STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, November 28, 2013

Uhai Cup 2013 yafikia patamu, nusu fainali kuanza leo Chamazi

Moja ya hekaheka za michuano ya Uhai Cup 2013
MICHUANO ya vijana kwa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara U20 ya Uhai Cup imeingia hatua tamu ambapo timu nne za kucheza Nusu Fainali zimefahamika na kipute hicho kinaanza leo kwa pambano la mabingwa watetezi, Azam dhidi ya Coastal Union.
Nusu fainali nyingine itachezwa kesho kwa mchezo kati ya Yanga itakayoumana na Mtibwa Sugar ambayo jana iliing'oa Simba kwa mabao 3-2, ikitoka nyuma kwa mabao 2-0.
Mechi zote hizo zinachezwa uwanja wa Chamazi, ambapo pambano la leo kati ya Azam na Coastal linarejesha kumbukumbu ya mechi mbili kwa timu hizo zilipokutana katika mechi ya Fainali za mwaka jana na Coastal kukubali kipigo kabla ya kulipa kisasi jkatika mechi ya ufunguzi wa michuano ya msimu huu walipoibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Timu hizo mbili zilifuzu hatua hiyo ya nusu fainali kwa kuzinyoa timu za maafande, Azam ikiilaza Prisons-Mbeya na Coastal kuichapa JKT Oljoro.
Mtibwa walioiduwaza Simba iliyokuwa ikipewa nafasi ya kutwaa taji hilo sawa na Ashanti United, itapepetana na Yanga ambayo imeonyesha kubadilika msimu huu tofauti na msimu uliopita, japo timu iliyowang'oa Ashanti United katika mechji yao ya robo faiali ya jana wanalalamikiwa kubebwa.
Kama Yanga itafuzu hatua hiyo itaweka rekodi kwa mara ya kwanza kufika hatua hiyo kubwa tangu michuano hiyo ilipoanzishwa mwaka 2008.

Tasnia ya Habari yapata pigo; Dunia mzobora hatunaye, kusikwa mchana huu

Dunia Mzobora enzi za uhai wake
TASNIA ya Habari imeendelea kupata mapengo baada ya Mwandishi  Mwandamizi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Dunia Mzobora (49) kufariki dunia ghafla asubuhi ya jana wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Taifa Muhimbili alipokimbizwa kutoka Hospitali ya Aga Khan.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana zinasema kuwa, Mzobora aliyekuwa Kaimu Msanifu Mkuu wa gazeti la Uhuru, aliyewahi pia kuwa Naibu Mhariri wa Makala wa Mzalendo alifariki saa 12 asubuhi baada ya kuumwa ghafla usiku wa kuamkia jana akiwa nyumbani kwake.
Inaelezwa kuwa, mara baada ya kumaliza kulisimamia gazeti la Uhuru toleo la jana (Jumatano), hali yake ilibadilika na kulazimisha ndugu zake kumkimbiza hospitali ya Aga Khan, lakini hali ilizidi kuwa mbaya na kuwahishwa Muhimbili na wakati madaktari wakiendelea kuokoa maisha yake aliaga dunia.
Marehemu Mzobora, aliyezaliwa April 6, 1964 Mwandege mkoani Kigoma anatarajiwa kuzikwa mchana huu katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.
Binafsi niliwahi kufanya kazi na Mzobora enzi za uhai wake wakati nafanya kazi Uhuru/Mzalendo na alikuwa ni mchapakazi, mcheshi na mwanamichezo.
Licha ya ucheshi, lakini marehemu Mzobora alikuwa makini katika kazi yake na alikuwa mmoja wa 'mabosi' wangu waliokuwa wakipenda kwa kujiweka watanashati karibu muda wote kiasi kilikuwa napenda kumuita 'Papaa'.
Mungu aiweke mahali pema roho ya marehemu Dunia Mzobora, yeye katangulia nasi tu nyuma yake na MICHARAZO inaungana na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu kwa kuwataka wawe na subira.

Super Nyamwela kutoka na Dully Sykes

KIONGOZI wa safu ya unenguaji wa bendi ya Extra Bongo, Hassan Mussa 'Super Nyamwela' amesema  yupo mbioni kupakua wimbo mpya atakaoimba na nyota wa muziki wa kizazi kipya, Prince Dully Sykes.
Akizungumza na MICHARAZO, Nyamwela alisema wimbo ambao hapendi kuutaja jina kwa sasa utarekodiwa katika studio za msanii huyo, ziitwazo Dhahabu Records za jijini Dar es Salaam.
Nyamwela alisema huo ni wimbo wa nne kuelekea kupakua albamu yake ya tatu baada ya awali kutoa 'Tumechete', 'Maneno' na kibao kinachoendelea kutamba kwa sasa wa 'Duvele Duvele'.
"Nipo katika maandalizi ya kuingia studio kurekodi wimbo wangu mwingine mpya ambao nitaimba na Dully Sykes, nao utakuwa kama Duvele kwa namna ya midundo yake, lengo kuwapa burudani mashabiki wangu," alisema Nyamwela.
Nyamwela alisema, anahofia kutaja jina la wimbo huo kwa sasa kwa madai ni mapema mno, pia akihofia kuibiwa 'idea' kutokana na kuwepo kwa mtindo wa baadhi ya wasanii kuiba kazi za wenzao na kuzitanguliza mapema hewani.
"Ningeutaja kwa sasa, lakini nahofia wasanii vilaza ambao hawaumizi vichwa kutoa kazi zao badala yake usubiri wasikie mawazo ya wenzao na kuwahi kutoa hewani," alisema.
Nyamwela aliyeanzia kwenye muziki wa disko kabla ya kuibngia kwenye makundi ya muziki wa dansi miaka ya 1990, aliwahi kutamba na albamu mbili za 'Master of the Tample na 'Afrika Kilomondo' alizoimba na wasanii wenye majina mkubwa nchini kama Ally Choki, Richard Maalifa na Sir Juma Nature.