarajiwa kuendelea tena kesho kwa michezo minne katika viwanja vinne tofauti ambapo Rhino Rangers itakuwa nyumbani mjini Tabora kuikaribisha Mbeya City kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, huku Oljoro JKT itaialika Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid , Arusha.
Pambano jingine litazikutanisha Azam na Mgambo JKT zitakazoumana kwenye uwanja wa Chamazi na Mtibwa Sugar itakuwa nyumbani Manungu kuikaribisha JKT Ruvu.

Mtuhumiwa muhimu mauaji wa Bilionea wa Madini anaswa akitoroka


JESHI la  Polisi nchini limefanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa muhimu wa mauaji ya mfanyabiashara bilionea wa Arusha Erasto Msuya wakati akijaribu kutoroka kwenda Burundi.
Habari za uhakika zilizopatikana jana, zilisema mtuhumiwa huyo (jina tunalo), alikamatwa juzi asubuhi mkoani Kigoma akiwa katika harakati za kutoroka kuelekea nchi jirani ya Burundi.
Mtuhumiwa huyo ndiye anadaiwa kumshawishi marehemu kwenda kukutana na wauaji wake eneo la Mijohoroni wilayani Hai Agosti 7, mwaka huu na alikwenda pamoja na marehemu hadi eneo la tukio.
Habari zinadai mara baada ya marehemu kuuawa kwa kumiminiwa risasi zaidi ya 20, mtuhumiwa huyo alitoroka kutoka eneo la tukio akitumia moja kati ya pikipiki mbili zilizotumika katika mauaji hayo. 

Tangu kutokea kwa mauaji hayo, polisi ambao wameonyesha weledi wa hali ya juu katika upelelezi wa mauaji hayo, walikuwa wakimfuatilia mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa akijificha katika mikoa tofauti.
Habari nyingine zinadai kuwa watuhumiwa waliokodishwa kumuua mfanyabiashara huyo waliahidiwa kulipwa kitita cha Sh4 milioni kila mmoja na kila mmoja akalipwa malipo ya awali ya Sh1 milioni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo aliyesema ni 'muhimu' na kwamba mipango ya kumrejesha Moshi inaendelea kufanyika.
Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kunafanya idadi ya watuhumiwa ambao wamekwishakamatwa hadi sasa kufikia wanane wakiwamo wafanyabiashara wawili wenye ukwasi ambao tayari wamefikishwa mahakamani.